Vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoendelea Sudan
kusini vimesababisha janga la kibinaadamu. Hadi watu milioni mbili wanayakimbia
mapigano na mashirika ya kutoa misaada yanaonya juu ya kutokea janga kubwa la
kibinaadamu.
Mapigano makali yamezuka tena katika eneo la kaskazini
la Sudan Kusini lenye utajiri mkubwa wa mafuta. Raia wanaoweza kukimbia
wanalihama eneo hilo kuyanusuru maisha yao. Hata mashirika mengi ya kutoa
misaada yameondoka eneo hilo na mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya
mzozo wa Sudan Kusini Toby Lanzer amesema kwa kwa sababu hiyo watu takriban
500,000 hawana msaada.
Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa zaidi ya
asilimia 50 ya wakazi milioni kumi na mbili wa Sudan Kusini wanahitaji msaada
wa kibinaadamu.
Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu
imethibitisha kwamba watoaji misaada wanaweza kuifikia idadi ndogo tu ya watu
wanaohitaji msaada kwa dharura. Kukosekana msimu wa kupanda kutokana na vita
kunazidisha hali kubwa mbaya, amesema Pawel Krzysiek, mfanyakazi wa shirika
hilo katika mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba, wakati alipozungumza na DW.
"Wasiwasi mkubwa wa Kamati ya Kimataifa ya
Msalaba Mwekundu ni mustakabali wa raia. Tuko katika msimu wa mvua ambapo watu
walitakiwa kupanda mazao yao ili baadaye waje kuvuna chakula chao, lakini
shughuli zao za kilimo zimetatizwa."
Krzysiek amesema watoto ambao familia zao
zimelazimika kuyakimbia mapigano ndio wanaokabiliwa na hali ngumu zaidi. Kamati
ya Msalaba Mwekundu inasema watoto 250,000 wanakabiliwa na utapiamlo.
Umoja wa Mataifa umeonya kuhusu wimbi jipya la
mateso dhidi ya watoto. Shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia watoto,
UNICEF, limesema watoto kadhaa waliuwawa wiki iliyopita katika jimbo la Unity
na makundi ya watu waliojihami na silaha. Watoto wengine walibakwa, kutekwa
nyara au kusajiliwa kwa nguvu na kulazimishwa kujiunga na makundi ya
wapiganaji.
Jonathan Veitch wa shirika la UNICEF amenukuliwa
akisema baadhi ya washambuliaji ni watoto wa umri wa miaka 16. "Baadhi ya
wapiganaji walieleza kwamba inafaa kuwaua watoto kabla wakue na kurejea
kulipiza kisasi," alisema Veitch wakati wa mkutano kwa vyombo vya habari
mjini Geneva kupitia simu akiwa mjini Juba. Umoja wa Mataifa unakadiria watoto
13,000 wamesajiliwa kuwa wapiganaji na pande zote mbili za mzozo wa Sudan
Kusini.
Hospitali hatarini
Katika eneo la Kodok kaskazini mwa Malakal Shirika
la Msalaba Mwekundu linadhimini hospitali. Lakini kutokana na mapigano
yanayoendelea limelazimika kupunguza shughuli katika hospitali hiyo.
"Kutokana na mapigano tulilazimika kuondoa
sehemu ya wafanyakazi wetu kutoka eneo hilo na kuwapeleka katika eneo lililo
salama. Huo ni uamuzi mkubwa usiotarajiwa kwa sababu hospitali hii ni muhimu
sana kwa otoaji wa huduma za afya kwa watu wa eneo hili," alisema
Krzysiek.
Takriban wagonjwa 600 walikuwa wakipokea matibabu
katika hospitali hiyo kila wiki, hususan watoto. "Athari zaidi
zinatarajiwa kushuhudiwa wakati vita vitakapomalizika ghafla na msaada wa
kimataifa utakapopunguzwa kwa kiwango kikubwa," ameongeza kusema Pawel
Krzysie. Anafahamu fika kuwa hilo halitatokeo kwa haraka.
Wakati mashirika ya misaada yakiendelea kuhimiza
amani ili yaweza kusambaza misaada kwa raia, serikali ya Sudan Kusini ilipokea
silaha za za thamani ya dola milioni 38 mwaka jana kutoka kwa China ambazo imezilipia
kutumia mafuta.
Ukiukaji mkubwa wa haki za binaadamu
Jeshi la Sudan Kusini limenyoshewa kidole cha lawama
kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binaadamu wakati wa operesheni yake ya kupambana
na waasi iliyoanza mwishoni mwa mwezi uliopita katika jimbo la kaskazini la
Unity na kuenea katika majimbo ya Jonglei na Upper Nile. Katika tangazo lake
Shirika la Maendeleo la Mashariki na Pembe ya Afrika, IGAD, lilisema jeshi hilo
liliwapiga raia, kuviharibu vijiji na kufanya vitendo viovu na visivyokubalika.
Shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights
Watch limesema vyombo vya usalama vya Sudan Kusini vinazikanyaga haki za
binaadamu katika operesheni zao. Leslie Lefkow, afisa wa shirika hilo mjini
Abidjan nchini Cote d'Ivoire amesema wafungwa wanazuiwa na kuteswa bila
kutambuliwa Sudan Kusini.
"Shirika la Human Rights Watch limeorodhesha
matukio kadhaa ambapo jeshi na idara ya usalama ya kitaifa wamewazuia na wakati
mwingine kuwatesa wafungwa katika mwezi uliopita. Udhalilishaji huu unafanyika
wakati kukiwa na mashambulizi dhidi ya raia yanayofanywa na pande zinazopigana
Sudan Kusini."
Leslie amesema mbali na vita vinavyoendelea ni
muhimu pia kufanyike mageuzi ya sheria Sudan Kusini ili kudhibiti mamlaka ya
jeshi na vyombo vya usalama. Msemaji wa jeshi la Sudan Kusini Philip Aguer
amekanusha madai yote ya ukiukaji wa haki za binaadamu, akisema jeshi
linajilinda na kufuata utaratibu wa kutowashambulia raia.
Mwandishi:Cascais, Antonio (HA Afrika)
Tafsiri:Josephat Charo
Mhariri:Iddi Ssessanga




0 comments:
Post a Comment