WAZIRI MKUU Mizengo Pinda
amepokea hundi ya mfano (Dummy Cheque) yenye thamani ya sh. bilioni 1.5 kutoka
benki ya NMB zikiwa ni mchango wa taasisi hiyo kwenye kampeni ya uchangiaji
madawati kitaifa.
Akizungumza na Waziri Mkuu
ofisini kwake Magogoni jijini Dar es Salaam jana jioni (Jumatano, Aprili 29,
2015), kabla ya kukabidhi hundi hiyo, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Bw.
Tom Borghols alisema wameamua kutoa mchango ili kusaidia kupunguza tatizo la
uhaba wa madawati linalozikabili shule za msingi na za sekondari hapa nchini.
“Tunaelewa kwamba shule
nyingi hapa nchini zinakabiliwa na uhaba wa madawati … tunaamini kuwa elimu
bora inachangiwa pia na mazingira mazuri ya kusomea ikiwa ni pamoja na kukaa
kwenye madawati wanapoandika. Kama sehemu ya mchango wetu kwa jamii (CSR),
tumeamua kutenga sh. bilioni 1.5 ili zisaidie kupungua tatizo hilo,” alisema.
Akipokea mchango huo, Waziri
Mkuu aliushukuru uongozi wa benki hiyo ulioambatana na Bw. Borghols kwa kuamua
kusaidia juhudi za Serikali kutatua tatizo hilo. Alisema mchango huo ni mkubwa
na anaamini kwamba utawachochea wadau wengine kuchangia juhudi za Serikali
kutatua tatizo la madawati nchini.
“Nimecheki na watu wangu kwa
kweli mahitaji ni makubwa lakini naamini mchango wenu utasaidia kupunguza
tatizo la madawati kwa kiasi fulani. Tunawashukuru kwa uamuzi wenu wa kuchangia
suala hili la kitaifa,” alisema.
Hadi sasa Serikali inahitaji
kununua madawati 1,016,476 kwa ajili ya shule za msingi na za sekondari. Kati
ya hayo, madawati 892,772 yanahitajika kwa ajili ya shule za msingi na madawati
123,704 yanahitajika kwa ajili ya shule za sekondari.
Madawati hayo yote
yataigharimu Serikali kiasi cha sh. bilioni 91.4/- kwa gharama ya sh. 90,000/-
kwa kila dawati.
Hata hivyo, Serikali iliamua
kutenga fedha za chenji ya RADA ili zitumike kununua madawati na vitabu. Fedha
hizo, zilisaidia kununua madawati 168,163 kwa bei ya sh. 90,000/- kwa dawati
moja.
(mwisho.
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM
ALHAMISI, APRILI 30, 2015.
Irene K. Bwire
0 comments:
Post a Comment