KATIKA maisha ni jambo la kawaida kupata misukosuko,
makwazo, kuumizwa na mambo yanayofanana na hayo.
Kwa sababu tumeumbwa tofauti, wako walioumbwa
kushughulika na maisha ya wenzao lakini siku zote uko mwisho wao, hivyo hupaswi
kuruhusu wakukatishe tamaa.
Kwa nini nasema hivi, wako watu wamepitia magumu mengi
katika maisha yao au wanapitia magumu, lakini wanapoyavuka haya, hawataki
kuachilia na kusonga mbele, wanasahau kushughulika na maisha yao wanatazama ya
nyuma.
Kwa wale waumini wa dini ya Kikristo, ndani ya Biblia
kuna hadithi ya Yusufu ambaye aliuzwa na ndugu zake, baadaye alifungwa kwa
kusingiziwa. Lakini hayo yote hayakumzuia kufanya kazi kwa bidii na kufikia
ndoto zake.
Kama angetaka angewaweka ndugu zake waliomuuza moyoni,
alikataa hilo hakuweka kinyongo na alipopata madaraka aliwasaidia na kuwatunza
na hatusomi kuwa alilipiza kisasi mke wa Potifa.
Hali yake ya kuwa mfungwa haikumzuia kuja kutawala.
Ndivyo hivyo hivyo kwako leo, maisha yako ya nyuma hayana nafasi katika maisha
yako ya sasa na yajayo.
Eti kwa sababu umeishi kwa kuteseka sana,
umenyanyasika, umesimangwa basi wewe uwe mnyonge na wa kusaidiwa tu, hapana.
Kama bado uko hai una nafasi ya kuboresha maisha yako, haijalishi umepitia
mapito na changamoto ngumu kiasi gani, kumbuka bado unayo maisha mbele yako.
Wako wanaobakia kulalamika kwa kutopelekwa shule na
wazazi, wako waliopitia mikononi mwa mama wa kambo na kuteswa. Wako
waliofelishwa na walimu, wako waliotengana na ndugu zao na kila aina ya
changamoto za dunia hii lakini hayo yote ni mapito, ili mradi Mungu bado kakupa
pumzi songambele usiyatazame hayo.
Sio wakati wa kulalama na kuacha kutumia fursa
uliyonayo hata kama ni ndogo kuboresha maisha yako, kumbuka sio wewe peke yako
kila mtu amepitia na anapitia matatizo na mitihani ya dunia hii iliyojaa
kashikashi za kila aina.
Mazingira hayo magumu hayatupi kibali cha kulaumu
wengine na kukosa furaha bila sababu. Kama ulianguka simama, anza kutembea na
mwisho utakimbia, ni jambo la hatua na uvumilivu lakini zaidi ukiwa na dhamira
ya kushughulika na maisha yako ili yalete maana.
Lakini ukiamini kuwa Mungu yupo upande wako daima
utakuwa mwenye furaha, kuchangamka na mwenye matumaini. Kumbuka Mungu anaweza
kukuinulia watu wa kukusaidia, na watu hao hawalazimiki kukusaidia hivyo
chochote unachofanyiwa na mtu kipokee kwa moyo wa shukrani na kuzidi
kumwangalia muumba wako.
Tena hapa wale wakatisha tamaa, wenye wivu na
wasiopenda kuona mwingine anaishi maisha ya amani na furaha ndio wataibuka kwa
vikundi kukusengenya, na kukusemea kila lililo baya, kwa sababu furaha yao ni
kukuona ukiendelea kuteseka ama kunyanyasika.
Kumbuka kelele za chura hazimzuii tembo kunywa maji,
kama una dhamira ya kushughulika na maisha yako na kuyafanya yenye maana hapa
duniani, acha kusikiliza kelele za watu hao ambao mara nyingi ni wanakatisha
wengine tamaa wakati wao wenyewe maisha yao matatizo matupu.
Unachotakiwa kufahamu ni kuwa kila mtu na maisha yake,
tengeneza maisha yako kwa manufaa yako mwenyewe na sio kufurahisha wanadamu
wengine wasiokuwa na shukrani na wala hawapendi kukuona ukifanikiwa katika
maisha yako.
0 comments:
Post a Comment