Rais wa jamhuri ya muungano
wa Tanzania Mh. Dk.Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa serikali yake kwa sasa
haina mpango wa kutoa ajira mpya isipokuwa kuendelea kujenga mazingira mazuri
ya kurahisisha ukuaji wa sekta binafsi na kuvutia wawekezaji kuongeza mitaji
ili kukuza ajira nchini.
Akihutubia kilele cha sherehe
za siku ya wafanyakazi duniani ( MEI MOSI ), zilizofanyika kitaifa katika
uwanja wa CCM KIRUMBA jijini Mwanza, Rais Kikwete pia amewaonya vikali baadhi
ya waajiri binafsi wanaokwepa kulipa viwango vya mishahara vilivyoidhinishwa na
bodi za kisekta na kuagiza chama cha waajiri nchini ( ATE ), kuingilia kati suala
hilo ili kulinda haki za wafanyakazi.
Kuhusu malalamiko ya
wafanyakazi juu ya kukithiri kwa idadi ya wageni wasiokuwa na sifa ya kufanya
kazi nchini, Rais Kikwete amesema tayari serikali imetunga sheria ya udhibiti
wa vibali vya ajira zao ili kuondoa hisia iliyojengeka ya wageni kuchukua
nafasi za ajira hata kwa kazi ambazo wazawa wana uwezo wa kuzifanya.
Rais Kikwete pia amezungumzia
madai ya walimu yanayofikia zaidi ya shilingi bilioni 53 yakiwahusu walimu
70,668 – ambapo amesema kwamba hadi sasa jumla ya walimu 29,243 tayari
wamelipwa shilingi bilioni 23.2, huku walimu 7,169 ambao wanaidai serikali
shilingi bilioni 9.2 wakihaidiwa kulipwa madai yao na serikali ifikapo mwezi Agosti
mwaka huu.
Kwa upande wake katibu mkuu
wa shirikisho la vyama vya wafanyakazi Tanzania ( TUCTA ), Nicholas Mgaya
amesema wafanyakazi wana imani kuwa yapo mambo ambayo serikali ya awamu ya nne
inaweza kuyakamilisha kabla ya kumaliza muda wake ambayo ni pamoja na kulipa
kima cha chini cha awali cha mshahara unaokidhi mahitaji ya msingi cha mwaka
2006 yaani shilingi 315,000 kwa sekta ya umma na kuhakikisha katika sekta
binafsi hakuna mwajiri anayelipa chini ya shilingi 220,000 kwa mwezi, lakini
pia akagusia suala la amani ya nchi.
Kaulimbiu ya siku ya mei mosi
mwaka huu inasema mfanyakazi jiandikishe, kura yako ina thamani kwa maendeleo
yetu.
0 comments:
Post a Comment