Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa
hajaletewa majina ya watu 16 waliohukumiwa kifo kutokana na mauaji ya maalbino
nchini kwa sababu safari ya kisheria ya majina hayo kufikishwa kwake ni ndefu.
Rais Kikwete
aliyasema hayo jana, Jumapili, Aprili 12, 2015
wakati alipozungumza katika ibada maalum ya kuwekwa wakfu na kusimikwa
kwa Askofu Liberatus Sangu kuwa Mhashamu Baba Askofu wa Jimbo la Kanisa
Katoliki la Shinyanga.
Akizungumza
katika ibada hiyo iliyofanyika kwenye Kanisa Kuu la Mama Mwenye Huruma,
Ngokolo, mjini Shinyanga na mbele ya viongozi wengi wa Kanisa hilo wakiwemo
maaskofu wakuu, maaskofu na maaskofu wasaidizi 38, Rais Kikwete alitumia nafasi
hiyo kujibu madai kuwa Serikali yake haichukui hatua za kutosha kukabiliana na
mauaji ya albino na pia kufafanua juu ya shinikizo ambalo linatolewa na baadhi
ya mashirika yasiyokuwa ya serikali (ngo’s) yakimtaka Rais kutia saini ya
kuruhusu watu hao wanyongwe.
Rais Kikwete
aliwaambia viongozi hao wa dini: “Ninayo maombi maalum kwenu viongozi wa dini.
Naomba mtusaidie kuielimisha jamii ili iachane na imani za kishirikina.
Vikongwe wanauawa kwa sababu tu ya kuwa na macho mekundu na ujinga uliokithiri
unaosababisha Watanzania wenzetu wenye ulemavu wa ngozi (albino) kusakwa na kuuawa kikatili kabisa.”
“Nawaombeni
sana viongozi wa dini tusaidiane katika kukomesha ujinga huu mkubwa kwa kutoa
elimu kwa waumini wenu, ili wajue kuwa vikongwe wana macho mekundu kwa sababu
ya kutumia samadi ya ng’ombe kupikia kwa muda mrefu na kuwa kiungo cha albino
hakiweza kuleta utajiri wowote,” Rais aliwaambia viongozi hao wa dini.
Kuhusu madai
kuwa Serikali yake haichukui hatua za kutosha kukabiliana na mauaji ya albino,
Rais Kikwete aliwaambia viongozi hao: “Tumewatia mbaroni watuhumiwa wengi wa
mauaji ya albino. Watu 16 tayari wamehukumiwa kifo na wengine wanasubiri…kesi
zao zinaendelea kusikilizwa. Yapo maneno maneno, lakini binafsi kama Rais
sijaletewa majina ya watu hao.”
Aliongeza: “Ni
lazima tuelewe jinsi mfumo wetu wa kutoa haki unavyofanya kazi hasa katika eneo
hilo la kunyonga ama kutokunyonga. Ni mlolongo mrefu. Katika kesi za watu
kuhukumiwa kifo, kwanza kukata rufani ni lazima na wala siyo jambo la hiari ama
matakwa ya aliyehukumiwa. Pili,
tukimalizana na rufani ni lazima Kamati ya Msamaha (Committee on Prerogative of
Mercy) nayo ifanye kazi. Kwa hiyo ni utaratibu mrefu kidogo.”
Mhashamu Baba
Askofu Sangu ambaye aliteuliwa na Baba Mtakatifu Francesco kuwa Askofu Februari
2, mwaka huu, 2015, amechukua nafasi ya hayati Baba Askofu Aloysius Balina
ambaye alifariki dunia Novemba 6, 2012.
Wakati wa
uteuzi wake, Mosinyori Sangu alikuwa anafanya kazi kwenye Idara ya Uenezaji
Injili Ulimwenguni katika makao makuu ya Kanisa Katoliki, Vatican ambako
alifanya kazi kwa miaka minane.
Mwisho.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu
– Dar es Salaam.
13 Aprili,2015
0 comments:
Post a Comment