Mkutano huo
wa kwanza wa Jopo hilo unafanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi za
Sekretariati ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ya Jopo la Watu Maarufu Duniani
kwenye Jumba la North Lawn Building katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa
ambako Rais Kikwete atakuwa na ofisi zake za muda wakati anaongoza Jopo hilo.
Rais Kikwete
ambaye amewasili New York asubuhi ya leo, Jumatatu, Mei 4, 2015 baada ya safari
ndefu kutoka Dar es Salaam, ataendesha kikao cha Jopo hilo kwa siku nne mfululizo
kufuatia uamuzi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mheshimiwa Ban Ki Mooon, mwezi
uliopita wa kuteua Jopo la Watu Wanaojitegemea na Maarufu Duniani kuunda Jopo
la kutafuta njia ya kukabiliana na balaa la magonjwa ya milipuko katika miaka
ijayo.
Wajumbe
wengine wa Jopo hilo ni pamoja na Bwana Celso Luiz Nunes Amorimo, Waziri wa zamani
wa Mambo ya Nje (1993-1994 na 2003-2010)
na Waziri wa zamani wa Ulinzi wa Brazil; Bi. Micheline Calmy-Rey, Rais wa
zamani wa Muungano wa Uswisi na Bwana Marty Natalegawa, Waziri wa zamani wa
Mambo ya Nje na Mwakilishi wa Kudumu wa Indonesia katika Umoja wa Mataifa,
mjini New York.
Wengine ni
Bi. Joy Phumaphi, Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Viongozi wa Afrika Kukabiliana na Malaria ya African
Leaders Malaria Alliance na Waziri wa zamani wa Afya na Waziri wa Ardhi na
Nyumba wa Botswana na Bwana Rajiv Shah, ambaye
mpaka Januari mwaka huu alikuwa Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la
Marekani (USAID).
Wajumbe wa
Jopo ambao wameteuliwa katika nafsi na uwezo wao wenyewe, wametakiwa na Katibu
Mkuu Ban Ki Moon kutoa mapendekezo ya jinsi ya kuimarisha mifumo ya kitaifa na
kimataifa ili kuzuia ama kuipa dunia uwezo zaidi wa kudhibiti mabalaa ya
magonjwa ya milipuko katika siku zijazo kwa kutilia maanani mafunzo
yaliyotokana na mlipuko wa Ebola.
Kwa hakika,
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aliteua Jopo hilo kufuatia mlipuko wa Ebola
katika Afrika Magharibi, ambao haraka haraka ulitokea kuwa mmoja wa milipuko
hatari zaidi duniani kwa afya ya umma katika historia ya dunia, ukisababisha
ugonjwa kwa maelfu ya watu na kusababisha matatizo makubwa ya kijamii na
kiuchumi. Kusambaa kwa ugonjwa huo katika Guinea, Liberia na Sierra Leone
kumethibitisha umuhimu na uharaka wa kuimarisha mfumo na menejimenti ya mabalaa
ya magonjwa ya mlipuko duniani, ili kuweza kukabiliana vizuri zaidi na milipuko
ya namna hiyo katika siku zijazo.
Kabla ya
kuanza kikao chao, Wajumbe wa Jopo wamekutana na kufanya mazungumzo na Katibu
Mkuu Ban Ki Moon, ambaye tayari amewaomba kuwa wanatoa ripoti za mara kwa mara
kuhusu kazi yao na hatimaye kutoa Ripoti ya Mwisho Desemba mwaka huu, 2015.
Katibu Mkuu ataiwasilisha Ripoti hiyo kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
mwishoni mwa Desemba mwaka huu. Aidha, maamuzi mwafaka yatachukuliwa kutokana
na mapendekezo ya Jopo hilo.
Katika
kufanya kazi yake, Jopo litawasilisha na makundi mbali mbali ya watu, wakiwemo
wawakilishi wa nchi na jamii zilizoathiriwa na Ebola, mifumo ya Umoja wa
Mataifa, taasisi za fedha za kimataifa na kitaifa, taasisi za benki za
maendeleo za kikanda, mashirika yasiyokuwa ya kimataifa, nchi zilizounga mkono
mapambano dhidi ya Ebola, wafanyakazi wa afya, taasisi za kisomi na kitafiti,
nchi nyingine wanachama wa UN, sekta binafsi na wataalam wengine.
Umoja wa
Mataifa umetoa sekretarieti kwa ajili ya kusaidia kazi ya Jopo, ambalo pia lina
uhuru wa kuwasilisha na kukutana na wataalam waandamizi wa kundi la Wataalam la
Umoja wa Mataifa, ambalo hutoa ushauri wa kiufundi na masuala mengine kulingana
na mahitaji ya Jopo.
Kufuatia
mkutano huo wa kwanza, Jopo sasa linaweka mikakati ya namna ya kufanya kazi na
mpango wa kazi kwa kushauriana na Katibu Mkuu. Jopo linatarajiwa kukutana kila
baada ya wiki sita, mikutano mitatu ikiwa inafanyika New York, mmoja kwenye
Ofisi za UN nchini Uswisi, mmoja kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Afrika (AU)
mjini Addis Ababa, Ethiopia na safari moja katika nchi zilizoathiriwa na Ebola
za Guinea, Liberia na Sierra Leone.
Imetolewa
na;
Kurugenzi ya
Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar
es Salaam.
4 Mei, 2015
0 comments:
Post a Comment