Hata hivyo mazungumzo juu ya kulipitisha azimio
linaloufafanua mpango wa kuutekeleza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo,
yaligonga mwamba baada ya nchi za kiarabu kutaka mkutano uitishwe ili
kulijadili suala la kuifanya Mashariki ya Kati liwe eneo pasipo na silaha hizo.
Nchi za kiarabu zilitaka mkutano huo uitishwe mapema
mwaka ujao. Lakini Marekani na washirika wake wamelipinga pendekezo hilo. Israel
iliyohudhuria mazungumzo hayo kwenye Umoja wa Mataifa, ingawa haijautia saini
mkataba wa kuzuia uenezaji wa silaha za nyuklia ililipinga pendekezo la nchi za
kiarabu.
Inaaminika kwamba Israel ndiyo nchi pekee yenye
silaha za nyuklia katika Mashariki ya Kati lakini haijakiri kuwa na silaha
hizo. Naibu Waziri wa Marekani wa udhibiti wa silaha Rose Gottemoeller amesema
pendekezo la kuitisha mkutano linaenda kinyume na malengo ya muda mrefu ya nchi
yake.
Gottemoeller amehoji kwamba pendekezo juu ya kupiga marufuku
silaha za nyuklia katika Mashariki ya Kati halina matumiani ya kukubaliwa na
nchi zote.
Marekani imesema Misri na nchi nyingine za kiarabu
zinajaribu kuuteka nyara mchakato wa mazungumzo kwa kuiwekea Israel masharti.
Wajumbe
watoa mwito kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon.
Wajumbe waliokutana kwenye Umoja wa Mataifa
kuitathmini hatua iliyofikiwa katika kuutekeleza mkataba juu ya kupiga marufuku
silaha za nyuklia walitoa mwito kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa kuitisha
mkutano mapema mwaka ujao bila ya kujali iwapo Israel na jirani zake
wanakubaliana na ajenda ya mkutano. Kutokana na mkutano huo Israel inaweza
kulazimika kukiri kwamba inazo silaha za nyuklia.




0 comments:
Post a Comment