Tanzania imeungana na nchi
nyingine duniani kuomboleza kifo cha Rais wa zamani wa Afrika Kusini Mzee
Nelson Mandela aliyefariki dunia jana nyumbani kwake mjini Johannesburg baada
ya kuugua ugonjwa utokanao na maambukizi ya mapafu.
Rais Jakaya Kikwete
amemtumia salamu za rambirambi Rais Jacob Zuma wa Afrika ya Kusini na kupitia
kwake, kwa mkewe Bi. Grashia Machel, wanafamilia wote na wananchi wote wa
Afrika ya Kusini kufuatia kifo hicho cha Mzee Mandela.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa
na kurugenzi ya mawasiliano ya rais Ikulu, rais Kikwete ameuelezea msiba wa
Mzee Mandela kama msiba wa Afrika kwa ujumla hasa kutokana na mchango
uliotolewa na kiongozi huyo katika harakati za ukombozi na kuongeza kwamba
Afrika ya Kusini, Afrika na dunia kwa ujumla imepoteza mtu mashuhuri na shujaa
mkubwa wa Karne ya 20 na 21.
Rais Kikwete amemuelezea
Mzee Mandela kuwa ni kielelezo cha aina yake kwa wanadamu kwa moyo wake wa
kusamehe, huruma na upendo uliomuwezesha kuwaunganisha wananchi wa Afrika ya
Kusini kuwa taifa moja baada ya kipindi kirefu cha mapambano dhidi ya ubaguzi
wa rangi.
Kufuatia kifo hicho Rais
Kikwete ametangaza siku tatu za maombolezo kuanzia leo tarehe 6 hadi 8 Desemba,
2013, ambapo katika kipindi hicho bendera zote zitapepea nusu mlingoti.
anchi.
0 comments:
Post a Comment