Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam akitoa
taarifa ya mkutano wa wawekezaji (Round Table Investment Forum) na wakuu wa
nchi 5 za ukanda wa Afrika Mashariki utakaofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia
Machi 25 hadi 26 mwaka huu.
Kamishina wa Polisi wa Kanda Maalum
ya Dar es salaam Suleiman Kova akitoa taarifa ya hali ya ulinzi na usalama
katika jiji la Dar es salaam na vifo vya watu 7 waliopoteza maisha kutokana na
mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika jiji la
Dar es Salaam.
Na Aron Msigwa –MAELEZO.
Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji
wa mkutano wa wawekezaji (Round Table Investment Forum) wa Marais wa nchi 5 za
ukanda wa Afrika Mashariki utakaofanyika jijini Dar es salaam kuanzia Machi 25
hadi 26 mwaka huu.
Akitoa taarifa ya mkutano huo Mkuu
wa wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Saidi Meck Sadiki amesema kuwa Marais hao Paul
Kagame wa Rwanda, Pierre Nkurunzinza wa Burundi, Yoweri Museveni wa Uganda,
Uhuru Kenyatta wa Kenya na Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
watahudhuria mkutano huo wakiwa wameambatana na jumla ya wawekezaji 350.
Amesema Tanzania kwa mara nyingine
imepata heshima ya kuandaa mkutano huo na kufafanua kuwa wawekezaji hao
wamekwisha anza kuwasili jijini Dar es Salaam kuanzia Machi 22 , huku marais
nchi hizo wakitarajiwa kuwasili jijini humo kuanzia Machi 24,2015.
Amesema wakiwa nchini Tanzania
Marais hao watashiriki kwenye mkutano wa wawekezaji utakaofanyika ukumbi wa
Mikutano wa Kimataifa Mwalimu J.K.Nyerere kuanzia Machi 25 hadi 26,
watatembelea bandari ya Dar es Salaam ili kuona namna nchi za Ukanda wa Afrika
Mashariki zinavyoshirikiana katika masuala ya ushuru wa forodha na usafirishaji
wa bidhaa mbalimbali.
Amebainisha kuwa kabla ya kuaondoka
nchini Tanzania Machi 26, 2015 Marais hao pia watatembelea miundombinu ya reli
inayotumika kusafirisha mizigo nchi za maziwa makuu kwa lengo la kuimarisha
ushirikiano katika usafirishaji wa bidhaa mbalimbali baina ya nchi zao.
KUHUSU MVUA ZINAZOENDELEA KUNYESHA
JIJINI DAR ES SALAAM
Aidha, kuhusu mvua zinzoendelea
kunyesha katika jiji la Dar es salaam na kusababisha madhara, Mkuu wa Mkoa wa
Dar es salaam Saidi Meck Sadiki amewataka wananchi kuzingatia agizo la kuhama
mabondeni na maeneo mengine hatarishi ili waepuka maafa kufuatia watu 7
kupoteza maisha kutokana na kutokana na athari za mvua zinazoendelea kunyesha.
Akifafanua kuhusu matukio hayo Mhe.
Sadiki amesema maeneo yaliyokumbwa na mafuriko hayo na kupata maafa hayo ni
bonde la Mto Msimbazi na eneo la Buguruni kwa Myamani.
Amesema kuwa maeneo yaliyokumbwa na
mafuriko hayo yameonekana kuwa na wingi wa takataka ngumu na wingi wa mifuko ya
plastiki iliyotupwa na wakazi hao hali iliyochangia kuziba mifereji inayopeleka
maji katika bonde la mto Msimbazi na maji hayo kuhamia kwenye makazi ya watu.
Ameeleza kuwa kazi ya uokoaji ,
kumwaga dawa kwenye maji yaliyotuama ili kuzuia athari ya magonjwa ya milipuko,
kuzibua mifereji na kukusanya taka katika maeneo hayo inaendelea ili kuruhusu
maji kupita kwa urahisi na kuwataka wakazi hao kuepuka kutupa taka ngumu
zinazoziba mifereji ya maji.
Amesema Serikali inasubiri taarifa
kutoka kwa viongozi wa Serikali za Mitaa kwa maeneo ambayo wakazi wake wanaishi
kihalali ili waweze kupatiwa misaada ya kibinadamu.
Kwa upande wake Kamishina wa Polisi
wa Kanda Maalum ya Dar es salaam Suleiman Kova amethibitisha vifo vya watu hao
7 waliopoteza maisha kutokana na maeneo yao kukumbwa na mafuriko pamoja na
athari ya Umeme.
Akitoa ufafanuzi wa vifo hivyo
amesema kuwa watu 5 wamepoteza maisha kwa kusombwa na maji na wengine 2
wamepoteza maisha kutokana na ajali iliyosababishwa na Lori moja kugonga
Transfoma ya umeme eneo la Buguruni Mnyamani.
Kamishna Kova amesema tayari Jeshi
la Polisi kwa kushirikiana na Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji na Shirika la
Ugavi wa Umeme (TANESCO) wameunda kikosi kazi cha uokoaji.
Ametoa wito kwa madereva wa magari
ya mizigo, mgari binafsi na yale ya abiria kuepuka kupita katika maeneo
yaliyojaa maji ili kuepuka ajali na vifo vinavyoweza kuzuilika.
0 comments:
Post a Comment