Ni takriban miezi minne sasa tangu vyama vinne vya upinzani
nchini kupitia ushirikiano wao walioupa jina la Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa), kusaini makubaliano ya kushirikiana pamoja na
kusimamisha mgombea mmoja katika chaguzi zote zijazo.
Umoja huo unaoundwa na vyama CUF, Chadema, NCCR-
Mageuzi na NLD, unakabiliwa na kazi moja ngumu ya kufikia mwafaka wa
kumpata mgombea urais, kabla filimbi ya uchaguzi kupulizwa.
Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya siasa nchini
wanasema kabla ya kumpata mgombea mmoja, vyama hivyo vinne, vitalazimika
kufanya uamuzi katika sera zao kabla ya kuja na jibu la mgombea kutoka
chama kimojawapo atakayekuwa na sifa ya kupeperusha bendera kwa niaba ya
umoja huo.
Kufikia hatua hiyo, changamoto kubwa inayoukabili
umoja huo ni namna ya kumpata mgombea wa urais atakayetoa upinzani
mkubwa zaidi kwa mgombea wa chama tawala.
Historia ya wanaoweza kugombea
Mpaka sasa aliyekuwa mgombea wa urais katika
uchaguzi wa mwaka 2010 kupitia Chadema, Dk Willibrod Slaa ndiye
anayeonekana kuwa anaweza kupata mtaji mkubwa wa kura.
Matarajio haya yanahanikizwa na takwimu za
uchaguzi wa mwaka huo zinazoonyesha kuwa ndiye aliyepata kura nyingi
kulinganisha na wagombea wa vyama vingine vitatu ambavyo mwaka huu
vimeamua kujiunga pamoja kupitia Ukawa. Katika uchaguzi wa mwaka 2010,
Dk Slaa alipata asilimia 26.34 ya kura zote na kuweka rekodi ya upinzani
ikilinganishwa na wagombea wengine miongoni mwa wanaotajwa kuwania
nafasi hiyo ya Ukawa waliowawahi kugombea siku za nyuma.
Kwa CUF kuna kila dalili kuwa Profesa Ibrahim
Lipumba anaweza kupendekezwa kugombea kiti cha urais kupitia Ukawa.
Mgombea huyu si mgeni katika chaguzi, ameshiriki tangu mwaka 1995 bila
ya mafanikio.
Katika chaguzi nne zilizopita CUF kupitia Profesa
Lipumba kimekuwa katika mtiririko usioridhisha wa kupanda na kushuka
katika upataji wa kura za wananchi.
Katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka
1995, alipata kura 418,973, sawa na asilimia 6.43 ya kura zote na
kushika nafasi ya tatu akiwa nyuma ya Benjamin Mkapa wa CCM na Augustine
Mrema aliyegombea kwa tiketi ya NCCR- Mageuzi.
Profesa Lipumba aliingia tena katika uchaguzi wa
mwaka 2000 na kushika nafasi ya pili baada ya kupata kura 1,329,007
(sawa na asilimia 16.26) akiwa nyuma ya Mkapa na uchaguzi uliofuata
alipata kura 1,327,125 (sawa na asilimia 11.68) kabla ya kushuka tena
mwaka 2010 alipopata kura 695,667 (asilimia 8.06).
Kigogo mwingine wa Ukawa ni Mwenyekiti wa NCCR-
Mageuzi, James Mbatia. Hata hivyo, hajaonekana kuleta upinzani kwani
hana historia ya kugombea urais, licha ya kuwa chama chake kimepata
kusimamisha mgombea wa nafasi mara tatu.
0 comments:
Post a Comment