Hotuba zote mbili, ya kamati
na upinzani, zilieleza kushangazwa na kitendo cha waziri huyo kupinga watalii
kulipa tozo mara moja kila wanapoingia katika Hifadhi ya Serengeti na Ziwa
Manyara, badala yake kung’ang’ania walipe mara mbili, jambo ambalo ni kinyume
na maelekezo ya Bunge.
Akisoma taarifa ya kamati
kuhusu utekelezaji wa majukumu ya wizara hiyo, mwenyekiti wa kamati hiyo James
Lembeli alisema, “Takwimu zinaonyesha kwamba tangu Julai 2014 hadi Machi 2015,
hifadhi hizo mbili zilipoteza Sh1.4 bilioni kutokana na wizara kulazimisha tozo
mara mbili. Kamati inahoji, kuna masilahi gani waziri kutetea mfumo ambao
unaipotezea Serikali mapato?”
Alisema licha ya Bunge
kuazimia Nyalandu atekeleze hukumu ya Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha iliyomtaka
kutangaza katika gazeti la Serikali tozo mpya zitakazotumika katika hoteli
ndani ya Hifadhi za Taifa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, hakuzingatia suala
hilo.
“Kutokana na kuchelewa kuanza
kutumika kwa tozo mpya kama ilivyoamriwa na Mahakama, Serikali imepoteza Sh3
bilioni hadi kufikia Machi 15, 2015. Kamati inamtaka waziri (Nyalandu)
kulieleza Bunge nini kilimfanya akaidi kutekeleza hukumu iliyokuwa na masilahi
kwa Taifa,” alisema Lembeli.
Msemaji wa Kambi ya Upinzani
kuhusu wizara hiyo, Mchungaji Peter Msigwa alisema: “Fedha hizi Sh3 bilioni
zingeweza kununulia madawati ya watoto wanaokaa chini, kununua vitanda vya
wajawazito au kupunguza deni la (MSD) Bohari Kuu ya Dawa.”
Mchungaji Msigwa alisema ni
aibu kwa Nyalandu ambaye ametangaza nia ya kugombea urais, kusimama na kusoma
mafanikio ya wizara yake wakati amelisababishia Taifa hasara.
Katika hotuba yake, Msigwa
pia aligusia ujangili wa wanyamapori na kuhoji sababu za Serikali kushikwa na
kigugumizi cha kuteketeza tani 90 za shehena ya meno ya tembo yaliyohifadhiwa
katika maghala baada ya kukamatwa kutoka kwa watu mbalimbali.
Msigwa pia aliibua sakata la
kusafirishwa kwa wanyama hai kwenda Uarabuni akiitaka Serikali iweke hadharani
majina ya watu waliohusika.
Mbunge huyo wa Iringa Mjini
alisema ni wakati sasa kwa Serikali kuanika uozo huo hadharani kwa kuwa suala
la kusafirishwa kwa wanyama haliko mahakamani tena kama ambavyo Serikali
imekuwa ikijificha humo.
“Tunaomba majibu sasa, nani
alibeba wanyama wale maana kesi haiko tena mahakamani kama ambavyo mmekuwa
mkitueleza,” alisema Msigwa.
Alisema Watanzania wamechoka
kudanganywa kwa maneno matamu ya kuwapumbaza, wanachotaka ni kujua jinsi
rasilimali zao zinavyotumiwa vibaya.
0 comments:
Post a Comment