“Ni mabadiliko ya
haraka sana katika ukusanyaji wa mapato kutoka jumla ya wastani wa trilioni 5.4
mwaka 2010/2011 hadi trilioni 9.8 mwaka 2013/2014 kwa nchi nzima. Tafsiri ya
mabadiliko haya ni kuwa TRA inafanya vizuri” Dk. Shein amesema.
Alitoa mfano kwa upande
wa Zanzibar kuwa Mamlaka hiyo pia imeweza kuongeza ukusanyaji wa mapato kutoka
bilioni 91.69 mwaka 2011/2012 hadi bilioni 136.7 mwaka 2013/2014 huku makusanyo
ya mwaka 2014/2015 yakitarajiwa kuongeza kupita nwaka uliopita.
Akizungumza na Bodi ya
Mamlaka hiyo Ikulu leo, Dk. Shein amesema historia inaonesha kuwa kazi ya
kukusanya kodi kote duniani ina vikwazo vingi hivyo aliwataka watumishi wa
Mamlaka hiyo kutokata tamaa na changamoto zinazowakuta badala yake kuzitafuta
ufumbuzi na kuongeza juhudi kazini.
“changamoto zipo
haziwezi kuondoka na ukweli ni kuwa hata wakati wa Mitume kazi ya ukusanyaji
kodi ilikuwa ngumu kwa kuwa mfanyabiashara kama walivyo baadhi ya binadamu
akipatacho hapendi kukitoa”
Aliwahakikishia wajumbe
wa bodi hiyo walioongozwa na Mwenyekiti wake Bernard Mchomvu na Mkurugenzi Mkuu
wa Mamlaka hiyo Bwana Rished Bade kuwa Serikali zote mbili zinaridhika na
utendaji wa Mamlaka hiyo na zinaamini kuwa itafikia malengo ya serikali ya kuanzisha
mamlaka hiyo.
Dk. Shein ameipongeza
TRA kwa kubuni mikakati mbali mbali ya kuongeza mapato ya serikali lakini
akahimiza maandalizi ya kutosha, uwazi na elimu kwa walengwa ambao ni walipa
kodi.
“Katika mipango yetu
tunayoibuni kuongeza mapato ni muhimu kuzingatia uwazi kadri inavyowezekana kwa
kuwa kukosekana kwa uwazi na elimu ya kutosha kwa walengwa kunaweza kusababisha
matokeo yasiyotarajiwa” Dk. alieleza.
Mapema akitoa maelezo
kwa Mheshimiwa Rais, Mwenyekiti wa Bodi hiyo Bwana Bernard Mchomvu alisema
Mamlaka hiyo imejidhatiti kukusanya kodi ili kukidhi mahitaji ya taifa na
kwamba inachukua hatua mbali mbali kufikia malengo yake.
“Ili tuweze tuweze
kufikia malengo kukidhi mahitaji ya taifa tumepanga kuzitafutia ufumbuzi
changamoto zinazotukabili ikiwemo kuweka mazingira mazuri ya kukusanya kodi kwa
watumishi wa Mamlaka na mazingira mazuri ya watu kulipa kodi”alieleza Bwana
Mchomvu.
Alitaja baadhi ya
vikwazo vinavyozuia kukusanya mapato mengi zaidi kuwa ni pamoja na ukwepaji
kodi, uingizaji bidhaa kwa magendo, udanganyifu katika orodha ya bidhaa
zinayoingia na misamaha ya kodi jambo ambalo hivi sasa Serikali
inalishughulikia.
Bwana Mchomvu alieleza
umuhimu wa waheshimiwa Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kushiriki
katika kutoa elimu kwa walipa kodi ikiwemo matumizi ya mashine za kisasa za
mauzo ambazo baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakizipinga.
Alisema mashine hizo ni
bora na zinamsaidia mfanyabiashara kuweka mahesabu yake vizuri lakini inaonesha
wafanyabiashara wengi hawapendi mambo yao kujulikana.
Kwa upande wake
Mkurugenzi Mkuu wa TRA Bwana Rished Bade alieleza kuwa hivi sasa Mamlaka hiyo
inafanya mabadiliko kadhaa ikiwemo kuweka mfumo mpya wa forodha na ifikapo
mwezi Juni mwaka huu mfumo huo utaanza kutumia Zanzibar.
Aidha Mamlaka alisema
itaongeza uwazi katika kupitisha viwango vya kodi ili walengwa wavifahamu
mapema sambamba na kuongeza kasi ya utoaji wa elimu kwa walipa kodi.
Aliongeza kuwa Mamlaka
hiyo itaongeza nguvu pia katika kukabiliana na wakwepa kodi, itaajiri watumishi
zaidi ili kuwafikia walipa kodi wengi zaidi pamoja na kuwabadili watumishi mara
kwa mara kuepusha kuzoeleka katika eneo moja la kazi.
Mamlaka alieleza
Mkurugenzi Mkuu huyo kuwa ina mpango wa kuwapatia mafunzo zaidi watumishi wake
ili waweze kuwa na uwezo mzuri katika kutathmini thamani ya bidha na kodi zake.
Wajumbe hao wa Bodi ya
TRA wako Zanzibar kuhudhuria kikao cha bodi hiyo.
0 comments:
Post a Comment