Mama Salma Kikwete.
Na Anna Nkinda – Maelezo , Lindi
Wanafunzi wa kike wa Vyuo vya Mafunzo na Elimu ya Ufundi Stadi
(VETA) wametakiwa kutoogopa kusoma masomo magumu yanayosomwa na watoto wa kiume
kwani hata wao wanauwezo wa kufanya hivyo na kwa kujifunza kwao fani hizo
wataweza kupata ajira kirahisi.
Wito huo umetolewa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati wa
uzinduzi wa awamu ya pili ya mradi wa VETA kwa ajili ya sekta ya gesi na
mafuta ya petroli wenye madhumuni ya kuimarisha ajira kwa vijana kupitia ufundi
stadi uliofanyika katika chuo cha VETA mkoani Lindi
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo
(WAMA) akiwa chuoni hapo alitembelea karakana ya chuo hicho na kujionea
wanafunzi wakijifunza kwa vitendo ufundi wa magari, umeme, useremala
na masomo ya kompyuta wanafunzi wote katika madarasa hayo ni wa kiume
kasoro darasa la ufundi umeme ambako alimkuta mwanafunzi wa kike mmoja.
Pia katika darasa la kompyuta kulikuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wa
kike hii inaonyesha kuwa wanafunzi wengi wa kike wanapenda kusoma masomo ya
ukatibu mahsusi (muhtasi) ambayo wanaona kuwa ni rahisi kwao na
kuyakimbia yale ambayo ni magumu kwa kudhani kuwa hawawezi kusoma.
“Chuo cha VETA Lindi kina jumla ya wanafunzi 224 kati ya hao wasichana ni
63, kutokana na upatikanaji wa rasilimali zilizopo katika mikoa ya Kusini
Shirika la Madini limefadhili wanachuo 64 kati ya hao wasichana ni 11 mimi kama
mzazi na mdau wa maendeleo wa mkoa huu nauliza tuko wapi na je tutafika?,
alihoji Mama Kikwete.
Mwenyekiti huyo wa WAMA alisema makusudio ya VETA ni kuona kijana
akimaliza mafunzo yake anaweza kujiajiri lengo likiwa ni kuwaondoa vijana wengi
kutoka kwenye eneo lisilo la ajira na kupata ajira kwani si lazima mtu
aajiriwe ofisini na kuwataka wasome kwa bidii ili waweze kufika mbali.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa huo Ludovick Mwananzila alisema ugunduzi wa
gesi katika mikoa ya Kusini ni kitu kipya nchini hivyo basi wananchi bila ya
kupewa mafunzo fani hiyo inaweza kutoweka.
Alisema chuo hicho kama kitatumika vizuri kitakuwa ni mkombozi mkubwa kwa
wananchi wa mkoa huo na kuwaomba wazazi kuwa tayari kuwapeleka watoto wao choni
hapo kwani wataweza kuajiriwa au kujiajiri wenyewe pindi watakapomaliza mafunzo
yao na hivyo kujikwamua na hali ngumu ya maisha.
Mkurugenzi Mkuu wa VETA nchini Mhandisi Zebadiah Moshi alizishukuru
kampuni za British Gas ya Uingereza ambao wametoa mchango wa kuimarisha
mafunzo kwa wanafunzi katika vyuo vya Lindi na Mtwara na Voluntary
Services Organisation (VSO Tanzania) ambao ndiyo wanaratibu mafunzo hayo.
Mhandisi huyo alisema chuo hicho ndicho kinachonufaika zaidi na mafunzo
hayo kwani yataboresha mafunzo ya elimu kutokana na ushirikiano uliopo,
walimu watajengewa uwezo katika mafunzo na wanafunzi watakaomaliza katika vyuo
hivyo watakuwa na umahiri mkubwa zaidi.
Alisema,“Vyuo vyetu vitapata vifaa vya kisasa vya kufundishia na mafunzo
haya yatakuwa ya kiwango kizuri. Tunaahidi kuimarisha uhusiano uliopo na
tutasimamia na kuhakikisha kuwa uhusiano huu unatimiza malengo
yaliyokusudiwa”.
Kwa upande wao baadhi ya wanafunzi wa chuo hicho kutoka Mtwara na Lindi
ambao walitoa ushuhuda jinsi walivyoweza kunufaika na mafunzo ya VETA
walisema watu wengi wanaposikia kijana anaenda kusoma hapo wanamdharau na
kuona kuwa ameshindwa kila kitu katika maisha na kukimbilia huko jambo
ambalo si kweli kwani mafunzo wanayopewa ni mazuri na yanawasaidia katika
maisha yao.
“Tunaiomba Serikali iongeze idadi ya wanafunzi wanaojiunga na vyuo hivi
hii itawasaidia vijana wenzetu ambao tunakutana nao mitaani kipindi cha likizo,
vijana hawa ni wengi na hawana ajira ili nao waweze kupata elimu kama hii
tunayoipata sisi kwani pindi wakimaliza mafunzo yao wataweza kujiajiri au
kuajiriwa”, walisema wanafunzi hao.
Mradi huo ambao ni wa miaka miwili kuanzia mwaka 2013 hadi 2015
umeanzishwa na kuendelezwa na kampuni ya British Gas ya Uingereza, Voluntary
Services Organisation (VSO Tanzania) , wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi
Stadi, Serikali ya Uingereza kupitia idara yake ya Maendeleo ya Kimataifa(DFID)
British Council na VETA utatoa mafunzo kwa zaidi ya wanafunzi 224 kutoka kwa
walimu wenye uzoefu wa kimataifa kwa kushirikiana na walimu wao na kukifanya
chuo hicho kufikia viwango vya kimataifa.
Pia utaboresha matumizi ya lugha ya kiingereza kwa walimu 15 kwa sababu
vijana watakaowafundisha wanatarajiwa kuajiriwa katika makampuni ya ndani na ya
kimataifa, hivyo lugha ya kiingereza ni nyenzo muhimu ya mawasiliano na walimu
wanne kutoka karakana nne za chuo hicho watajengwa uwezo kwa kupewa kozi
zenye hadhi ya kimataifa ili wapate tuzo zinazotambulika kitaifa.
Awamu ya kwanza ya
mradi huo ulizinduliwa mwishoni mwa mwaka 2012 katika chuo cha Ufundi VETA
Mtwara na Makamu wa Rais Dk. Gharib Bilal.


0 comments:
Post a Comment