KIUNGO tegemeo wa Simba, Jonas Mkude, amewaambia
viongozi wake wasithubutu kumwacha kipa wao mzoefu Ivo Mapunda.
Mkude amesema: “Mapunda bado ana mchango mkubwa
katika timu, kwanza katika msimu uliomalizika ameweza kuokoa hatari nyingi
ambazo pengine kama si yeye timu ingemaliza ikiwa kwenye nafasi mbaya.”
Ingawa viongozi wa usajili wa Simba wanadaiwa
kugawanyika kuhusu kumpa mkataba Ivo, Mkude alisema ni vizuri viongozi wake
wakalitazama jambo hilo kwa jicho la mbali kwani uwepo wake ni muhimu kuliko
kuwaacha makipa ambao bado hawana uzoefu wa kutosha.
“Ni kweli kuna makipa chipukizi, lakini bado
wanahitaji msaada wa wakongwe kwani watawaongoza namna ya kufanya vizuri
kuhakikisha wanakuwa manufaa kwa timu kwa miaka ijayo,” alisema.
“Ndio maana mpaka kesho nikuulizwa ni mkongwe
gani arudishwe Simba, nitakutajia Mwinyi Kazimoto, kwani pengo lake
bado linaloonekana.”
Mkude alisema mbali ya uwezo alionao Mapunda,
lakini pia amekuwa mshauri mzuri kwa vijana katika kuwajenga namna ambavyo
wanaweza kufika mbali zaidi katika maisha ya soka.
“Siingilii majukumu ya viongozi wangu, lakini kuhusu
Mapunda wakimwacha pengo lake halitazibwa kwani ni muda mwafaka kwa makipa
chipukizi kujifunza mambo mengi kwa Mapunda,” alisema.
Hakusita kutoa ya moyoni kwamba umakini wa
hali ya juu unatakiwa kwenye kikosi chao ili kuwalinda wachezaji wenye mchango.


0 comments:
Post a Comment