TAKRIBANI miaka 15 imepita tangu ilipotokea ajali katika kijiji cha Idweli wilayani Rungwe mkoa wa Mbeya, iliyosababisha vifo vya watu walioungua wakichota petroli kwenye gari lililopinduka.
Hata hivyo, tukio la namna hiyo limejirudia tena kijijini hapo na safari hii watu wawili, wamekufa na wengine 18 kujeruhiwa wakati wakichota mafuta kwenye gari lililopinduka. Lori hilo lilikuwa likisafirisha mafuta kutoka Dar es Salaam kwenda Malawi.
Lilipinduka kijijini hapo juzi. Vifo hivyo viwili vya wakazi wa kijiji hicho, Maria Pajela (18) na Wiliam Pascal (38), vimetonesha makovu ya huzuni ya ndugu na jamaa wapatao 40 waliopoteza maisha na kulazimu miili yao kuzikwa kaburi moja, kutokana na kuharibika zaidi na kushindwa kutambuliwa.
Akitoa taarifa juu ya ajali ya juzi saa 3 usiku, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi alisema waliofariki na waliojeruhiwa, walikuwa katika harakati za kuiba mafuta kutoka katika gari aina ya Scania lenye namba za usajili T 891 AQZ likiwa na tela lenye namba T 821 ARF.
Alisema gari hilo mali ya Ailis Sanga, lilipakia petroli yenye ujazo wa lita 41,000, likitoka Dar es Salaam kwenda Malawi. Lilikuwa likiendeshwa na Zawadi Nyato (46) mkazi wa Sae jijini Mbeya akiwa na utingo wake, Frank Yohana (24) mkazi wa Mbozi.
Baada ya kufika kijijini hapo, liliacha njia na kupinduka. Dereva na utingo waliokolewa na kupelekwa kituo cha Polisi Kiwira kupata fomu namba tatu ya kwa ajili ya matibabu.
Kamanda alisema baadhi ya wakazi, walivamia lori hilo na kutoboa tangi la mafuta, hali iliyosababisha mafuta kuanza kumwagika na kusambaa maeneo mbalimbali ikiwemo kwenye makazi ya watu.
Kwa mujibu wa kamanda, watu hao hawakujali hatari iliyokuwa ikiwakaribia, badala yake waliendelea kukinga mafuta kwa kutumia vyombo vyao zikiwemo ndoo, madishi, karai na madumu.
“Wakati wakiendelea na harakati za wizi huo,wakazi hao walijikuta wakiwa katika moto mkubwa baada ya lori hilo kulipuka na hapo ndipo wawili kati yao wakapoteza maisha na waliosalia kujeruhiwa vibaya,” alisema Kamanda.
Alitaja majeruhi katika ajali hiyo, ambapo wanaume ni 13 na wanawake watano ni Shukuru Kanzale (21), Nuru George (30), Asante Boniface (38), Joseph Jamson (18), Joseph Paschal (30), Siza Kanesa (22),Alex Daud (35), Oscar Yosia (23), Traiphon Moasi (37) na Samson Mbwila (29).
Majeruhi wengine ni Veronica Elia (30), Dora Michael(35), Rabsen Ayub (26), Wasiwasi Spika (32), Asia Anon (20), Bahati Kyando (23),Christopher Erasto(32) na Melisa Sanane (50) wote wakazi wa kijiji cha Idweli.
Kati ya majeruhi hao, 16 wamelazwa katika Hospitali ya Misheni Igogwe na wawili wamelazwa Hospitali ya Serikali Makandana, Tukuyu na hali zao zinaendelea vizuri.
Katika tukio la mwaka 2000 katika kijiji hicho cha Idweli, gari lililohusika lilikuwa likitoka Dar es Salaam kwenda Malawi. Lilianguka kijijini hapo, kutokana na utelezi katika mteremko unaoishia kwenye kijiji hicho.
Tukio lingine la watu kuungua moto nchini, kutokana na kutaka kujipatia mafuta ya bure, lilitokea mwaka jana katika eneo la Mbagala Rangi Tatu, jijini Dar es Salaam la mwaka 2014.
Watu wanne walipoteza maisha na wengine 21 kujeruhiwa vibaya baada ya kwenda kuchota mafuta yaliyokuwa yanamwagika wakiwa na ndoo, vidumu vya lita tano na vyombo vingine bila kuchukua hadhari.
0 comments:
Post a Comment