Tarehe 01/05/2014, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete aliunda Tume ya Uchunguzi kuhusu
malalamiko yaliyotokana na utekelezaji wa Operesheni Tokomeza. Aliteua
Makamishna watatu ambao ni Mhe. Balozi Jaji (Mst) Hamisi Amiri Msumi
(Mwenyekiti wa Tume), Mhe. Jaji (Mst) Stephen Ernest Ntashima Ihema (Kamishna),
Mhe. Jaji (Mst) Vincent Kitubio Damian Lyimo (Kamishna) na Ndugu Frederick
Kapela Manyanda (Katibu wa Tume).
Operesheni Tokomeza ilikuwa Operesheni iliyobuniwa
na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa lengo jema na muhimu la kupambana na
ujangili unaotishia urithi wetu wa wanyama pori, hususani tembo, faru, nyati,
twiga, pundamilia n.k.
Hadidu
Rejea kwa Tume
Kuchunguza
namna Operesheni Tokomeza ilivyotekelezwa;
Kuchunguza iwapo maafisa waliotekeleza Operesheni Tokomeza
walizingatia sheria, kanuni, taratibu na hadidu rejea walizopewa;
Kuchunguza iwapo maafisa waliotekeleza Operesheni
Tokomeza walivunja sheria, kanuni, taratibu na hadidu rejea walizopewa;
Kuchunguza iwapo kuna watu waliokiuka sheria yoyote
wakati wa utekelezaji wa Operesheni Tokomeza na iwapo hatua zilizochukuliwa na
maafisa wa Operesheni Tokomeza dhidi ya wakosaji hao na mali zao zilikuwa
sahihi;
Kupendekeza hatua zinazostahili kuchukuliwa dhidi ya
maaafisa wa Operesheni Tokomeza waliokiuka sheria, kanuni, taratibu na hadidu
rejea za Operesheni Tokomeza; na
Kupendekeza mambo yanayopaswa kuzingatiwa katika
kupanga na kutekeleza Operesheni nyingine kama hii ili kuzuia na kuepuka
malalamiko mengine kama yaliyotokea kwenye Operesheni Tokomeza.
3.0 Kukamilika
kwa kazi ya Tume
3.1 Tume
imekamilisha kazi yake na kukabidhi taarifa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, tarehe 10 Aprili, 2015. Kwa maagizo ya Rais tumeisoma
na kuichambua taarifa hiyo vya kutosha. Kwa hakika Tume imefanya kazi kubwa
sana, na nzuri sana ya uchunguzi na uandishi wa taarifa. Kazi imefanywa kwa
weledi na umakini wa hali ya juu na kwa lengo dhahiri la kutenda haki. Katika
siku 265, Tume ilitembelea wilaya 38 katika mikoa 20 na kuhoji jumla ya
mashahidi 259. Mikoa iliyohusika ni Kigoma, Katavi, Rukwa, Mbeya, Kagera,
Geita, Shinyanga, Simiyu, Mara, Lindi, Mtwara, Ruvuma, Iringa, Morogoro, Pwani,
Tabora, Singida, Manyara, Arusha na Tanga.
3.2 Tume
imejitahidi kuwahoji wote waliokuwa na malalamiko, kuwahoji mashuhuda, kuwahoji
watuhumiwa, na kukusanya ushahidi wa aina mbalimbali ili ama kuthibitisha
makosa pale yalipofanyika na kupendekeza hatua za kuchukua, au kujiridhisha
kuwa tuhuma na malalamiko hayakuwa ya msingi. Kazi hiyo imefanywa vizuri na kurahisisha
kazi ya Serikali ya kuchukua hatua zinazostahili.
4.0 Operesheni
Tokomeza ilivyotekelezwa
4.1 Tume
ilibaini kuwa katika kipindi cha mwezi mmoja cha utekelezaji wa Operesheni Tokomeza
iliyoanza tarehe 4 Oktoba, 2013, mafanikio mengi yalipatikana, ikiwemo:
Watuhumiwa 1,030 wa makosa mbalimbali yanayohusu
ujangili na uvunaji haramu wa misitu walikamatwa na kufikishwa kwenye vyombo
vya sheria;
Kukamatwa kwa meno ya 211 yenye uzito wa kilo 522,
meno ya ngiri 11, mikia ya wanyama mbalimbali 36, ngozi za wanyama mbalimbali
21, pembe za swala 46, mitego ya wanyama 134, ng’ombe 7,621 waliokuwa wanachungwa
ndani ya hifadhi na misitu, baiskeli 58, pikipiki 8 na magari 9;
Katika kipindi cha Operesheni kulikamatwa jumla ya
bunduki za kijeshi 18, bunduki za kiraia 1,579, risasi 1,964, mbao vipande
27,913, mkaa magunia 1,242, magogo 858 na misumeno 60.
Operesheni ilifanikiwa kupunguza kasi ya mauaji ya
tembo kutoka tembo wawili kwa siku hadi tembo wawili kwa mwezi wakati wa
Operesheni;
4.2 Operesheni
ilisitishwa rasmi tarehe 01/11/2013 ili kupisha uchunguzi wa malalamiko
yaliyojitokeza. Baada tu ya kusitishwa kwa Operesheni wafugaji wengi
wamerudisha mifugo yao katika maeneo ya hifadhi yaani Mapori ya Akiba, Hifadhi
za Taifa, Hifadhi za Misitu na Maeneo Oevu na ujangili ukaanza kurejea. Aidha
watuhumiwa waliokuwa wametoroka kukimbia Operesheni wameanza kurejea kwenye
makazi yao.
5.0 Vitendo
vya Ukiukwaji wa Sheria, Kanuni, Taratibu na Hadidu Rejea
5.1 Tume
imebaini kuwa katika utekelezaji wa Operesheni kulikuwa na matukio ya ukiukwaji
wa Sheria, Kanuni, Taratibu na Hadidu Rejea. Ukiukwaji huu umesababisha madhara
kwa wananchi mbalimbali ikiwemo vifo, madhara ya mwili na kadhalika.
5.2 Tume
ilichunguza matukio 15 ya vifo, na kuridhika kuwa vifo tisa (9) kati ya hivyo
vilisababishwa na mateso ambapo watendaji kwenye Operesheni walitumia nguvu kubwa
kupita kiasi dhidi ya watuhumiwa wakati wa ukamataji au kuhoji. Kabla ya vifo watu
hao walikuwa chini ya ulinzi wa askari wa Operesheni na kuna ushahidi wa
kitabibu (medical reports), ushahidi wa kimazingira na ushahidi wa kuona,
unaohusisha vifo vya marehemu hao na mateso kutoka kwa askari wa Operesheni.
Tume haikupata ushahidi wa kuhusisha vifo sita (6) vilivyobaki moja kwa moja na
Operesheni Tokomeza.
5.3 Tume
ilichunguza madai ya mateso yaliyosababisha madhara kwenye miili ya wahusika.
Walalamikaji walieleza Tume kwamba waliteswa ili waoneshe silaha au nyara
zilipofichwa au wakiri kujihusisha na ujangili au ujambazi na wataje washirika
wao wa mtandao wa ujangili. Kulikuwa pia na malalamiko ya udhalilishwaji.
Malalamiko hayo yalitoka kwenye wilaya ishirini na mbili (22) za mikoa
mbalimbali. Yapo matukio ambayo walalamikaji waliweza kuleta mbele ya Tume uthibitisho
wa kuteswa, na walionesha makovu na kutoa vyeti vya matibabu na PF 3 walizopewa
baada ya kuumia.
5.4 Tume
imebaini kuwepo matendo mbalimbali ya ukiukwaji wa sheria, kanuni, taratibu na
hadidu rejea uliofanywa na baadhi ya askari wa Operesheni na maafisa wengine
walioshiriki katika utekelezaji wake, ikiwemo matukio yanayoashiria rushwa na
udanganyifu mbalimbali.
5.5 Tume
ilishughulikia pia tuhuma za wizi, upotevu na uporaji wa mali. Walalamikaji wa
kundi hili walieleza Tume kuwa wakati wa utekelezaji wa Operesheni, waliibiwa
au kupoteza fedha na mali zao wakati na baada ya kukamatwa au kupekuliwa na
askari wa Operesheni. Tume ilichunguza jumla ya matukio ishirini na tatu (23) ya
aina hiyo na kubaini kuwa malalamiko mengi yalitokana na askari wa Operesheni
kutofuata sheria, kanuni na taratibu za ukamataji, kuhoji na upekuzi maungoni
mwa watuhumiwa na kwenye nyumba zao. Kasoro zilizoonekana ni pamoja na
kutoshirikisha viongozi au watu huru katika upekuzi na kutojazwa hati za
upekuzi mara baada ya upekuzi. Kasoro nyingine ni askari wengi kuingia kwenye
nyumba kwa wakati mmoja. Aidha, Tume imebaini walalamikaji wengine waliongeza
chumvi katika ushahidi wao kuhusu idadi ya mali na fedha zilizopotea au kuibiwa
na hivyo ushahidi wao kutoaminika au kuthibitika.
5.6 Tume
ilichunguza malalamiko ya kubakwa wakati wa utekelezaji wa Operesheni. Matukio
yaliyochunguzwa na Tume yalikuwa katika Kijiji cha Iputi, Wilaya ya Ulanga, Mkoa
wa Morogoro na Kijiji cha Mwantimba Wilaya ya Bariadi, Mkoa wa Simiyu na Wilayani
Sikonge. Hata hivyo wote waliodai kubakwa hawakujitokeza mbele ya Tume kutoa
ushahidi wao, hivyo Tume haikuweza kuchunguza malalamiko yao. Alijitokeza
mlalamikaji mmoja Wilayani Ulanga, Morogoro, lakini Tume haikuridhika na
maelezo yake, ambayo hayakutosheleza kubainisha kosa kwenye utekelezaji wa
Operesheni Tokomeza.
5.7 Tume
ilibaini kuwa wapo watuhumiwa waliofikishwa mahakamani na kutiwa hatiani na
wengine kuachiwa. Tume imeona kuwa hatua hii ilikuwa sahihi kisheria. Lakini
Tume ilibaini pia kuwa baadhi ya watuhumiwa hawakufikishwa mahakamani. Badala
yake maafisa wa Operesheni walijichukulia mamlaka ya kutoa adhabu kwa watuhumiwa
kama vile kukamata na kuzuia mali zao, kuchoma moto nyumba na mali zilizokuwa
kwenye maeneo ya hifadhi, kuua au kujeruhi mifugo iliyokutwa kwenye maeneo ya
hifadhi au kuuza kwa mnada ng’ombe waliokamatwa kwenye maeneo ya hifadhi. Hatua
nyingine inayolalamikiwa ni kuchukua bunduki zinazomilikiwa kisheria.
5.8 Tume imebaini
kwamba katika baadhi ya maeneo askari wa Operesheni walichoma nyumba moto kwa
madai ya nyumba hizo kujengwa kwenye hifadhi. Malalamiko hayo yalitoka katika
Wilaya za Mlele na Mpanda, Mkoa wa Katavi, Wilaya ya Momba, Mkoa wa Mbeya;
Wilaya za Nkasi na Sumbawanga, Mkoa wa Rukwa; na Wilaya ya Simanjiro, Mkoa wa
Manyara. Katika uchunguzi wa matukio haya Tume imebaini yafuatayo:
Wanakijiji hawakupewa taarifa ya kutosha kuhamisha
mali zao kabla ya kuchoma nyumba zao;
Baadhi ya wanakijiji walipoteza vyakula na mali zao
katika zoezi hilo la uchomaji moto;
Kuna vijiji vilivyosajiliwa lakini sehemu ya
vitongoji vyake viko ndani ya Hifadhi za Taifa;
Kuna maeneo ya hifadhi au ushoroba (buffer zone)
ambayo hayana alama za mipaka kati ya hifadhi
au ushoroba na vijiji husika;
Kuna nyumba ambazo hazikuwa kwenye eneo la hifadhi
au ushoroba na hivyo zilichomwa moto kinyume cha sheria.
Baadhi ya matukio na malalamiko ya kuchomewa moto
nyumba yalitokea kabla ya Operesheni.
5.9 Uchunguzi
wa Tume umebaini kuwepo kwa tatizo kubwa la wafugaji kutoka nje ya nchi na
wafugaji wenyeji kuingiza mifugo yao katika Mapori ya Akiba, Hifadhi ya Misitu,
Maeneo Oevu na Hifadhi za Taifa. Maeneo yaliyoathirika sana na tatizo hili ni
Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Pori la Akiba la Kigosi – Moyowosi, Pori la
Akiba la Maswa, Mapori ya Akiba ya Biharamulo – Burigi – Kimisi na Pori la
Akiba la Kijereshi.
Katika baadhi ya maeneo imethibitika kwamba wapo
ng’ombe waliouawa kwa kupigwa risasi baada ya kukutwa ndani ya hifadhi.
Aidha, Tume imeridhika kwamba kuna ng’ombe wa
walalamikaji waliokamatwa na kuuzwa kwa mnada. Uuzaji wa ng’ombe katika tukio
hili haukuzingatia utaratibu wa kisheria.
5.10 Tume
ilipata ushahidi kwamba katika maeneo mbalimbali askari wa Operesheni
walikamata au kuchukua bunduki, risasi pamoja na vitabu vyake hata kwa silaha zinazomilikiwa
kihalali. Maeneo ambayo yalikuwa na malalamiko ya watu kuchukuliwa silaha zao
ni mikoa saba (7) ambayo ni Katavi, Mbeya, Lindi, Morogoro, Tabora, Manyara na
Pwani ambapo jumla ya watu sitini na mbili (62) walijitokeza mbele ya Tume
kulalamika tukio hili.
6.0 Hatua
Zitakazochukuliwa na Serikali
6.1 Baada
ya kupitia kwa kina taarifa ya Tume, pamoja na mapendekezo ya Tume, Serikali
itafanya yafuatayo:
Hatua za kimashtaka zitaendelea kwa shauri la mauaji
ambalo upelelezi wake umekamilika na hatua za kiuchunguzi zitaendelea kwa
mashauri mengine nane (8) ya mauaji ambayo upelelezi wake haujakamilika;
Hatua za kisheria na kiutawala zitachukuliwa dhidi
ya watuhumiwa waliothibitika kuwatesa watu 15 wakati wa Operesheni;
Hatua za kiuchunguzi zinazofanywa na TAKUKURU kuhusu
tuhuma za rushwa na udanganyifu zilizothibitika zitaendelea;
Silaha zinazodaiwa kumilikiwa kihalali zitafanyiwa
uhakiki na ukaguzi wa kina kuhusu umiliki na matumizi yake na endapo hakutakuwa
na sababu nyingine za kisheria za kuzuia urejeshwaji, wamiliki warejeshewe
silaha zao kwa mujibu wa sheria na taratibu;
Mali ambazo zimethibitika kuchukuliwa wakati wa
Operesheni kwa tuhuma za kuhusishwa na uvunaji haramu wa mazao ya misitu
zirejeshwe endapo hakutakuwa na sababu za kisheria kuendelea kuzishikilia;
Serikali itafanya uhakiki wa vijiji ambavyo
vimesajiliwa na vimo ndani ya hifadhi ili kutatua migogoro ya ardhi kati ya
hifadhi na vijiji. Aidha, Serikali itahakikisha kunakuwa na ushirikiano wa
karibu kati ya Msajili wa vijiji au mamlaka husika na Wizara ya Maliasili na Utalii ili kuepuka
kusajili vijiji ndani ya maeneo ya hifadhi;
Wizara ya Maliasili na Utalii itatayarisha kanuni
zitakazoweka utaratibu wa kuwaondoa watu waliovamia na kujenga makazi katika
hifadhi;
Sheria zote zinazolinda maeneo ya hifadhi zitafanyiwa
marekebisho ili kuongeza adhabu kwa kosa la kuingiza mifugo kwenye Hifadhi bila
kujali uraia wa wamiliki wa mifugo hiyo;
Kwa vile Tume imejiridhisha
na faida kubwa na mafanikio ya Operesheni Tokomeza, Serikali
itaendelea na Operesheni kama hizo kadri itakavyojitajika
ili kuokoa maliasili za Taifa, ikiwemo wanyama, hifadhi na
misitu. Hata hivyo ushauri wa Tume juu ya kuboresha upangaji, usimamizi
na utekelezaji wa Operesheni hizo itazingatiwa kikamilifu.
7.0 Mawaziri
Waliojiuzulu
Tume ilijiridhisha kuwa Mawaziri wote waliojiuzulu,
yaani Mhe. Dkt. Emmanuel J. Nchimbi, Mb., Mhe. Balozi Khamis Kagasheki, Mb.,
Mhe. Mathayo D. Mathayo, Mb., na Mhe. Shamsi V. Nahodha, Mb., hawakuhusika moja
kwa moja na makosa yoyote ya utekelezaji kwenye Operesheni Tokomeza. Hivyo,
waliwajibika kisiasa tu na hakuna hatua nyingine inayostahili dhidi yao.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
8 Mei, 2015
0 comments:
Post a Comment