Songea.
Watu
zaidi ya 270 wa Kijiji cha Litapwasi, Wilaya ya Songea, mkoani Ruvuma wamelazwa
wengi wao wakiwa na hali mbaya katika Zahanati ya Lyangweni na Hospitali ya
Misheni ya St Joseph, Peramiho baada ya kunywa togwa inayosadikiwa kuwa na
sumu.
Tukio hilo lilitokea juzi mchana kwenye
sherehe ya Kipaimara kwa mtoto Dickson Nungu (14) na kuzua hofu kubwa kwa
wakazi wa kijiji hicho ambao wanaonekana kutoamini kilichotokea.
Wingi wa wagonjwa hao umesababisha zahanati
hiyo kuelemewa na kiasi cha wengine kulazwa chini kwenye udongo, barazani na
kwenye miembe wakisubiri kupatiwa huduma ya kwanza.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Mihayo
Mskhiela alisema polisi inawashikilia watu watatu kuhusiana na tukio hilo na
vinywaji na mabaki ya chakula kilicholiwa vimezuiliwa huku sehemu ikichukuliwa
sampuli ili kupelekwa kwa Mkemia Mkuu kwa uchunguzi zaidi.
Alisema waliopatiwa matibabu na kuruhusiwa ni
watu 50 huku 190 wakiwa bado wanatibiwa Lyangweni na wengine 30 wakilazwa
Peramiho. Hata hivyo, Kamanda Mshkhiela alisema walioathirika wanaendelea
kuongezeka.
Mtoto Nungu, ambaye ni mwanafunzi wa darasa la
sita katika Shule ya Msingi Litapwasi, alipata Kipaimara hicho na mara baada ya
chakula cha mchana, waalikwa walipewa pombe za kienyeji na wengine togwa. Baada
ya muda mfupi, waliokunywa togwa na chakula, kila mmoja kwa wakati wake alianza
kujisikia maumivu ya tumbo na kuharisha mfululizo huku wengine wakitapika damu.
Mama mzazi wa kijana huyo, Philbeta Ngonyani
(36), ambaye pia amelazwa katika Hospitali ya Misheni Peramiho alisema:
“Nimefikishwa hospitalini jana (juzi) saa nane usiku nikiwa sijitambui kutokana
na maumivu makali kwa kuharisha mfululizo baada ya kunywa togwa.”
Akielezea tukio hilo alisema, anakumbuka siku
moja kabla ya tukio, (Jumamosi iliyopita) yeye na wenzake (majirani)
walishirikiana kupika togwa na walianza kazi hiyo saa sita adhuhuri na kumaliza
saa 10 jioni na kisha kuiweka katika chumba kimoja ili ipoe kisha walimkabidhi
ufunguo wa chumba hicho mtu aliyemtaja kuwa ni jirani yao, Ridhiwan Shawa ili siku
ya sherehe mtu atakayehitaji kinywaji ampatie.
Alisema, juzi mchana mara baada ya mwanaye
kutoka kanisani, waalikwa walifika nyumbani kwake wakiwa na watoto wao na
baadhi ya ndugu na jamaa zao kwa ajili ya kujumuika kumpongeza kijana huyo na
vyakula mbalimbali vilipikwa kama wali, pilau na ugali.
Alisema mara baada ya kula, vinywaji
vilitolewa na kijana wake na baadhi ya watu walipatiwa soda na wengine waliomba
pombe za kienyeji na togwa. “Waliokunywa pombe na soda hawakudhurika lakini
waliokunywa togwa wengi walianza kusikia maumivu ya tumbo na kuanza kuharisha
na kutapika mfululizo na wengine kuharisha damu, baadhi walirudi nyumbani na
wengine walikimbilia zahanati.”
Alisema yeye, mumewe Ines Nungu pamoja na
kijana wao mwingine, Matson wanaumwa tumbo, kuharisha na kutapika.
Jirani ambaye pia amelazwa, Aloysia Ngonyani alisema alifikishwa
hospitalini hapo juzi usiku wa saa saba akiwa na maumivu makali ya tumbo huku
akihara na kutapika baada ya kunywa togwa.
0 comments:
Post a Comment