WAZIRI MKUU Mizengo Pinda
amesema amevutiwa sana na kazi iliyofanywa katika muda mfupi kwenye shamba la
kahawa la Aviv lililoko kwenye kijiji cha Lipokela, wilaya ya Songea Vijijini
mkoani Ruvuma.
Amesema katika kipindi
cha mwaka mmoja na miezi saba, eneo kubwa la shamba limepandwa miche ya kahawa
na mingine imezaa na imeshavunwa ikilinganishwa na wakati alipofika shambani
hapo Julai 2013 na kutembelea tu kitalu cha miche ya zao hilo.
Ametoa kauli hiyo jana
jioni (Jumatatu, Februari 2, 2015) wakati akizungumza na wafanyakazi na
menejimenti ya shamba la Aviv baada ya kulitembelea na kukagua miundombuinu ya
umwagiliaji wa matone ya maji kwenye shamba hilo.
“Mkuu wa shamba hili, Bw.
Medu amenieleza kwamba mpaka sasa, wameshavuna kahawa mara moja na wanatarajia
kuvuna tena hivi karibuni; lakini ili waweze kuanza kupata faida ni lazima
wavune mara nne.”
“Kilimo kinataka
uvumilivu na kinataka uwekezaji mkubwa... ni lazima kiwepo; hata kwa wakulima
wadogo ni lazima kiwepo licha ya ugumu wake. Sasa ukisema kilimo ni kigumu na
ukaacha kulima wakati una mke na watoto, je hao watakula wapi?”, alihoji.
Aliwasifu wamiliki wa
shamba hilo kwa kuchagua kulima zao la kahawa kwani lina walaji kila mahali
ulimwenguni kote. “Wameamua kulima kahawa aina ya Arabicaambayo inakubalika
duniani. Uhitaji wa kahawa hii upo kila mahali kwa sababu wanywaji wapo,”
alisema.
Waziri Mkuu alisema
pamoja na mafanikio hayo, shamba la Aviv linakabiliwa na changamoto ya nishati
kwani linahitaji megawati 2.5 ili liweze kuendesha mitambo yake ambayo kwa sasa
inatumia mafuta yanayoligharimu fedha nyingi.
Aliwataka
wamiliki wa shamba hilo waendelee kuwa wavumilivu wakati Serikali ikiendelea
kutafuta ufumbuzi wa suala hilo.
Mapema, akisoma risala ya kampuni ya Aviv, Mkuu wa shamba hilo
ambaye pia anasimamia uzalishaji wa zao la kahawa Afrika Mashariki, Bw. Medu
Medappa alisema hadi sasa wamekwishalima hekta 1,060 na zote zimekwishawekewa
miundombinu ya umwagiliaji wa matone na kati ya hizo, hekta 810
zimekwishapandwa miche ya kahawa.
“Shamba letu lina ukubwa
wa hekta 2,000 na hadi sasa tumeshalima hekta 1,060 na zilizobakia ni kwa ajili
ya kutunza mazingira na uoto wa asili kwenye vilima vinavyotuzunguka,” alisema.
Alisema hadi sasa
wamekwishaajiri wafanyakazi 1,500 kwenye shamba hilo na kutoa mafunzo kwa
wakulima wanaoishi vijiji vya jirani. “Pia tumewapatia miche ya bure kaya 673
na kutokana na mafunzo tunayowapa, wanavijiji wameweza kulima kahawa
inayoendana na viwango vya kimataifa vya uzalishaji kahawa ambavyo ni miezi
22,” alisema.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Bw. Said Mwambungu akijibu moja ya
hoja kwenye risala ya Bw. Medappa iliyohusu eneo la hekta tisa kuchukuliwa na
Wakala wa Ujenzi wa Barabara (TANROADS), alisema eneo hilo ni muhimu kwa ujenzi
wa barabara za mkoa huo kama ambavyo shamba hilo ni muhimu kwa mkoa huo.
“Lile eneo limetengwa na
TANROADS kwa ajili ya kutengeneza kokoto za ujenzi wa barabara. Barabara za
lami tunazitaka. Tunahitaji kazi hii iendelee la sivyo barabara zetu zitakufa,”
alisema.
Alisema watu wa TANROADS
wakimaliza kazi yao, lile eneo litabaki tupu na mwekezaji huyo anaweza
kulitumia kadri atakavyoona inafaa kwa sababu liko ndani ya eneo lake.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI
YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE,
FEBRUARI 3, 2015.
Irene K. Bwire
0 comments:
Post a Comment