Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akisalimiana Viongozi wa Chama CCM wakati alipowasili Uwanja wa Ndege wa Karume Pemba aliposhiriki katika sherehe za Siku ya Wafanyakazi Duniani zilizofanyika leo Viwanja vya Kiwanda cha Makonyo Wawi Pemba.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akisalimiana Viongozi wa vyama vya Wafanyakazi
wakati alipowasili katika Viwanja vya Kiwanda cha Makonyo
Wawi Pemba katika sherehe za Siku ya Wafanyakazi Duniani zilizofanyika leo.
Wafanyakazi wa Wizara ya Afya Kisiwani Pemba
wakipita mbele ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein alipokuwa akipokea maandamano
ya wafanyakazi wa Taasisi za Serikali na Binafsi wakati
wa Kilele cha sherehe za Siku ya Wafanyakazi Duniani zilizofanyika leo katika
Uwanja wa Kiwanja Kiwanda cha Makonyo Wawi.
Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akisalimiana
na Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mwanajuma Majid wakati alipowasili katika
Uwanja wa Ndege wa Karume Pemba aliposhiriki katika sherehe za Siku ya
Wafanyakazi Duniani zilizofanyika leo Viwanja vya Kiwanda cha Makonyo Wawi
Pemba
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewahakikishia watumishi wa umma kuwa Serikali
itawalipa, mapema kwenye mwaka wa fedha unaoanza Julai 2015/2016, malimbikizo
yao yote ya madai yanayotokana na kasoro zilizojitokeza wakati wa marekebisho
ya mishahara na posho.
Akizungumza na wafanyakzi wakati wa Maadhimisho ya
Siku ya Wafanyakazi Duniani leo yaliyofanyika katika viwanja vya Kiwanda cha
Mkonyo kilichoko Wawi wilaya ya Chakechake Pemba, Dk. Shein amewahakikishia
watumishi hao kuwa Serikali inazifanyia kazi kasoro hizo na kuwahakikisha kuwa
hakuna mtumishi atakayepoteza haki yake.
“Serikali inaendelea kuyahakiki malimbikizo hayo na
tayari tumeshafanya uamuzi wa kuyalipa katika bajeti ya mwaka wa fedha
2015/2016”alisisitiza Mheshimiwa Rais.
Sambamba na kuwahakikishia malipo hayo, Dk. Shein
alibainisha kuwa hatua zote zinazochukuliwa na Serikali kuimarisha hali ya
wafanyakazi lengo lake ni kulifanya suala la kuwapatia maslahi bora watumishi
wa umma liwe ni suala endelevu kadri uchumi unavyoimarika.
Miongoni mwa hatua hizo ambazo amezitaka kuwa ni
miongoni mwa mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Saba katika kuimarisha utumishi
wa umma ni kupitisha sheria mbalimbali zikiwemo Sheria Na. 2 ya Utumishi wa
Umma ya mwaka 2011.
Aidha alieleza kuwa kanuni 12 za Sheria za
Kazi zimetungwa katika kipindi hiki na kuanza kutumika miongoni mwao ni za
Sheria ya Ajira Namba 11, Sheria ya Mahusiano Kazini Namba. 1, zote za mwaka
2015 na Kanuni za mwaka 2014 za Sheria ya Utumishi wa Umma Namba 2 ya mwaka
2011.
Katika mnasaba huo ametoa wito kwa watumishi
na waajiri kusoma vyema na kufahamu Sheria ya Utumishi wa Umma ya Mwaka 2011
kwa kuwa ndio msingi wa mambo yote yanayohusu sheria, maslahi, makosa na adhabu
zake.
Dk.Shein aliwaeleza wafanyakazi hao kuwa
Serikali ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha Sera ya Usalala Kazini ili
kuweka mfumo mzuri wa afya katika maeneo ya kazi kwa lengo la kuwakinga
wafanayakazi na ajali na majanga mengine katika sehemu za kazi.
Kwa hivyo aliwataka watumishi wote nchini
kuendelea kufanyakazi kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za kazi zinavyoelekeza na
kusisitiza kuwa ni lazima katika utendaji wao kuhakikisha kuwa wanatenda haki
na kuwaheshimu wananchi kwa kuwa Serikali yote akiwemo yeye mwenyewe Mheshimiwa
Rais wanawajibika kwa wananchi.
Katika hotuba yake hiyo Dk. Shein aliipongeza
Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi na Utumishi wa Umma kwa kazi nzuri
inayofanya kuratibu na kuweka uhusiano mzuri kati ya Serikali, wafanyakazi na
kusimamia ipasavyo Sera na Sheria mbalimbali zinazohusu kazi na ajira.
Kwa hivyo aliwahakikishia kuwa Serikali
anayoiongoza inazingatia sana umuhimu wa uhusiano huo na siku zote itakuwa
tayari kushirikiana nao kwa lengo la kuzitafutia ufumbuzi changamoto
zinazowakabili wafanyakazi wote Unguja na Pemba.
Katika hatua nyingine Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi amewasihi wafanyakazi na wananchi kwa jumla
kuhakikisha kuwa wanashiriki vyema katika uchaguzi mkuu ujao huku wakizingatia
kuendeleza mafanikio ya kuimarisha amani, umoja na mshikamano.
“Halitakuwa jambo jema utaratibu huu wa
kidemokrasia ukawa ni chanzo cha kuvuruga amani, umoja na mshikamano” Dk. Shein
alisisitiza na kuongeza kuwa aliyedhamiria kutenda lake aseme na nafsi yake
kwanza kabla hajafanya hivyo.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya
Rais, Kazi na Utumishi wa Umma, Mheshimiwa Haroun Ali Suleiman alieleza kuwa
katika kukuza uelewa wa jamii kuhusu sheria za kazi, sheria za kazi za Zanzibar
zimetafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili na wizara hiyo kwa kushirikiana na Shirika
la Kazi Duniani(ILO) imeziweka sheria hizo katika lugha nyepesi.
Waziri Haroun alibainisha kuwa Wizara yake
inaendelea na zoezi la uwekaji wa taarifa za watumishi wa umma katika mfumo wa
kieletroniki hatua ambayo itasaidia katika kuimarishaji wa kutunza kumbukumbu
za taarifa zao na kulinda haki zao wakiwa kazini na baada ya kustaafu.
Aidha Wizara yake alisema imefanikiwa kupunguza
migogoro ya kazi kutoka 179 mwaka 2012/2013 hadi migogoro 102 mwaka 2013/2014.
Awali akizungumza katika hafla hiyo Katibu Mkuu wa
Shirikisho la Wafanyakazi Zanzibar-ZATUC Bwana Khamis Mwinyi Mohamed
alimpongeza Mheshimiwa Rais kwa utayari wake wakati wowote kushirikiana na
Shirikisho hilo kitendo ambacho kimezidi kujenga mahusiano mazuri kati ya
Shirikisho na Serikali.
Aliipongeza Serikali kwa kutoa fursa kwa wafanyakzi
kushiriki katika michakato mbalimbali ya masuala ya kitaifa hivyo kuwafanya
kuwa sehemu ya maamuzi na matokeo yatokanayo na michakato hiyo.
Katibu Mkuu huyo aliiomba serikali kuangalia upya
kodi zinazotozwa wafanyakazi katika mishahara pamoja na malipo ya viinua mgongo
na pensheni.
Nae Mkurugenzi wa Chama cha Waajiri Zanzibar
(ZANEMA) Bwana Salah Salim Salah alisisifu kuzidi kuimarika
kwa mahusiano kati ya waajiri na wafanyakazi jambo ambalo limerahisisha utatuzi
wa migogoro baina ya pande mbili hizo.
Hali hiyo imewezesha kuwepo na mawasiliano na
mashauriano ya mara kwa mara kati ya pande hizo na kuondokana na yale
yaliyotokea zaid ya miaka 126 huko nchini Marekani ambako wafanyakazi walipodai
haki zao walikumbana na kadhia na vurugu zilizosababish baadhi yao kupoteza
maisha.
Mkurugenzi huyo alieleza kuwa mwaka huu ni
mwaka muhimu kwa wajiri na wafanyakazi kama walivyo wananch iwenginek kutokana
na nchi yetu kuelekea Uchaguzi Mkuu kwa kuhakikisha uchaguzi huo haiwi chanzo
cha vurugu ambazo zinaweza kuharibu nchi na uchumi wake.
Katika maadhmisho hayo Mheshimiwa Rais
alikabidhi zawadi mbalimbali kwa watumishi bora kutoka ofisi na taasiii mbalimbali
za umma.
0 comments:
Post a Comment