MWENYEKITI wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT) Dk Didas Masaburi amesema jumuiya hiyo itapigana kufa au kupona kuona Tanzania inabadili mfumo wa sasa wa uendeshaji wa serikali unaolenga kuifanya serikali kuwa tajiri kuliko wananchi, hatua ambayo imekuwa inawafanya wananchi kukimbilia siasa na kufanya kazi serikalini kama njia ya kuwa na maisha bora.
Amesema lengo la ALAT ni kuona nchi inajenga mfumo wa kuwawezesha wananchi kuwa matajiri na serikali ikusanye kodi kutoka kwao hatua itakayowezesha uchumi wa pande zote mbili kukua kwa uwiano na kuondoa hali ilivyo sasa ambapo ingawa uchumi wa Taifa unakua, kuna umasikini kwa wananchi wa tabaka la chini, jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa Taifa.
Dk Masaburi ambaye pia ni Meya wa Jiji la Dar es Salaam aliyasema hayo alipozungumza na Wakuu wa Idara na Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma, wakiongozwa na Meya wa Manispaa hiyo Emmanuel Mwiliko na baadaye alipozungumza na Wakuu wa Idara wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji Lilian Matinga.
Mwenyekiti wa ALAT yupo katika ziara ya kuitembelea mikoa ya Dodoma na Kigoma ambayo ipo katika Mpango wa Ukuzaji wa Sekta ya Biashara Ndogo na za Kati (SMEs), Awamu ya Nne, unaofadhiliwa na Serikali ya Denmark kupitia Shirika lake la Maendeleo (DANIDA), lengo likiwa ni kukuza biashara ndogo katika ngazi za mitaa, kwa ushirikiano baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP).
Mpango huo unaofanyika kwa majaribio katika mikoa hiyo miwili kabla ya kutekelezwa nchi nzima, unapimwa katika viashiria vinne vya Ushirikiano wa Sekta Binafsi na Umma, Uboreshaji wa Mazingira ya Biashara kwa kuondoa vikwazo, Ongezeko la Uwekezaji na mwisho ni Matokeo ya Ukuaji wa Biashara na Uwekezaji katika maeneo husika kama chachu ya utekelezaji wa mpango huo kwa nchi nzima.
DANIDA imepanga kutumia zaidi ya Sh milioni 297 katika utekelezaji wa mpango huo utakaokamilika ifikapo mwaka 2019, kwa kuzipatia fedha halmashauri zitakazobuni miradi itakayotekelezwa chini ya PPP kwa lengo la kuchochea ukuaji wa uchumi kwa wafanyabiashara wa chini na kati.
Akizungumzia mfumo wa biashara na uwekezaji nchini, Dk Masaburi alisema mfumo uliopo sasa si mzuri kwa vile umekuwa unaifanya serikali kukusanya fedha karibu zote kutoka kwa wananchi kwa mlundikano wa kodi na mwishowe kuwaacha wananchi wakiwa masikini wakubwa.
“Sasa hivi hapa tukipasua vichwa vyetu karibu wote mtakuwa mnawaza kugombea ubunge au kufanya kazi serikalini kwa vile mnajua huko ndiko kwenye fedha za kuboresha maisha.
“Vijana wetu wakihitimu vyuo vikuu wanakimbilia CCM wakiona hakuna sehemu ya kupenya wanatoka na kukimbilia Chadema au CUF huko wakikwama wanarudi tena CCM na mwishowe wanakimbilia mitaani jambo ambalo ni hatari,” alisema Dk Masaburi.
Baada ya kukamilisha ziara hiyo mkoani Dodoma, Dk Masaburi anayefuatana na Katibu wa ALAT Taifa , Habraham Shamumoyo, wataendelea na ziara katika mkoa wa Kigoma kutoa ushawishi wa mpango huo kwa watendaji wa halmashauri za mkoani humo.
Home
News
Masaburi asema kuwa watapigana kufa na kupona ili kuona tanzania inabadili mfumo wa sasa unao onyesha tanzania kuwa tajiri kuliko wananchi wake
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment