Maalim Seif akutana na wanachama walioomba kugombea nafasi za Ubunge kupitia CUF.
Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad, akizungumza na wagombea wa Uwakilishi, Ubunge na Udiwani wa CUF katika ukumbi wa Majid, Kiembesamaki.
Mkurugenzi wa Mipango na Chaguzi wa CUF Omar Ali Shehe akizungumza katika mkutano na wagombea wa Uwakilishi, Ubunge na Udiwani wa CUF katika ukumbi wa Majid, Kiembesamaki.
Baadhi ya wagombea Uwakilishi, Ubunge na Udiwani wa CUF Unguja wakijitokeza kwenye mkutano huo. (Picha na Salmin Said, OMKR)
Na Hassan Hamad, OMKR
Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF) Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amewataka wagombea wa nafasi mbali mbali ndani ya chama hicho kujenga imani na kamati za uteuzi za kuwapata wagombea kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Amesema kamati zote zilizoteuliwa kufanya kazi hiyo zitafanya kazi zake kwa umakini bila ya kujali wadhifa au umaarufu wa mgombea.
Maalim Seif ameeleza hayo katika kikao maalum cha kupeana nasaha na wanachama walioomba kugombea nafasi za Ubunge, Uwakilishi na Udiwani upande wa Unguja, kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao, kikao kilichofanyika ukumbi wa Majid, Kiembe Samaki.
Amefahamisha kuwa kamati zilizochaguliwa zimewekewa vigezo maalum na zitafanya kazi ya kuwateuwa wanachama wenye moyo wa kujituma na kukitumikia chama ili kiweze kupata ushindi.
Amewapongeza wanachama wa chama hicho kwa kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi hizo, hali inayodhihirisha demokrasia ndani ya chama hicho.
Mapema akisoma taarifa ya maendeleo ya uteuzi wa wagombea, Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa CUF Omar Ali Shehe amesema jumla ya wanachama 310 wamejitokeza kugombea Uwakilishi na Ubunge kwa majimbo 32 ya Unguja.
Amesema hatua inayofuata sasa ni kwa wagombea hao kufanyiwa usaili, kazi inayotarajiwa kufanyika mwishoni mwa wiki hii ambapo kwa upande wa Pemba tayari kazi hiyo imeshafanyika.
Mhe. Shehe amesema kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa chaguzi za vyama vingi mwaka 1995, chama hicho kinatarajia kusimamisha wagombea wa Udiwani katika wadi zote za Zanzibar, hatua inayoonesha kupevuka kwa chama hicho kisiasa.
0 comments:
Post a Comment