Katika taarifa kwa mnasaba wa Siku ya Afrika ambayo
inaadhimishwa leo, Mugabe ambaye pia ni mwenyekiti wa Umoja wa Afrika amesema
Waafrika wana jukumu nzito sana la kukabiliana na sera za wakoloni mambo leo
ambao wanataka kuvuruga ustawi wa kiuchumi na kisiasa ambao umepatiakana barani
Afrika tokea ukoloni usambaratishwe.
Amesema Umoja wa Afrika umechukua hatua
imara kiuchumi na kisiasa kwa lengo la kulinda mustakabali wa Afrika.
Amesema
Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika limechukua hatua za kuleta amani
na usalama katika bara hilo .
Mugabe amesema muungano wa kiuchumi baina ya
nchi za Afrika ni stratijia ya dharura katika kuleta maendeleo ya kijamii na
kiuchumi barani humo.
Rais wa Zimbabwe amesema bara Afrika lina utajiri mkubwa
wa madini na kilimo na iwapo utajiri huo utatumiwa ipasvyo maisha ya watu
barani humo yataboreka kupitia kuangamizwa njaa, umasikini na maradhi.
Huku
akiashiria kuhusu wimbi la Waafrika wanaopoteza maisha wakivuka Bahari ya
Mediterranea wakitafuta maisha bora Ulaya,Mugabe ametoa wito kwa viongozi wa
Afrika kuchukua hatua ya kuondoa taswira mbaya ya Afrika.
Mugabe
amekumbusha kuwa Waafrika wanakimbilia nchi za Ulaya ambazo zimetajirika
kutokana na uporaji wa rasilimali za bara Afrika.


0 comments:
Post a Comment