Image
Image

Mataifa yashughulikie changamoto za Burundi.


Tumeandika mara kadhaa kuhusu hali ya amani ilivyotetereka Burundi. Mara zote tumejitahidi kutoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuongeza juhudi za usuluhishi na upatanishi kati ya wapinzani na Serikali ya Burundi ili isiendelee kuzalisha wakimbizi.
Tunatambua kwamba viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) walikutana Dar es Salaam, wiki mbili zilizopita, kwa lengo la kujadili mgogoro wa Burundi. Tunatambua pia kwamba siku waliyokutana ndiyo lilitokea jaribio la kumpindua Rais Pierre Nkurunziza, hali ambayo ilivuruga hata ajenda na maazimio ya kikao.
Badala ya kutoka na maazimio mazito yenye lengo la kuupatia ufumbuzi mgogoro ulioibuka kutokana na Rais wa nchi hiyo kutaka kuwania muhula wa tatu wa uongozi kinyume cha Katiba yao, waliishia kulaani jaribio la mapinduzi ambalo licha ya kushindikana, lilichochea maandamano zaidi, mapambano zaidi kati ya askari na raia na mauaji zaidi.
Taarifa zilizopo zinaonyesha kwamba zaidi ya watu 20 wameuawa na wengine zaidi ya 431 kujeruhiwa huku mamia kwa maelfu ya raia wa Burundi wakikimbia kuwa wakimbizi katika nchi za Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na Tanzania.
Haya yote yanatokea kwa sababu ya kukiukwa kwa Makubaliano ya Amani yaliyofikiwa mjini Arusha kwamba kiongozi mkuu wa nchi hatakaa madarakani kwa zaidi ya vipindi viwili vya miaka mitano mitano. Wananchi wanaotaka makubaliano hayo ya amani yaheshimiwe, baada ya rais huyo kutawala vipindi viwili vya miaka mitano mitano, ndiyo wanaoandamana na baadhi yao kuishia kupigwa risasi; wanajeruhiwa na kuuawa.
Madhara ya uamuzi huo ni kumiminika kwa wakimbizi katika nchi jirani. Mazingira yamewafanya Warundi kuitoroka nchi yao wakiwa hawana chakula, fedha, nguo, matandiko wala dawa na wakitembea usiku kucha kwa ajili ya kusalimisha roho zao.
Kwa hiyo, Tanzania iliyoshiriki kikamilifu kurejesha amani Burundi kufuatia machafuko ya mwaka 1994, inalazimika kuwapokea tena wakimbizi ambao taarifa zinaonyesha wamefikia zaidi ya 100,000. Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) ndilo linalopaswa kuwaangalia wakimbizi hao, lakini maadamu wako nchini, huu ni mzigo mkubwa kwa Tanzania.
Kumekuwa na propaganda nyingi za kutaka kuonyesha kwamba Burundi kuko shwari isipokuwa wakorofi wachache. Propaganda hizo ni pamoja na mechi iliyoandaliwa Alhamisi iliyopita jijini Bujumbura ambayo ili kuonyesha kwamba kuna amani ya kutosha na Rais alionekana akicheza mpira, lakini Jumapili kiongozi wa chama cha upinzani cha Union for Peace and Develoment, Zedi Feruzi na mlinzi wake waliuawa kwa risasi.
Katika nchi yenye amani hakuna mauaji ya kiholela; katika nchi yenye utulivu raia hawakimbii na kwenda kuishi kama wakimbizi; katika nchi inayojali haki, chama tawala hakiwezi kuunda vikundi vya kupiga watu wanaopinga sera za Serikali. Vilevile, nchi inayojali utawala bora haifungii wala kuvipiga mabomu vyombo vya habari vya binafsi na nchi inayojali watu wake haiwezi kuwaacha watembee mwendo mrefu na kufia ugenini tena kwa magonjwa yanayozuilika kama kipindupindu.
Tunaiomba jumuiya ya kimataifa iongeze juhudi za kuwasaidia wakimbizi walioko nchini ambao wanakabiliwa na hali ngumu lakini zaidi tunaomba ziongezwe juhudi kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Burundi ili isiendelee kuzalisha wakimbizi.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment