CCM ipo kwenye wakati mgumu
wa kutafuta mrithi wa Jakaya Kikwete katika nafasi ya urais na mwenyekiti wa
chama hicho kikongwe nchini baada ya Rais huyo wa sasa kuongoza nchi kwa
vipindi viwili vya miaka mitano kila kimoja na hivyo kulazimika kuondoka Ikulu
kutokana na utashi wa kikatiba.
Kutokana na hilo, zaidi ya
makada 20 wanatajwa kuwa na nia ya kuomba ridhaa ya CCM kugombea urais ili
kuongoza Serikali ya Awamu ya Tano na watatakiwa kutangaza, kuchukua fomu na
kuzirudisha ndani ya takribani siku 32 kabla ya Julai 2 ambayo ni siku ya
mwisho iliyowekwa na chama hicho.
Wakati makada hao wa CCM
wakijipanga kufanya shughuli kubwa za kutangaza nia ya kuomba wanachama wao
wawape ridhaa ya kugombea urais, baadhi ya vyama vya upinzani vimeshatangaza
ratiba zao lakini kinyang’anyiro kikubwa kitakuwa wakati vyama vilivyo chini ya
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vitakapofanya mchujo wa kumpata mgombea
atakayewakilisha umoja huo.
Kwa mujibu wa ratiba za
makada wa CCM, kesho Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa atafanya mkutano wa
hadhara kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha kutangaza rasmi nia ya
kuomba kuteuliwa na CCM kugombea nafasi hiyo ya juu nchini.
Timu ya Lowassa, ambaye
aliwaambia wahariri wa vyombo vya habari mwanzoni mwa wiki kuwa atatangaza nia
Mei 30, imekuwa ikitoa matangazo mbalimbali kwenye vyombo vya habari na
mitandao ya kijamii kutaarifu tukio hilo la kuanza rasmi kwa safari aliyoiita
“ya matumaini”.
Katika mkutano wake na
wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari mapema wiki hii, Lowassa alihifadhi
majibu ya baadhi ya maswali, akisema ni sehemu ya masuala atakayozungumzia
kwenye hotuba yake ya kutangaza dhamira yake ya kuomba urais.
Tukio hilo litakalofanyika
kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha litarushwa moja kwa moja na vyombo
vinane vya habari kwa muda wa saa nne kuanzia saa 8:00 mchana hadi saa 11:00
jioni.
Habari ambazo Mwananchi
imezipata kutoka vyanzo mbalimbali zinaeleza kuwa kumekuwa na maandalizi ya
hali ya juu jijini Arusha kuelekea siku ya tukio hilo ikiwa ni pamoja na
kuwasili kwa watu mbalimbali wanaomuunga mkono wakiwamo wajumbe wa Halmashauri
Kuu ya CCM.
Lowassa, ambaye ni mbunge wa
Monduli, alikuwa waziri mkuu wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Nne, lakini
akalazimika kujiuzulu mwaka 2008 baada ya Kamati ya Bunge kuibua kashfa ya
kuingia mkataba wa ufuaji umeme wa dharura na kampuni iliyokuwa haina sifa ya
Richmond RDC, uamuzi ambao anasema aliufanya ili kuiokoa nchi.
Lowassa pia aliwahi kuwania
urais mwaka 1995, lakini CCM ikampa nafasi Benjamin Mkapa kuongoza Serikali ya
Awamu ya Tatu.
Wakati Lowassa na timu yake
wakiwa katika mikakati hiyo, makada wengine wa CCM ambao nao wanawania nafasi
ya kuteuliwa na chama hicho, pia wamejipanga kutangaza nia zao kila mmoja kwa
wakati wake huku wanne kati ya hao wakitoa taarifa kutangaza nia katika siku
mbili tofauti Jumapili na Jumatatu katika maeneo tofauti.
0 comments:
Post a Comment