Katika mkutano wake wa 16 na 17, Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, pamoja na mambo mengine, lilijadili Taarifa ya Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali iliyotokana na Taarifa ya Ukaguzi wa
Akaunti ya Tegeta Escrow uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali.
Baada ya majadiliano, Bunge lilipitisha maazimio
kadhaa yaliyoelekezwa kwa Serikali kwa ushauri na utekelezaji. Mojawapo ya
maazimio hayo yalimtaja Ndugu Eliakim C. Maswi, ambaye ndiye Katibu Mkuu wa
Wizara ya Nishati na Madini, kuwa amehusika kijinai au kimaadili katika miamala
iliyotokea katika akaunti ya Tegeta Escrow.
Wakati anahutubia Taifa kupitia Wazee wa Dar es
Salaam tarehe 22 Desemba, 2014, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alisema
ifuatavyo:-
“Kuhusu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini,
kwa vile ni Mtumishi wa Umma, anatawaliwa na Sheria na Kanuni za Utumishi wa
Umma. Hivyo, nimeshaelekeza Mamlaka kuchunguza tuhuma zake na hatimaye
ikibainika ana makosa hatua za kinidhamu zitachukuliwa.”
Tuhuma dhidi ya Ndugu Eliakim C. Maswi
zimeshughulikiwa katika ngazi mbili tofauti. Amechunguzwa na Sekretarieti ya
Maadili ya Umma, kisha baada ya hapo alichunguzwa pia na Kamati ya Uchunguzi wa
Awali iliyoundwa na mamlaka yake ya nidhamu.
Sekretarieti ya Tume ya Maadili
Kifungu 18 (2) (c) na (3) cha Sheria ya Maadili ya
Viongozi wa Umma kinaipa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma mamlaka na
uwezo wa kuchunguza tuhuma yoyote ya kuvunjwa kwa maadili ya uongozi wa umma
yanayotawaliwa na Sheria hiyo. Tuhuma dhidi ya Ndugu Eliakim C. Maswi zilizomo
kwenye maazimio ya Bunge zinatawaliwa na Sheria hiyo.
Katika kutekeleza majukumu yake, Sekretarieti ya Maadili
ya Umma ilifanya uchunguzi wa awali na kisha kumhoji Ndugu Eliakim C. Maswi
tarehe 19 Desemba, 2014.
Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma
haijabaini kuwepo kwa maslahi binafsi katika uamuzi uliofanywa na Katibu Mkuu,
Wizara ya Nishati na Madini wa kuruhusu fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow
kutolewa. Aidha, hawakubaini ukiukwaji wowote wa maadili ya viongozi wa umma
uliofanywa na Ndugu Eliakim C. Maswi. Waliona kuwa yote aliyoyafanya
yalizingatia matakwa ya Sheria, ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja
na ridhaa ya TANESCO. Hivyo, Sekretarieti ya Maadili haikuona msingi wowote wa
kuendelea na shauri la Ndugu Eliakim C. Maswi, na wamelihitimisha.
Kamati ya Uchunguzi wa Awali ya Mamlaka ya Nidhamu
Kwa mujibu wa Kifungu 4(3) (d) cha Sheria ya
Utumishi wa Umma Na. 8 ya mwaka 2002 (kama ilivyorekebishwa) Katibu Mkuu
Kiongozi ndiye Mamlaka ya Nidhamu ya Makatibu Wakuu.
Kwa kuzingatia Azimio husika la Bunge, na kwa
maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Katibu Mkuu Kiongozi aliunda
Kamati ya Uchunguzi wa Awali dhidi ya Ndugu Eliakim C. Maswi, Katibu Mkuu wa
Wizara ya Nishati na Madini, chini ya Kifungu cha 36 cha Kanuni za Utumishi wa
Umma za mwaka 2003 kinachotamka ifuatavyo:-
“Where it is necessary to institute disciplinary
proceedings against a public servant, the disciplinary authority shall make
preliminary investigations before instituting disciplinary proceedings.”
Kwa mamlaka aliyonayo chini ya Kanuni 35(2)(b) na
Kanuni 37 ya Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2003, Katibu Mkuu Kiongozi
alimpumzisha Bwana Eliakim C. MASWI kutekeleza majukumu yake ya kazi ya Katibu
Mkuu ili kupisha uchunguzi wa awali. Uchunguzi wa awali ulifanyika chini ya
Kanuni ya 36 ya Kanuni za Utumishi wa Umma zilizotajwa, pamoja na Kifungu 4(3)
(d) cha Sheria ya Utumishi wa Umma Na. 8 ya mwaka 2002, kama ilivyorekebishwa.
Kwa mamlaka aliyonayo chini ya Kanuni zilizotajwa
kwenye ibara 3.3 hapo juu, Katibu Mkuu Kiongozi aliteua Kamati ya Uchunguzi wa
Awali na kuipa Hadidu za Rejea zifuatazo:
3.4.1 Kubainisha
wajibu na madaraka halisi ya Katibu Mkuu, Wizaraya Nishati na Madini, kwenye
uendeshaji wa TANESCO kwa ujumla, na hususan kwenye kufungua, kuendesha na
hatimaye kufungwa kwa akaunti ya Tegeta Escrow.
3.4.2 Kubainisha
na kupata maelezo ya kina juu ya kuhusika kwa Bwana Eliakim C. Maswi
katika mchakato na mtiririko mzima wa akaunti ya Tegeta Escrow, tangu
kufunguliwa hadi kufungwa.
3.4.3 Kubainisha
na kupata maelezo ya kina iwapo kuna jambo lolote ambalo Bwana Eliakim C. Maswi
alilifanya au ambalo alipaswa kulifanya lakini hakulifanya,
linalomstahilisha achukuliwe hatua za nidhamu.
3.4.4 Kubainisha
na kupata maelezo ya kina iwapo katika hatua yoyote ya mchakato na mtiririko wa
tangu kufunguliwa hadi kufungwa kwa akaunti ya Tegeta Escrow, Bwana Eliakim C.
Maswi alifanya jambo lolote linalodhihirisha matumizi mabaya ya mamlaka
yake kama Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, kwa namna iliyosababisha
hasara ya aina yoyote ile kwa Taifa la Tanzania.
Kubainisha na kupata maelezo ya kina iwapo katika
hatua yoyote tangu akaunti ya Tegeta Escrow ilipofunguliwa hadi
ilipofungwa, Bwana Eliakim C. Maswi hakuchukua tahadhari ya kutosha kulinda
maslahi ya umma na kusababisha kupotea kwa fedha za umma kwa uzembe au
matumizi mabaya ya madaraka.
Kubainisha iwapo kuna mahali popote katika mchakato
wa akaunti ya Tegeta Escrow ambapo Bwana Eliakim Chacha Maswi alifanya jambo
lolote linaloashiria kitendo cha kijinai, au kukiuka maadili ya viongozi wa
umma.
Kuandaa taarifa ya uchunguzi wa awali kwa msingi wa Hadidu
za Rejea zilizomo humu na kuiwasilisha kwa Katibu Mkuu Kiongozi. Taarifa hiyo,
pamoja na mambo mengine, ipendekeze hatua za kuchukuliwa kwa kila eneo ambalo
Kamati itabaini umuhimu wa hatua kuchukuliwa.
Mapendekezo ya Kamati ya Uchunguzi wa Awali
Kamati haijabaini kosa lolote ambalo linaweza
kusababisha Ndugu Eliakim Chacha Maswi, Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na
Madini, kufunguliwa mashtaka ya kinidhamu kwa kukiuka Sheria ya Utumishi wa
Umma Sura 298 ikisomwa pamoja na Kanuni zake za mwaka 2003 kwa kuruhusu Benki
Kuu ya Tanzania kutoa fedha zilizokuwa katika Akaunti ya Tegeta Escrow.
Hitimisho la Uchunguzi wa Awali
Uchunguzi wa Awali uliofanywa na Sekretarieti ya
Maadili umebaini kuwa Ndugu Eliakim C. Maswi hana makosa yoyote ya kimaadili
katika mchakato wa fedha za akaunti ya Tegeta Escrow.
Hali Kadhalika Uchunguzi wa Awali uliofanywa na
Kamati ya Uchunguzi wa Awali iliyoundwa na Katibu Mkuu Kiongozi umebaini kuwa
Ndugu Eliakim C. Maswi, “hakutenda au kuhusika na jambo lolote linaloashiria
vitendo vya jinai au kukiuka Maadili ya Viongozi wa Umma”.
Ushahidi wa vielelezo uliotolewa kwenye Sekretarieti
ya Maadili na kwenye Kamati ya Uchunguzi wa Awali umejitosheleza kuthibitisha
kwamba Ndugu Eliakim C. Maswi alitenda kazi yake kwa kiwango kinachoridhisha
kwa kufanya mawasiliano na mamlaka mbalimbali na kwa nyakati tofauti kwa lengo
la kuhakikisha na kujiridhisha kwamba kufungwa kwa Akaunti ya Tegeta Escrow
kunafanyika kwa usahihi.
Hakuna ushahidi wowote kuwa Ndugu Eliakim C. Maswi
alikuwa miongoni mwa waliopata mgao wa fedha au fadhila yoyote kutokana na
kufungwa Akaunti ya Tegeta Escrow.
Kwa nafasi yake ya mamlaka ya nidhamu Katibu Mkuu
Kiongozi, ameridhika kuwa Ndugu Eliakim C. Maswi hana makosa yoyote
aliyoyafanya katika mchakato wa akaunti ya Tegeta Escrow yanayostahili adhabu.
Hivyo, mchakato wa kinidhamu, kimaadili na kijinai dhidi yake umefikia mwisho
wake. Mwenye mamlaka ya uteuzi atatafakari taarifa hizi na kuamua cha kufanya
kuhusu ajira yake baadaye.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
8 Mei, 2015
0 comments:
Post a Comment