Wanafunzi kadhaa wamejeruhiwa nchini Kenya baada ya jeshi la polisi
nchini humo kutumia mbwa na mabomu ya kutoa machozi kwa minajili ya
kuwatawanya wanafunzi wa shule ya msingi ya Lang'ata iliyoko jijini
Nairobi, walioandamana kupinga kitendo cha kunyang'anywa uwanja wao wa
michezo uliouzwa kwa mwekezaji binafsi.
Taarifa zinasema kuwa, wanafunzi hao wenye hasira na wengineo
wakionekana kubeba fimbo na marungu, waliangusha ukuta na uzio mpya
uliojengwa kutenganisha shule yao na uwanja huo. Taarifa hiyo imeeleza
kuwa, machafuko hayo yametokea baada ya wanafunzi kurejea shuleni
kufuatia kumalizika mgomo wa wiki mbili wa waalimu wa shule za umma na
kukuta kiwanja chao cha michezo kimezungushiwa uzio.
Mbunge Kenneth Okoth amesema kuwa, makumi ya wanafunzi wamejeruhiwa
na kulazwa hospitalini, kutokana na askari polisi kutumia nguvu kupita
kiasi na mabomu ya kutoa machozi dhidi ya wanafunzi hao. Naye Raila
Odinga kiongozi wa mrengo wa CORD amekosoa vikali utumiaji wa nguvu
kupita kiasi uliofanywa na jeshi la polisi dhidi ya wanafunzi. Taarifa
zinaeleza kuwa, baadhi ya wanaharakati wametiwa mbaroni kwa kuwashawishi
wanafunzi kufanya vurugu hizo.
0 comments:
Post a Comment