KIRAKA mpya wa Yanga, Deus Kaseke, ametua klabuni hapo
na mkwara wa mwaka.
Baada ya kutambulishwa tu, kiungo huyo akatamka
mambo mawili. Kwanza, ametaka apewe jezi namba nne ambayo tayari Yanga wamempa,
lakini pili anataka kocha amchezeshe winga wa kushoto, ili aweze kuifanyia
makubwa klabu hiyo.
Habari za ndani ya Yanga awali zilisema kuwa Kaseke
aliutaka uongozi umpe jezi hiyo kwani inampa nafasi ya kujisikia huru zaidi,
lakini namba hiyo ilikuwa ikitumiwa na beki wa kati Rajab Zahir ambaye yupo
kwenye mazungumzo ya mwisho na Yanga ili kuongeza mkataba mpya.
“Mbali na kutaka apewe jezi namba 4 pia anasisitiza
angependa kucheza winga wa kushoto akidai inamfanya ajiamini na kuisaidia timu
kupata mabao kwani pia ni mfungaji mzuri,” kilisema chanzo hicho.
“Katika suala hilo la jezi ndio utata zaidi kwani
viongozi walimgomea kwa madai tayari inayo mtu ambaye ni Rajab Zahir, ambaye
uongozi unaendelea kuzungumza naye kwa ajili ya usajili wa mkataba mpya.”
Hata hivyo katika mkutano wao na wanahabari mchana
wa jana, uongozi wa Yanga ulifichua kuwa umempa kiungo huyo mpya mkataba wa
mwaka mmoja na kuridhia ombi lake la kutaka apewe jezi namba 4 kama alivyotaka.
“Kaseke atavaa jezi namba 4 na mkataba wake ni wa
mwaka mmoja. Wengine ambao mpaka sasa tumewasajili ni kipa Deo Munishi ‘Dida’
ambaye tumempa mktaba wa miaka miwili kama ilivyo kwa Haruna Niyonzima, huku
Mbuyu Twite akipewa mkataba wa mwaka mmoja,” alisema Meneja wa Yanga, Hafidh
Saleh.
Aidha menejja huyo aliweka bayana kwamba Yanga
itaanza kambi ya mazoezi kujiandaa na msimu mpya Juni 8, ikiwa ni siku mbili tu
tangu Kocha Mkuu, Hans Pluijm kurejea kutoka kwenye mapumziko nyumbani kwake
Ghana.
Katika hatua nyingine, Yanga inajipanga kuhakikisha
inafanya kweli katika mashindano ya Kombe la Kagame, ikipiga mahesabu ya
kuzishusha timu tatu kubwa barani Afrika za Zesco ya Zambia, TP Mazembe na
Mamelodi Sundwons ya Afrika Kusini, ili kufanya mashindano mafupi.


0 comments:
Post a Comment