Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Mhe. Anne Kilango
Malecela (wa pili kulia) akimsikiliza Meneja Upangaji Mikopo wa Bodi ya Mikopo
ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Bi. Emma Sabaya (kushoto) leo (Jumatano,
Aprili 22, 2015) jijini Dar es Salaam. Naibu Waziri alifanya ziara ya kikazi
katika Bodi hiyo na kukutana na uongozi wa Bodi.
Mkurugenzi wa Mipango, Utafiti na TEHAMA wa Bodi ya Mikopo ya
Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Bw. Asangye Bangu (mwenye tai ya njano)
akimweleza Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Mhe. Anne
Kilango Malecela (kulia) jinsi kumbukumbu za waombaji wa mikopo
zinavyohifadhiwa katika Bodi hiyo jijini Dar es Salaam leo (Jumatano, Aprili
22, 2015). Naibu Waziri alifanya ziara ya kikazi katika Bodi hiyo na kukutana
na uongozi wa Bodi.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya
Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Bw. Hamisi Chagonja akimkabidhi zawadi Naibu
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Mhe. Anne Kilango Malecela jijini Dar es
Salaam leo (Jumatano, Aprili 22, 2015). Naibu Waziri alifanya ziara ya kikazi katika
Bodi hiyo na kukutana na uongozi wa Bodi.Picha na HESLB.
Na Mwandishi Wetu.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Mhe.
Anne Kilango Malecela ameilekeza Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu
(HESLB) kuongeza kasi ya utoaji elimu kwa wadaiwa wake na umma kwa ujumla ili
kuongeza makusanyo ya marejesho na hatimaye kuwa na mfuko endelevu wa mikopo ya
wanafunzi.
Akizungumza na uongozi wa Bodi hiyo jijini Dar
es Salaam leo (Jumatano, Aprili 22, 2015), Naibu Waziri Malecela amesema
wadaiwa wa Bodi hiyo wakielewa umuhimu wa kulipa mikopo yao, kasi ya ulipaji
itaongezeka.
“Ongezeni juhudi zaidi na hasa tengenezeni
matangazo ya televisheni yanayotoa elimu ili kuwakumbusha wadaiwa na wananchi
kwa ujumla juu umuhimu wa kulipa,” amesema Naibu Waziri wakati wa ziara yake ya
kikazi katika ofisi za Bodi hiyo jijini Dar es Salaam.
Maelekezo ya Naibu Waziri yalifuatia taarifa ya
utekelezaji wa majukumu ya Bodi iliyowasilishwa na Naibu Mkurugenzi wa Habari,
Elimu na Mawasiliano wa HESLB Bw. Cosmas Mwaisobwa ambaye alitaja changamoto
mbalimbali zinazoikabli HESLB ikiwemo wakopaji wengi na waajiri
kutokutoa ushirikiano kwa Bodi katika urejeshwaji mikopo.
“Wakopaji wengi ambao
mikopo yao inapaswa kuanza kurejeshwa hawatoi ushirikiano wa kutosha kwa Bodi
katika kurejesha mikopo yao, na hili linachangiwa pia na kutokuwepo kwa
Vitambulisho vya Kitaifa ambavyo vingerahisisha ugunduzi wa wapi walipo wadaiwa
hao,” amesema Mwaisobwa katika kikao na Naibu Waziri.
Mwaisobwa alitaja
changamoto nyingine kuwa ni pamoja na mtazamo potofu kuwa fedha zinazotolewa na
Bodi hiyo ni ruzuku badala ya mikopo na kuongezeka kwa idadi ya waombaji mikopo
wakiwemo hata wale ambao wazazi wao wana uwezo wa kuwagharamia.
Kwa mujibu wa Mwaisobwa,
changamoto nyingine ni pamoja na baadhi ya wazazi, walezi na waajiri na
wafadhili wenye uwezo kujitoa katika kugharamia wanafunzi wanaosoma katika
taasisi za elimu ya juu kwa kutegemea mikopo inayotolewa na Bodi.
Pamoja na changamoto hizo,
Mwaisobwa, kwa Niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi alimweleza Naibu Waziri
Malecela kuwa katika mwaka wa masomo 2014/2015, kati ya waombaji wa mikopo 39,411 wa mwaka wa
kwanza waliofanyiwa tathmini ya uwezo wa kiuchumi, wanafunzi 33,595 walipangiwa
mikopo.
Kati ya hao, amesema Mwaisobwa, wanafunzi 31,238 ni
wa shahada ya kwanza katika vyuo vya ndani, 2,117 ni wa
wanafunzi wa Diploma ya Ualimu katika fani ya sayansi na hisabati na wengine 160 ni
wa mwaka wa kwanza wanaosoma nje ya nchi. Wanafunzi 80 ni wa
shahada ya Umahiri na Uzamivu katika vyuo vya ndani ya nchi.
Mikopo hiyo hutolewa ili
kugharamia maeneo sita ambayo ni chakula na malazi; mafunzo kwa vitendo; vitabu
na viandikwa; fedha za utafiti; ada ya mafunzo; na mahitaji maalumu ya kitivo
HESLB ilianzishwa kwa
sheria ya Bunge na 9 ya mwaka 2004 na kuanza kazi rasmi mwezi Julai, 2005 ili,
pamoja na majukumu mengine kutoa mikopo kwa wanafunzi wahitaji waliodahiliwa
katika taasisi za elimu ya juu. Aidha, jukumu jingine la Bodi ni kudai na
kukusanya mikopo yote iliyotolewa kwa wahitimu wa taasisi za elimu ya juu
kuanzia mwaka 1994 wakati Serikali ilipoanza kukopesha wanafunzi.
Kwa mujibu wa Mwaisobwa, jumla ya wanafunzi
291,582 wamenufaika na mikopo ya elimu ya juu inayotolewa na Serikali kati ya
mwaka 1994 na Juni mwaka jana (2014). Jumla ya kiasi cha fedha kilichokopeshwa
hadi kufikia mwaka jana (Juni, 2014) ni Tshs 1.8 trilioni ambapo Tshs 51.1
bilioni zilitolewa na iliyokuwa Wizara ya Elimu Juu, Sayansi na Teknolojia na
Tshs 1.75 trilioni zimetolewa na HESLB tangu ilipoanza kazi rasmi Julai 2005.
0 comments:
Post a Comment