WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema Serikali
imeanzisha Kurugenzi ya Wauguzi na Wakunga katika Wizara ya Afya na Ustawi wa
Jamii ili kurahisisha utatuzi wa changamoto zinazowakabili kwenye utoaji
wa huduma kwa umma.
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumanne, Mei 5, 2015),
wakati akizungumza wauguzi na wakunga pamoja na wakazi wa mkoa wa Mara kwenye
kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wakunga Duniani yaliyofanyika kwenye
viwanja vya Mkendo, mjini Musoma.
“Nina taarifa kuwa kuanzia mwaka ujao wa fedha
(2015/2016), Kurugenzi hiyo itakuwa na bajeti yake yenyewe itakayotumika
kuboresha huduma za wauguzi na wakunga nchini. Haya yote yanafanyika kwa kuwa
Serikali inatambua na kuthamini shughuli za wauguzi na wakunga hapa nchini,”
alisema.
Alisema mafanikio yaliyofikiwa ya kupunguza vifo vya
watoto na vifo vya wanawake yamechangiwa na kazi nzuri zinazofanywa na wakunga
licha ya kuwa kada hiyo inakabiliwa na upungufu mkubwa wa watumishi.
Alisema ili kukidhi mahitaji ya wakunga nchini,
Serikali imeongeza idadi ya wanafunzi wanaojiunga na fani ya uuguzi na ukunga.
Akitolea mfano, Waziri Mkuu alisema: “Mwaka 2009 tulikuwa na wanafunzi wa
uuguzi na ukunga 617 wa ngazi ya Cheti na 925 wa ngazi ya Diploma. Kufikia
mwaka 2014 idadi hiyo iliongezeka kufikia wanafunzi 2,566 wa Cheti sawa na
ongezeko la asilimia 315 na wanafunzi 2,294 wa Diploma sawa na ongezeko la
asilimia 141 katika kipindi cha miaka mitano.”
Akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na hadhara
hiyo, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi Jamii, Dk. Stephen Kebwe alisema Tanzania
ni miongoni mwa nchi tano barani Afrika ambazo zimeweza kupunguza vifo vya
watoto na kuvuka Malengo ya Milenia.
Alitumia fursa hiyo kuwahimiza wanaume wa mkoa huo
na wanaume wote nchini kukubali kutumia njia za uzazi wa mpango ili wawasadie
wenza wao kuwa na afya imara. Pia aliwataka waachane na dhana potofu za mitaani
bali wafuate tiba na huduma sahihi uzazi wa mpango kwenye vituo vya afya.
“Inashangaza kuona baadhi ya wanaume wanawaacha wake
zao eti kwa sababu hawazai, lakini wakiwaacha baada ya muda unasikia yule mama
amepata ujauzito, hapo kosa ni la nani?” aliuliza.
“Pia ninawasihi akinababa waachane na dhana potofu
kuhusu njia ya kufunga kizazi. Ninawahimiza washiriki njia hii ya kufunga
kizazi wanaposhauriwa kufanya hivyo kwa sababu kufunga ule mrija hakumuondolei
mwanaume hadhi ya kufanya tendo la ndoa, bado inawezekana hata baada ya kufunga
mrija,” alisisitiza.
Mapema, akitoa salamu kwenye maadhimisho hayo,
Mkurugenzi Mkazi wa taasisi ya Mama Ye, Bw. Craig Ferla aliitaka Serikali na
wadau waliangalie suala la vifo vya akinamama na watoto kwa jicho la tofauti na
kulipigia kelele zaidi ili uwekezaji kwenye fani ya ukunga na uuguzi uweze
kuongezwa.
Bw. Ferla ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Utepe
Mweupe wa Muungano wa Uzazi Salama Tanzania, alisema Serikali na wadau
mbalimbali wamekuwa wakipigia kelele idadi ya vifo vinavyotokana na ajali za
barabarani lakini hakuna mtu anayesema chochote kuhusu vifo vya wanawake na
watoto wachanga.
“Watu wanapiga kelele kuwa Taifa limepoteza watu 972
kati ya Januari na Aprili mwaka huu, lakini hatujui kwamba katika kipindi hicho
hicho Taifa limepoteza wanawake na watoto 15,000 kutokana na matatizo ya uzazi
na hii ni mara 15 zaidi lakini hakuna anayepiga kelele,” alifafanua.
Alisema wanawake 8,000 hupoteza maisha kila mwaka
kutokana na uzazi wakati watoto 40,000 hupoteza maisha wakiwa katika mwezi wao
wa kwanza duniani. “Vifo vya ebola tangu ianze vimefikia 10,000 lakini dunia
nzima imeitikia lakini hivi vya akinamama hakuna anayesema chochote.”
“Kuna tatizo jingine ambalo linakwenda kimyakimya
nalo ni la vifo vya watoto wanaozaliwa wafu. Hawa wanafikia 47,000 kwa mwaka
ambao ni karibu watoto 15,000 kwa miezi minne lakini nalo pia hakuna
anayelisemea licha ya kuwa ni janga kubwa kitaifa,” aliongeza.
“Ninaiomba Serikali na wadau wawekeze zaidi katika
kada ya wakunga ili tuweze kuokoa maisha ya akinamama na watoto,” alisema
Mkurugenzi huyo ambaye kwa muda wote alitumia Kiswahili fasaha na kuufanya
mkutano mzima umshangilie kwa nguvu.
(mwisho)
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM
JUMANNE, MEI 5, 2015.
Irene K. Bwire
0 comments:
Post a Comment