Ametoa agizo hilo jana jioni (Jumatatu, Februari 23, 2015) wakati akizungumza na viongozi mbalimbali wa mkoa wa Iringa waliofika kusikiliza majumuisho ya ziara ya siku sita ya Waziri Mkuu kwenye mkoa huo. Mkutano huo ulifanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi ulioko Mafinga, wilayani Mufindi.
“Tafuta wote waliokaa zaidi ya miaka 10. Ni lazima tuwabadilishe... niletee orodha mapema iwezekanavyo,” alisema Waziri Mkuu.
Alisema nia ya zoezi hilo ni kuongeza ufanisi kwani watumishi wakikaa sehemu moja kwa muda mrefu wanakuwa butu kwa kukosa ubunifu kwenye kazi zao, wanaota mizizi na kugeuka kuwa chanzo cha matatizo katika baadhi ya sehemu.
Alimtaka pia Mkuu huyo wa mkoa pamoja na timu yake wasimamie vizuri ukusanyaji wa mapato ili kuongeza kiwango cha mapato cha mkoa huo. “Na siyo hilo tu, simamieni vizuri matumizi ya fedha zilizopangwa kwenye miradi mbalimbali ili kuleta maendeleo ya kweli kwa wananchi mnaowaongoza,” alisisitiza.
Alisema mkoa wa Iringa ni wa pili kwa kuwa na kiwango cha juu cha pato la mwanachi wa kawaida baada ya Dar es Salaam ambao ndiyo unaongoza nchini. “Katika taarifa ya Mkuu wa Mkoa, tulielezwa kwamba pato la mwananchi wa Iringa katika mwaka 2013 lilikuwa ni wastani wa shilingi 1,660,532/- ambazo ni sawa na shilingi 138,377/- kwa mwezi au shilingi 4,612/- kwa siku”.
Alisema pato la mwananchi wa Iringa linakua vizuri ikilinganishwa na mwaka 2006 ambapo pato hilo lilikuwa shilingi 589,607/- na limeongezeka hadi kufikia shilingi 1,660,532/- mwaka 2013. Alivitaja viashiria vya kukua kwa uchumi kuwa ni pamoja na ujenzi wa nyumba za kisasa zenye umeme, elimu bora, afya bora na upatikanaji wa vifaa vya mawasiliano kwenye ngazi ya kaya.
Alisema kulingana na taarifa ya Shirika la Fedha Duniani (IMF), Tanzania imeondolewa kutoka miongoni mwa nchi 10 barani Afrika zenye umaskini mkubwa na kwamba sasa Tanzania ni miongoni mwa nchi 20 duniani ambazo uchumi wake unakua kwa kasi kubwa.
“Kukua kwa pato la mkoa kumechangiwa hasa na kuwepo kwa mashamba makubwa ya tumbaku, chai, viwanda vya chai, misitu na viwanda vya mbao. Tukitumia vizuri fursa hizi, na tukijipanga vizuri tutaweza kuongeza pato la mkoa kuzidi hapa tulipo,” alisema.
Aliwataka watendaji wote katika ngazi zote, wawe na dhamira ya kuwaletea wananchi maendeleo na hivyo kuwaondolea umaskini na kuongeza pato lao kwa kila mmoja. “Ninawasihi sana viongozi wa mkoa tutangulize maslahi ya wananchi na siyo maslahi yetu binafsi. Tukifanya hivyo, wananchi wataona kweli tunawasaidia na tunastahili kuwaongoza,” aliongeza.
Waziri Mkuu amemaliza ziara ya siku sita katika mkoa wa Iringa na leo anakwenda Makambako, Njombe kuzindua uandikishaji wa Daftari la Mpiga Kura. Baadaye mchana, ataelekea Mbeya kuanza ziara ya kikazi ya siku sita kukagua shughuli za maendeleo katika mkoa huo.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, FEBRUARI 24, 2015.
0 comments:
Post a Comment