Kampeni hiyo ilizinduliwa
jana katika kituo cha mabasi yaendayo mikoani cha Ubungo (UBT) jijini Dar es
Salaam, ikishirikisha madereva na wadau wengine mbalimbali wa sekta ya usafiri.
Wafanyakazi wa ITV/Radio One pamoja na Vodacom walishiriki kazi ya kubandika
stika zinazohamasisha kampeni hiyo, wakiongozwa na Kamanda wa Kikosi cha
Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga. Kampeni hiyo inatambulishwa na kauli mbiu
isemayo, 'Zuia ajali sasa, toa taarifa mapema'; lengo likiwa ni kuhamasiha umma
kwa asilimia mia moja katika kuhakikisha kuwa ajali za barabarani nchini
zinapungua kwa kiwango kikubwa.
Ilielezwa kuwa utekelezaji wa
kampeni hiyo utawahusisha zaidi wananchi, ambao wamepewa namba ya simu ya
mkononi ya 0800 757575 ili kupiga bure kwa nia ya kutoa taarifa. Kwamba, ikiwa
wataona kuna madereva wanakiuka sheria za usalama barabarani na kuendesha
mabasi kwa mwendokasi unaohatarisha usalama wao, watoe taarifa kupitia namba
hiyo.
Aidha, ilifafanuliwa zaidi
kuwa miongoni mwa hatua zitakazochukuliwa baada ya hapo ni pamoja na
kupigwa picha za madereva husika pamoja na mabasi yao, ambazo zitarushwa moja
kwa moja kupitia vituo vya ITV na Radio One pamoja na Capital Radio; na
kisha polisi watawakamata kabla hatua zaidi za kisheria kuchukuliwa.
Hakika, sisi tunaunga mkono
kampeni hii. Tunaiunga mkono kwa sababu yenyewe inaonekana kuwa ni tofauti
kulinganisha na kampeni kadhaa zilizowahi kuwapo hapo kabla, hii ikienda mbali
zaidi kwa kuwaanika madereva wanaohusika katika kuvunja sheria na pia mabasi
yao. Ni wazi kuwa mafanikio ya kampeni hii yatasaidia kwa kiwango kikubwa
kupunguza ajali nchini kwani ni wazi kuwa hakuna dereva atakayependa kuonekani
kila mmoja kupitia televisheni na kutangazwa jina lake redioni kuwa yeye ni
mkorofi. Kwa sababu hiyo, kama ushirikiano utakuwa wa kutosha, madereva wa
mabasi watabadili nyendo zao na kuzingatia sheria.
Isitoshe, ni imani yetu
vilevile kwamba hakutakuwa na mmiliki wa basi atakayevumilia kuwa na dereva
mvunja sheria kwani madhara ya kuwa na madereva wa aina hiyo yanafahamika,
mojawapo ikiwa ni kuharibiwa kwa mali yake (basi). Ushiriki wa polisi utasaidia
pia kufanikisha kampeni hii kwani madereva wakorofi watakamatwa na kuchukuliwa
hatua.
Kwa kuzingatia yote hayo,
ndipo nasi tunapoona kuwa sasa kuna kila sababu kwa wananchi na wadau wengine
wote wa usalama barabarani kuunga mkono kampeni hii. Abiria watekeleze wajibu
wao kwa kupiga namba hiyo ya bure na kutoa taarifa za madereva wavunjao sheria.
Hili ni jambo muhimu kuzingatiwa kwani kwa kufanya hivyo, ni wazi kwamba janga
hili litapata dawa.
Tunasisitiza umuhimu wa
kuunga mkono kampeni hii kutokana na ukweli kuwa hivi sasa, watu wengi
wasiokuwa na hatia hupoteza maisha kila uchao.
Wapo pia wanaopata ulemavu wa
kudumu kutokana na ajali hizi ambazo kimsingi, nyingi husababishwa na madereva
wasiozingatia sheria za usalama barabarani.
Kwa mfano, rekodi za Kikosi
cha Usalama Barabarani zinaonyesha kuwa mwaka 2013, katika kipindi cha kuanzia
Januari hadi Juni peke yake, taifa lilikumbwa na ajali za barabarani 11,311,
ambazo zilisababisha maafa ya watu 1,739 na majeruhi 9,889. Kipindi cha Januari
hadi Juni 2014, ajali zilizotokea nchini zilikuwa 8,405, zikigharimu maisha ya
watu 1,743 na majeruhi 7,523. Mwaka huu hali siyo nzuri pia kwani kuanzia
Januari Mosi hadi Aprili Mosi peke yake, tayari watu 969 wameshafariki dunia.
Hali hii haipaswi kuachwa hata kidogo. Ni lazima jitihada za ziada zifanyike
kuhakikisha kwamba ajali zinapungua.
Tunasisitiza kuwa
kampeni hii ya 'Zuia ajali sasa' iungwe mkono kwa kila hali. Kwa kufanya hivyo,
ni wazi kwamba janga hili la ajali za barabarani litapatiwa dawa. Idadi ya vifo
vya watu wasiokuwa na hatia na pia ile ya watu wanaosababishiwa ulemavu wa
kudumu itapungua kwa kiasi kikubwa. Shime, kila mmoja aunge mkono kampeni hii
ya 'Zuia ajali sasa, toa taarifa mapema'.
0 comments:
Post a Comment