Milio ya risasi imesikika leo katika Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Kongo, ambako wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kinshasa, wanaandamana
kupinga pendekezo la marekebisho ya sheria inayoweza kuchelewesha uchaguzi wa
rais mwakani.
Maandamano hayo ya umma yaliyoitishwa na
vyama vya upinzani kwa lengo la kupinga hatua ya bunge kupitisha kipengele cha
katiba kitakachorefusha uchaguzi wa rais wa mwaka ujao wa 2016, ambacho
kinajadiliwa katika vikao vya Baraza la Seneti. Upinzani unamtaka Rais Joseph
Kabila, ambaye amekuwepo madarakani kwa miaka 14 sasa, kuachia nafasi hiyo
pindi kipindi chake kitakapomalizika mwaka ujao wa 2016.
Milio hiyo ya risasi ilisikika wakati ambapo
mamia ya wanafunzi waliokuwa wakiandamana leo huku wakipiga kelele wakisema
''Kabila ondoka madarakani!'', walipokutana na kundi dogo la askari polisi.
Katika eneo la Ndjili, vijana waliliharibu gari moja la polisi.
Mjini Brussels, Ubelgiji, kiongozi wa
upinzani, Etienne Tshisekedi, amewasihi watu wa Kongo kufanya kila jitihada
kuundoa madarakani ''utawala usio na manufaa.'' Tshisekedi ambaye anatibiwa
mjini humo, amewataka polisi na wanajeshi kuwalinda raia na kutotekeleza amri
wanazopewa, za kuwaua watu wasio na silaha.
Taarifa iliyotolewa na shirika la haki za
binaadamu la Kongo, imeeleza kuwa watu 28 wameuawa tangu siku ya Jumatatui
katika maandamano hayo ya kuipinga serikali. Hata hivyo, maafisa wa Kongo
wanasema kuwa idadi ya watu waliouawa ni watano.
Watu 20 wanashikiliwa na jeshi na polisi
Msemaji wa Serikali ya Kongo, Lambert Mende,
amesema askari polisi wawili waliuawa kwa risasi siku ya Jumatatu na wengine
wawili waliuawa na waporaji. Polisi na jeshi linawashikilia kiasi watu 20
waliokuwa wanaandamana.
Akizungumzia kuhusu mvutano huu wa pendekezo
la mabadiliko ya kifungu cha katiba, yatakayoweza kuuchelewesha uchaguzi wa
rais mwaka ujao 2016, kati ya serikali ya Kongo na upinzani, mchambuzi wa
masuala ya kisiasa nchini Kongo, Fidel Bafilemba, anasema nia ya Rais Kabila ni
sawa na kutaka kuizamisha nchi ya Kongo.
Bafilemba ambaye alikuwa akizungumza na Idhaa
ya Kiswahili ya DW, amesema, ''Hauwezi kuongoza nchi kwa zaidi ya miaka 14 na
ushindwe kujenga jeshi, ushindwe kuendeleza siasa, ushindwe kujenga uchumi,
kila kitu Kongo hakiendelei. Na wakati katiba inakwambia wewe una mihula miwili
tu na umefika mwisho, sasa Kongo leo inaelekea katika njia mbaya sana, inakuwa
kama vile boti inayotaka kuzama.''
Hata hivyo, wakosoaji wanasema hatua hiyo ni
njama ya Rais Kabila kutaka kuendelea kubakia madarakani. Wanasema serikali
inataka kuifanyia marekebisho sheria hiyo ya uchaguzi na kuamuru lifanyike
zoezi la kuwahesabu watu nchini humo kabla ya uchaguzi.
Rais Kabila, mwenye umri wa miaka 43,
aliingia madarakani Januari mwaka 2001, baada ya baba yake Laurent Kabila
kuuawa, na alishinda katika uchaguzi wa mwaka 2006 na 2011. Katiba ya Kongo
inamzuia Kabila kugombea katika uchaguzi wa urais kwa muhula wa tatu, hapo
mwakani.
0 comments:
Post a Comment