Image
Image

Ajira kwa vijana yaelezwa bado nichangamoto kwao katika kujikomboa kiuchumi




Na Mwandishi Wetu
WIMBI kubwa la kuwa na vijana wasiokuwa na kazi limeelezwa kuwa tatizo duniani kote na serikali mbalimbali zinatakiwa kuliangalia hilo kwa undani na kulitatua.

Kauli hiyo imetolewa na Mratibu wa Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini na Mwakilishi wa shirika la maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Alvaro Rodriguez.

Mratibu huyo alisema hayo katika mazungumzo yake na Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari (UTPC) Abubakar Karsan.

Alisema ukosefu wa kazi kwa sasa ni tatizo la kijamii na kwamba, shauri hilo lisipoangaliwa kwa makini linaweza kuwa chanzo cha matatizo makubwa ya usalama na amani katika taifa.

Alvaro Rodriguez ambaye alifika katika ofisi za UTPC kuangalia mambo yanayofanyika katika ofisi hiyo wakati akiwa ziarani Mwanza wiki iliyopita, alisema kama tatizo la ajira litaendelea kuwapo, vijana wanaoathirika wanaweza kufikiria njia nyingine isiyo ya kistaarabu kufanikisha mambo yao.

Alisema Umoja wa Mataifa unaendelea kushirikiana na serikali mbalimbali kuhakikisha kwamba tatizo la ajira kwa vijana linamalizwa ili jamii isiingie katika mtafaruku utakaokosesha amani na usalama na hivyo kusimamisha maendeleo yaliyofikiwa katika jamii.

Bila kutaja makundi ya kigaidi yanayotikisa dunia kwa sasa kama Al - Qaeda na washirika wake Boko Haram, Al - Shabab, Islamic State of Iraq na Levant (ISIL) alisema makundi mengi ya kigaidi duniani yanatokana na vijana kutojua wafanye nini na mazingira waliyonayo na hivyo kuwa rahisi kushawishika.

Alisema makundi ya hatari mara nyingi ni ya vijana ambao wanashindwa kupata riziki au hawajui wafanye nini kupata riziki na serikali zimewaacha bila kuwaangalia.

Aidha alisema Umoja wa Mataifa utaendelea kusaidia kuhakikisha kwamba masuala muhimu yanayowezesha maendeleo kama demokrasia yanazingatiwa ili kuiwezesha jamii kufanya maamuzi sahihi ya vile wanavyotaka kupanga maendeleo yao.

Alisema Demokrasia huwezesha wananchi kujua namna wanavyoweza kutengeneza mustakabali wao katika masuala ya ustawi wa jamii na maendeleo huku haki zao za msingi zikilindwa.

Mapema Mkurugenzi Mtendaji wa UTPC, Bw. Karsan alimwambia mratibu huyo mambo ambayo yamefanywa na umoja huo na changamoto walizokumbana nazo kwa kuzingatia mpango mkakati wake wa mwaka 2011-2013.

Umoja huo ambao ulianzishwa mwaka 1996 na kusajili na wizara ya mambo ya ndani kama taasisi isiyokuwa ya kiserikali (NGO) mwaka uliofuata, umefanikiwa kuanzisha mfuko wa kusaidia vyombo vya habari kwa jina la Daudi Mwangosi, aliyekuwa Mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa habari wa Iringa (IPC).

Aidha alimwambia kwamba wamefanikisha mafunzo ya kuongeza umahiri wa uandishi wa habari na pia kuwaelezea umma juu ya uhuru wa vyombo vya habari.

Pia alielezea mafanikio yaliyopatikana katika kampeni za kuelimisha umma na kuelewana miongoni mwa wadau mbalimbali wa sekta ya habari.

Alisema hata hivyo bado wanaendelea na kampeni yao kutaka mabadiliko ya malipo kwa waandishi wa habari wanaojitegemea ambao ndio wanatoa mchango wa asilimia 75 hadi 80 za habari zinazotangazwa au kuchapishwa.

Aidha wanaendelea kutoa mafunzo ya kanuni na maadili kwa waandishi wa habari na kuendelea kukabiliana na tatizo la usalama katika mpango mkakati wa mwaka 2015 – 2019.

Katika ziara hiyo ya kanda ya Ziwa, mratibu huyo aliambatana na mshauri mwandamizi wa masuala ya haki za binadamu Dk Chitralekha Massey na Mtaalamu wa mawasiliano wa umoja huo hapa nchini HoyceTemu.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment