Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa
Jakaya Mrisho Kikwete na wanajopo wenzake mashuhuri duniani ambao wanatafuta
jinsi gani dunia inavyoweza kukabiliana vizuri zaidi na magonjwa ya milipuko
katika siku zijazo, leo, Jumanne, Mei 5, 2015, wamekutana na Wawakilishi wa
Kudumu katika Umoja wa Mataifa (UN) wa nchi
tatu za Afrika Magharibi ambazo zimeathiriwa na ugonjwa wa Ebola.
Rais Kikwete na wanajopo wenzake wamekutana na
mabalozi hao, ikiwa ni mwendelezo wa Jopo hilo, kukutana na kuwasikiliza watu
mbali mbali katika vikao vyake kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New
York kwa nia ya kupata maoni na mawazo ya watu hao, hasa wale wanaokabiliana na
ugonjwa wa Ebola katika nchi za Guinea, Liberia na Sierra Leone, nchi zinajulikana
kama wanachama wa Manu River Union.
Tokea Jumatatu, Mei 4, 2015, Rais Kikwete na
wanajopo wenzake kutoka nchi za Brazil, Botswana, Indonesia, Uswisi na Marekani
wamekuwa wanasikiliza watu mbali mbali, wakiwemo wataalam wa magonjwa,
madaktari na wasimamizi wa shughuli za kibinadamu katika maeneo ya majanga,
ikiwa ni maandalizi ya kutoa mapendekezo yao ya kukabiliana na magonjwa ya
milipuko katika siku zijazo kama walivyoombwa na Katibu Mkuu wa UN, Mheshimiwa
Ban Ki Moon.
Kwa maelekezo ya Mheshimiwa Ban Ki Moon wakati
anateua Jopo hilo, wanajopo wameombwa kutumia uzoefu na mafunzo yaliyopatikana
katika kubabiliana na ugonjwa wa Ebola katika kuandaa Ripoti yao ya jinsi ya
kukabiliana na magonjwa ya namna hiyo katika siku zijazo. Ripoti hiyo inatarajiwa
kukabidhiwa kwa Mheshimiwa Ban Ki Moon Desemba mwaka huu, 2015.
Mwakilishi wa Guinea katika UN, Mheshimiwa Balozi Mamadi
Toure amelieleza Jopo jinsi nchi hiyo iliyokuwa ya kwanza kugundua mgonjwa wa
Ebola ilivyojikuta katika hali ya kuwa na uwezo mdogo wa kukabiliana na balaa
la ugonjwa huo kwa sababu ya mfumo dhaifu wa sekta ya afya na miundombinu
iliyokuwa imesambaratika wakati wa miaka mingi, zaidi ya miaka 20, ya utawala
wa kijeshi nchini humo.
Balozi Toure ameeleza jinsi nchi hiyo ilivyokumbana
na vikwazo vingi mwanzoni katika kukabiliana na ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na
ukosefu wa elimu kwa wananchi, ujinga wa baadhi ya wananchi na hata kuingizwa
kwa siasa za upinzani katika jambo hilo ambako kulizuia ama kuchelewesha
waathirika kwenda ama kupelekwa hospitali.
“Wananchi wa Guinea walikuwa hawakuandaliwa kiasi
cha kutosha kukabiliana na ugonjwa huo ambao bado unaendelea katika nchi hiyo
na nchi za jirani za Liberia na Sierra Leone. Kwa sababu ya upinzani wa kila
aina na hasa wa kisiasa, ulitokea uhasama wa moja kwa moja wa wananchi kwa
maofisa wa Serikali na wahudumu wa ugonjwa huo. Baadhi yao walishambuliwa na
wananchi na kuna tukio moja ambako watu waliuawa,” amesema Balozi Toure.
“Ulikuwepo upinzani wa kisiasa na hata kidini, na
yote mawili hayakusaidia kuzuia kusambaa haraka kwa ugonjwa huo. Watu walikataa
kwenda hospitali kutibiwa, wagonjwa walifichwa ndani ya nyumba na hata watu
waliposhauriwa kuacha kula nyama ya wanyapori bado walikataa. Kwa hakika
ujinga, uongo na wananchi kudanganywa viliathiri sana jitihada za kukabiliana
na ugonjwa huo haraka zaidi.”
Balozi huyo, kama walivyosema mabalozi wenzake wa
Liberia na Sierra Leone, amesisitiza kuwa mwanzoni mwa ugonjwa huo hapakuwepo
na uratibu wowote na hakuna mtu aliyejua jinsi gani ya kukabiliana na hali
hiyo.
Hata hivyo, mabalozi wote watatu wamekubaliana kuwa
ushirikiano kati ya viongozi wa nchi hizo tatu kwa nia ya kukabili ugonjwa huo
kwa pamoja, umechangia sana kupunguza hali ya maambukizo ya ugonjwa huo katika
nchi hizo tatu.
Jopo hilo linaendelea na kikao chake mjini New York
leo.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
6 Mei, 2015
0 comments:
Post a Comment