Kamati ya kudumu ya bunge ya ardhi maliasili na
mazingira kwa mara nyingine tena imekataa kujadili bajeti ya wizara ya
maliasili na utalii kwa madai kuwa wizara hiyo haijatekeleza maelekezo ya bunge
yanayolenga kuimarisha shughuli za uhifadhi nchini na kuongeza mapato ya
serikali yanayotakiwa kutumika kwa shughuli za maendeleo ya jamii na taifa.
Akiongea jijini Dar es Salaam muda mfupi baada ya
mkutano kati ya wizara na kamati hiyo kuvunjika, mwenyekiti wa kamati ya kudumu
ya bunge ya ardhi maliasili na mazingira James Lembeli amesema wizara imekwenda
kinyume na maagizo ya kamati kuhusu kurekebisha mipaka ya hifadhi ya taifa ya
sadani na hifadhi ya taifa ya ruaha kinyemelea bila kufuata taratibu za
kisheria na pia kuchelewa kuridhia viwango vya tozo za utalii kwa shirika la
hifadhi za taifa Tanzania TANAPA na mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro utaratibu
ambao unaikosesha serikali fedha nyingi mpango ambao amesema usipodhibitiwa utaua
uhifadhi ambao umekuwa na mchango mkubwa kwa pato la taifa.
Nao baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo akiwemo Mary
Mwanjelwa na Grace Kiwelu wamesema uamuzi wa kukataa kujadili bajeti hiyo
umefikiwa na wajumbe wote wa kamati hiyo na umezingatia maslahi ya taifa bila
kujali itikadi za vyama na kwamba wizara ya maliasili na utalii sasa imetakiwa
kupeleka maelezo ya kuridhisha mjini dodoma mei 14 mwaka huu vinginevyo
hawatakuwa tayari kujadili wala kuipitisha bajeti ya wizara hiyo.
Akiongea kuhusu mgogoro huo ambao umesababisha
bajeti ya wizara yake kushindwa kujadiliwa na kamati chini ya utaratibu wa
kawaida,waziri wa maliasili na utalii Lazaro Nyalandu amesema serikali imepokea
maelekezo ya kamati baada ya kuomba ipewe muda wa kuandaa majibu ambayo sasa
yatawasilishwa mbele ya kamati mjini dodoma wiki ijayo.
0 comments:
Post a Comment