MKUU wa Wilaya ya Kinondoni , Paul Makonda (pichani) amesema wanaobeza uwezo wake kiutendaji baada ya kuteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kushika wadhifa huo, wasubiri waone atakavyokuwa.
Aidha, ameweka wazi kile anachoamini anashutumiwa na kubezwa na watu kuhusu uteuzi huo na kusema wanaofanya hivyo, wanafahamu kwamba masuala yao kadhaa ndani ya wilaya hiyo yanayokwenda kinyume na taratibu, hayatafanikiwa.
Akiendelea kujibu wanaoshutumu uteuzi wake kupitia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari, alisema kwa sasa hawezi kutoa ahadi ni nini atafanya isipokuwa, anasubiri kuingia ofisini.
Akihojiwa katika kipindi cha asubuhi cha Redio ya Clouds, alisema pia anamsikiliza Rais atakachomwambia afanye kwa kuwa yeye ni mwakilishi wake wilayani humo.
Akizungumzia kuhusu taarifa za kupata nafasi hiyo kuwa gumzo katika jiji kuliko wakuu wengine wa wilaya, alisema inaonesha ni kwa jinsi gani watu wanatambua utendaji wake.
Alisema alipata taarifa za uteuzi huo wakati akitoa mada katika kikao cha kazi cha Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) na kushangaa watu wakipeana taarifa.
“Kuna watu wanabeza uteuzi wangu kwa kuonekana nimepewa wilaya kubwa. Nataka kuwaambia wasubiri waone tu,” alisema na kutaka Watanzania kuacha tabia ya kumjadili mtu au jambo bila kufahamu vizuri.
Alisisitiza kuwa Watanzania wamekuwa na tabia ya kushabikia jambo wasilolijua au mtu wasiyemjua kwa kufuata mkumbo; jambo ambalo siyo zuri ni vyema kufahamu kwanza ndipo uweze kusema.
Akizungumzia baadhi ya vyombo vya habari vilivyotoa taarifa za uteuzi wake kwa kumdhihaki, alisema wamefanya hivyo kwa maslahi yao ya kuuza.
Pia alielezea uteuzi wake umekuwa gumzo, kutokana na uwezo wake wa kazi katika UVCCM pamoja na uwezo wake kwenye Bunge Maalumu la Katiba.
Uteuzi wa Makonda ambao umefanywa na Rais Kikwete, unaonesha kuwashitua wengi; hali ambayo imefanya watu wengi kumbeza hasa kupitia mitandao ya kijamii.
Baadhi ya wanaobeza, wanadai kwamba Makonda hana sifa ya kuongoza wilaya kubwa kama Kinondoni, ambayo ina changamoto na migogoro mingi ya ardhi.
Makonda ambaye ni Katibu wa Chipukizi na Uhamasishaji wa UVCCM, jina lake limekuwa kubwa hivi karibuni baada ya kutuhumiwa kushiriki kuvuruga mdahalo ulioandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere, tuhuma alizokanusha.
Pia, kujitokeza kwake hadharani kumpinga mmoja wa watu wanaotajwa kuwania urais, kuliongeza jina hilo kuwa maarufu. Maisha ya Makonda pia ambaye baada ya kushindwa Umakamu Mwenyekiti wa Taifa wa UVCCM, alitoa shutuma kuhusu uchaguzi huo na baadaye alirejeshwa ndani ya umoja huo kwa kupewa nafasi anayoshikilia sasa ya ukatibu wa uchipukizi na uhamasishaji.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment