WHO imesema visa vipya vya kipindupindu kwa
siku vimepungua kutoka 915 tarehe 18 mwezi huu hadi 100 kwa sasa na hali hiyo
imesababishwa na hatua zilizochukuliwa kudhibiti mlipuko ikiwemo kuimarisha
huduma za kujisafi.
WHO inasema harakati za kudhibiti
Kipindupindu zinafanywa kwa ushirikiano baina ya serikali ya Tanzania na wadau
kama vile Umoja wa Mataifa na madaktari wasio na mipaka, MSF.
Dokta Rufaro Chatora ni mwakilishi wa WHO
nchini Tanzania.
“Licha ya
visa vya kipindupindu kushuka katika siku chache zilizopita, hali bado
ni mbaya mno, mbali na kipindupindu sisi pia tunasimamia shughuli zingine za
kiafya mathalani kwa siku kuna wazazi 72 wanajifungua na kati yao 17 ni Kagunga.”
Wakati huo huo shirika la kuhudumia
wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR limesema idadi ya wakimbizi wa Burundi
wanaoingia Tanzania imepungua kama anavyoeleza msemaji wake Adrian Edwards.
“Kazi
inafanywa ili kupanua uwezo wa kambi katika ukanda mzima, mmiminiko wa
wakimbizi kutoka Burundi haujapungua lakini kiwango sasa kimepungua na tunapata
wakimbizi 100 kwa siku katika nchi zinazopokea wakimbizi, tukizingatia takwimu
mpya tumepokea zaidi ya wakimbizi 90,000 katika ukanda huu, ikiwa ni pamoja na
10,000 DRC, 47,000 Tanzania na 28,000 Rwanda na 5,500 Uganda. “
Umoja wa Mataifa unasema kijiji cha Kagunga
ambacho ndio kilikuwa kitovu cha mlipuko sasa wakimbizi wote wanakaribiwa
kuondolewa ili kazi ya kupulizia dawa kukinga maambukizi mapya iweze kufanyika.


0 comments:
Post a Comment