Aidha, Naibu Katibu Mkuu huyo amelitaka Jopo hilo
linaloangalia jinsi gani dunia inavyoweza kujiandaa na kukabiliana ipasavyo na
milipuko ya magonjwa kama Ebola katika siku zijazo, kuangalia sababu za msingi
za kusambaa kwa kasi sana kwa ugonjwa wa Ebola katika nchi za Afrika Magharibi
za Guinea, Liberia na Sierra Leone kulinganisha na kasi ya kusambaa kwa ugonjwa
huo katika nchi nyingine za Afrika zilizopata kukabiliwa na ugonjwa huo kama
vile Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Uganda.
Mheshimiwa Eliasson aliyasema hayo , Jumatano, Mei
6, 2015 wakati alipokutana na kuzungumza na Jopo linaloongozwa na Rais Kikwete
kwenye ofisi za Rais Kikwete kwenye Jengo la North Lawn Building katika Makao
Makuu ya Umoja wa Mataifa (UN) mjini New York.
Akizungumza na wajumbe wa Jopo hilo ambalo mbali na
Rais Kikwete wanatoka nchi za Brazil, Botswana, Indonesia, Uswisi na Marekani,
Bwana Eliasson amewataka wajumbe wa Jopo hilo kupendekeza jinsi ya kukabiliana
na magonjwa ya milipuko katika siku zijazo kwa sababu Ebola siyo ugonjwa wa
mwisho wa mlipuko kushambulia dunia.
“Nyie mnajua, kama mimi ninavyojua, kuwa katika
dunia ya leo kutakuwepo na mlipuko mwingine, kutakuwepo na mara
nyingine…itakuwepo Ebola nyingine ama ugonjwa unaofanana na Ebola. Hivyo, tunahitaji
maandalizi ya kiwango cha juu kupambana na hali hiyo itakapojitokeza. Lenu ni
Jopo linalojitegemea na hivyo tunaamini litakuja na mapendekezo ambayo yatatuwezesha
kukabiliana na hali hiyo,” alisema Bwana Eliasson ambaye ni raia wa Sweden.
Kuhusu kasi ya kusambaa kwa ugonjwa wa Ebola katika
nchi za Afrika Magharibi za Guinea, Liberia na Sierra Leone, Naibu Katibu Mkuu
alisema kuwa ni vyema na ni jambo la msingi sana kwa Jopo hilo kuangalia kwa
nini ugonjwa huo ulisambaa kwa kasi ya kutisha kuliko wakati mwingine wowote
katika historia ya miaka 40, tokea ulipogunduliwa kwa mara ya kwanza katika
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
“Tunajua kuwa nyie kazi yenu siyo kuchunguza ugonjwa
wa Ebola. Ugonjwa huu tunautumia tu kuweka msingi wa miaka ya mbele. Hivyo ni lazima kuangalia sababu za kiini
kabisa za kwa nini ugonjwa huo ulisambaa kwa kasi kubwa katika nchi hizo tatu.
Tunajua kuwa hizi ni baadhi ya nchi masikini zaidi duniani. Tunaambiwa kuwa
idadi ya waliofariki baada ya kupata ugonjwa huo ilikuwa ni asilimia 60. Lakini
kama ugonjwa huo huo ungelipuka katika nchi iliyoendelea kasi ya vifo ingekuwa
asilimia 25 tu.”
Mheshimiwa Eliasson alikuwa mmoja wa viongozi na
wataalam ambao tokea Jumatatu wiki hii wamekuwa wanakutana na kuzungumza na
wajumbe wa Jopo hilo ambalo liliteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa
(UN)Mheshimiwa Ban Ki Moon Aprili 2, mwaka huu, 2015.
Mheshimiwa Ban Ki Moon alilitaka Jopo hilo linalojitegemea
kupendekeza jinsi gani ya kuimarisha mifumo ya kitaifa na kimataifa, ili kuzuia
na kujenga uwezo wa kukabiliana ipasavyo na mabalaa ya kiafya, kwa kutilia
maanani mafunzo ambayo yametokana na mlipuko wa Ebola katika nchi tatu za
Afrika Magharibi ambao umeua watu karibu 10,000 katika muda mfupi.
Alhamisi, Mei 7, 2015 wajumbe wa Jopo hilo
wameshinda wamejifungia wakijadiliana wenyewe kwenye Kituo cha Utulivu (Retreat
Centre) cha Green Tree nje kidogo ya Jiji la New York.
Leo, Ijumaa, Mei 8, 2015 watakutana na kuwaelezea
juu ya kazi yao Wawakilishi wa Kudumu wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa na
baadaye Rais Kikwete atakutana na kuhutubia mkutano wa waandishi wa habari,
ikiwa ni kitendo cha mwisho cha mkutano huo wa kwanza wa Wajumbe wa Jopo hilo
ambalo watakutana mara sita kabla ya kuwasilisha Ripoti yao kwa Mheshimiwa Ban
Ki Moon Desemba mwaka huu.
Rais Kikwete na ujumbe wake, ataondoka mjini New
York jioni ya leo kwenda Algiers, mji mkuu wa Algeria kuanza ziara rasmi ya
kiserikali ya siku tatu katika nchi hiyo rafiki ya Afrika Kaskazini.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
8 Mei, 2015
0 comments:
Post a Comment