WANAFUNZI wa Shule ya Seminari ya Kiislamu ya Mivumoni
jijini Dar es Salaam, husoma kwa siku tano kama kawaida, lakini `wikiendi’ yao
huwa siku za Alhamisi na Ijumaa. Hii ina maana kuwa siku za masomo huanza
Jumamosi na kuendelea Jumapili, Jumatatu hadi Jumatano.
Kwa kawaida, siku za masomo wakati ambapo shule zinakuwa
hazijafungwa huwa Jumatatu hadi Ijumaa, isipokuwa kwa siku za sikukuu za
kitaifa.
Shule hiyo ya kutwa iliyopo katika Manispaa ya Kinondoni
eneo la Kinondoni B, iko chini ya msikiti wa Mtambani, ina wanafunzi wa kidato
cha kwanza mpaka kidato cha nne.
Hata hivyo, shule hiyo imetakiwa kubadili utaratibu wake wa
siku za masomo, kwa maelezo kuwa unakwenda kinyume na taratibu za Wizara ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Imeelezwa kuwa utaratibu huo ni ukiukwaji mkubwa wa taratibu
na kanuni za nchi, kwani kwa kufanya hivyo shule hiyo inawakosesha watoto haki
yao ya msingi.
Akizungumzia suala hilo, Kaimu Mkaguzi Mkuu wa Elimu Kanda
ya Dar es Salaam, Suzan Samuel alisema shule hiyo tayari imeshauriwa mara
mbili, kubadili utaratibu huo ili kuendana na sheria zilizopangwa.
Alisema shule zote husajiliwa na Wizara ya Elimu, hivyo
kutakiwa kufuata taratibu zilizopangwa na wizara hiyo, ikiwemo ya kufanya kazi
kati ya Jumatatu mpaka Ijumaa, na si vinginevyo.
"Tulipata taarifa kuwa wana utaratibu huo, wakaguzi
walikwenda kutembelea mara ya kwanza, kweli tukakuta watoto hawasomi Alhamisi
na Ijumaa, tukawashauri lakini bado wanaendelea," alisema.
Alisisitiza kuwa ni kosa kubwa kwa wanafunzi kutosoma katika
siku ya Alhamisi na Ijumaa.
"Kusoma Jumamosi na Jumapili hiyo ni juu yao, lakini
kosa kubwa ni kutosoma siku hizo mbili za kazi, ambazo sheria yetu inasema
hivyo," alisema.
Alisema tayari wamewapelekea barua ya kujieleza, kwa nini
wasichukuliwe hatua kwa kukiuka sheria zilizopo, lakini bado hawajajibu.
Alisema pia barua nyingine wamepeleka kwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, kwa kuwa
na yeye ndiye mtendaji mkuu.
"Taratibu ziko wazi na zinajulikana kuwa shule zote
zifuate sheria zilizopo, hata kama ni shule za seminari. Nadhani hata
walipokwenda kuomba usajili wizarani, walikiri kufuata sheria, lakini sasa
wamebadilika," alisema.
Alisema kama wangekuwa wamepata kibali kutoka wizarani,
ingekuwa haina tatizo, lakini wao wameamua kufanya kienyeji.
Alisema kama kuna shule nyingine, zimejiamulia utaratibu
wao, zihakikishe zinafuata sheria za nchi. Mkuu wa Shule hiyo, Dadi Hemed,
akizungumza na gazeti hili, alisema hawaoni tatizo kwa wao kupumzika Alhamisi
na Ijumaa, bali kitu cha muhimu ni kusoma siku tano, jambo ambalo wanalifanya.
Aliliambia gazeti hili kuwa wameamua kupumzika siku hizo
mbili, kwa madai ya wanafunzi wa kidato cha pili na nne hufanya mitihani ya
majaribio ya ndani ya shule.
"Kikubwa tunasoma siku tano kama shule zingine, tofauti
ni hiyo ndogo tu, lakini hatuoni kama tuna tatizo kupumzika siku hizo na kusoma
Jumamosi na Jumapili," alisema Hemed.
Hemed alikiri kupokea barua ya kutaka wajieleze, lakini
alisema kuwa bado wanaifanyia kazi. Alisisitiza kuwa hakuna tatizo kupumzika
siku hizo mbili.
Baadhi ya wanafunzi waliohojiwa kwa masharti ya kutotajwa
majina gazetini, walikuwa na maoni tofauti.
Mmoja wao anayesoma kidato cha pili, alisema utaratibu huo
hauko sawa ila kwa kuwa ni maamuzi yamepitishwa haina jinsi inabidi wakubaliane
nao.
Alisema kimsingi inatakiwa waendane na shule zingine, lakini wanashangaa
wao kupumzika siku hizo mbili.
“Wakati mwingine inatia uvivu kwenda shule, unaamka Jumapili
asubuhi wenzako wamelala wewe inatakiwa kwenda shule. Inaweza ikachangia utoro
kwa wanafunzi.
Mwanafunzi mwingine anayesoma kidato cha nne, alisema kwa sasa
utaratibu huo wanauona ni wa kawaida, lakini unawapa taabu wageni wanaoanza
shule hiyo au kuhamia.
0 comments:
Post a Comment