Ndugu Wanahabari,
NILIPOKUWA
katika ziara ya bara la Ulaya kati ya Oktoba 21 mpaka Novemba 2 mwaka huu
(2013), nilipokea kwa njia ya barua pepe ripoti inayoitwa "Taarifa ya Siri
ya Chadema" ambayo pia ilikuwa imesambazwa katika mitandao mbalimbali ya
kijamii.
“Taarifa
ya Chadema inasema kwamba chama hicho (chama changu) kilikuwa kimechunguza
mwenendo wangu tangu mwaka 2008 hadi 2010 na kubaini kuwa mimi napokea fedha
kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kuivuruga Chadema.
Ripoti
hiyo ilinihusisha pia na mwananchi raia wa Ujerumani, Andrea Cordes ambaye, kwa
mujibu wa ripoti hiyo, alinisaidia kupokea na kuhifadhi kiasi cha dola 250,000
za Marekani kupitia kwenye akaunti yake binafsi.
Taarifa hii
ya kutunga na iliyojaa uongo wa kiwango cha kutisha, imenifadhaisha,
kunisikitisha na kunikasirisha.
Taarifa hii iliibuliwa katika
kipindi ambacho nilikuwa safarini kutetea haki za Watanzania na Waafrika ambao
utajiri wao wa rasilimali unafaidiwa na watu wachache waliohifadhi mali katika
nje za nje na pia kupigania makampuni ya mataifa tajiri yalipe kodi stahiki katika
nchi zetu.
Pengine lengo la ripoti hiyo lilikuwa ni kutaka
kunipoteza kutoka katika nia na dhamira yangu ya dhati ya kutaka Watanzania
wafaidike na utajiri wao. Muda ambao watunzi wa ripoti hiyo waliamua kutoa
taarifa yao unazua maswali mengi kuliko majibu.
Nafahamu
kwamba mimi ni mwanasiasa ambaye nimekuwa mlengwa (target) wa mashambulizi
kutoka kwa makundi mbalimbali ya wanasiasa na vikundi vyao.
Kama mwanasiasa,
niko tayari kupokea changamoto zozote zinazokuja na uanasiasa wangu.
Hata
hivyo, ambacho sitakubali ni kwa watu kutumia jina langu na uanasiasa wangu
kunichafua mimi binafsi na watu wengine wasiohusika kwa sababu ya kutaka
kutimiza malengo yao ya kidhalimu.
Raia huyo wa Kijerumani
tayari amekana kuhifadhi fedha zangu. Kwa maelezo yake kwa baadhi ya viongozi
wa Chadema amekana kuwa na akaunti inayotajwa na amekana pia kuwepo nchini
Ujerumani katika siku na wakati uliotajwa kwenye ripoti hiyo.
Ripoti
hiyo imemtaja pia mtu kama Dk. Charles Kimei, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB
ikidai kwamba nilikutana naye na alishiriki kwenye igizo hilo la kunipa fedha.
Niseme
mapema kwamba tangu kuzaliwa kwangu sijawahi hata mara moja kukutana na Dk.
Kimei popote pale ndani au nje ya nchi.
Kumuingiza mtu ambaye amejenga jina
lake kwenye taaluma ya kibenki kwa sababu tu ya lengo ovu la kumchafua Zitto
Zuberi Kabwe si uungwana bali ni unyama.
Kutokana na uchafuzi
huu wa wazi dhidi ya taswira yangu binafsi na watu wengine walioingizwa kwenye
mkumbo huu, nimeandika rasmi kwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk.Wilbrod Slaa
kumwomba athibitishe kwamba kinachoitwa Taarifa ya Siri ya Chadema ni kweli ni
taarifa ya chama au kiikanushe ili niweze kuchukua hatua za kisheria dhidi ya
waandishi wa hekaya hiyo.
Cha ajabu, nimepokea ujumbe wa
kutishiwa maisha kutoka kwa mtu anayejiita Theo Mutahaba na kuahidiwa KUPOTEZWA
endapo nitaendelea na jitihada zangu za kupambana na ufisadi na kutafuta haki
kwa Watanzania wote pasipo kujali tofauti zao za kiitikadi, kikanda, kikabila
na kidini.
Natarajia kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya
wote ambao wamehusika na utungaji na uenezi wa taarifa hii.
Nitahakikisha
kwamba wahusika wanatafutwa na kufunguliwa mashitaka stahiki ya upotoshaji na
kuchafuana.
Ni matarajio yangu kwamba wale wenye mapenzi mema
na Tanzania, mimi binafsi na utawala wa sheria, wataelewa nia yangu ya kutafuta
haki katika suala hili.
Nimeamua kujitolea maisha yangu kwa
ajili ya Watanzania na kama alivyopata kusema Rais Mstaafu wa Afrika Kusini,
Nelson Mandela; “Struggle Is My Life.”
Forward Ever, Backward
Never- Kwame Nkrumah
Zitto Kabwe (Mb)
10/11/2013
0 comments:
Post a Comment