Katika hafla hiyo ambayo pia
ilihudhuriwa na Balozi wa China nchini Kenya Bw.Liu Xianfa ,Rais Kenyatta
aliandamana na Naibu wake William Ruto ambapo walionyeshwa jinsi ujenzi huo
unavyoendelea,huku wakandarasi wa ujenzi huo ambao ni kampuni ya China ya CRBC
ikiwa inaendelea kujenga daraja refu lenye umbali wa mita 1987.69 katika mbuga
ya wanyama ya Tsavo ambapo treni itapitia ili kurahisisha uvukaji huru wa
wanyama mbugani.
Mwandishi wetu Khamis Darwesh
ametuandalia ripoti ifuatayo kutoka mji wa Voi nchini Kenya
Akizungumza wakati wa ukaguzi
wa ujenzi katika daraja la Tsavo,Rais Uhuru Kenyatta amesema ujenzi wa reli hii
utafungua fursa nyingi kwa nchi ya Kenya na nchi jirani.
Kenyatta amesema mradi huu
hautanufaisha tu wale wanaoishi maeneo ambayo mradi huo unapitia bali kila
sehemu ya nchi.
"Tunaamini ya kwamba huu
mradi utakuwa wa manufaa kwa wakenya wote.Huu mradi utatusaidia sisi kama
wakenya kupunguza bei za bidhaa mbalimbali kwa sababu tutapunguza gharama za
usafirishaji.Mradi huu utawezesha maeneo kama hapa Taita Taveta ambako kuna
madini kuweza kusafirisha madini kwa kutumia treni"
Aidha Rais Kenyatta
aliwapongeza viongozi wote pamoja na serikali ya China kwa kuwaunga mkono
katika utekelezaji wa mradi wa ujenzi ya reli.
Wakati huohuo Naibu Rais
William Ruto alisema reli inayojengwa sasa na kampuni ya China ya CRBC
itaongeza wepesi wa kubeba mizigo na watu kwa asilimia 50.
Naibu Rais William Ruto aidha
alisema kufikia mwaka 2017 ujenzi wa reli hiyo utamalizika na treni kuanza
kubeba abiria na mizigo.
Ruto alisema reli hii
itasaidia pakubwa katika kuongeza mapato na kupanua biashara na uchumi wa nchi
ya Kenya.
"Itawawezesha wakenya
kulipa gharama ya chini ya usafirishaji wa mizigo pamoja na abiria.Hiyo
itachangia pakubwa kuhakikisha ya kwamba mali inayotoka nje ya Kenya na zile
tunazokuza humu nchini ambazo zinasafirishwa kwenda nchi nyingine tutalipa
gharama ya chini,tutangeza mapato kwa wakulima wetu,na biashara itapanuka
pamoja na uchumi wa taifa letu la Kenya"
Balozi wa China nchini Kenya
Bw.Liu Xianfa amesema China iko mstari wa mbele katika kuimarisha uhusiano wake
na nchi ya Kenya.
Alisema mbali na ujenzi wa
reli hii unaotekelezwa na kampuni ya China ya CRBC wenyeji wa Kenya wananufaika
kwa nafasi za ajira na pia kupata fursa ya mafunzo kuhusu utaalamu wa uhandisi
hasa kuhusu ujenzi wa reli kutoka kwa wahandisi wa China wanaojenga reli hiyo.
"Nahisi faraja sana
kwamba kila wakati tunaona wakenya wengi zaidi hasa vijana na wanawake
wakihusika katika ujenzi wa reli hii.Kuna vijana wengi na wanawake ambao
wanafanya kazi na wahandisi wa China na kufunzwa kuhusu teknolojia za ujenzi wa
reli.Naamini ushirikiano wa aina sio tu kwamba utaimarisha mradi huu bali pia
utachukua fursa nzuri katika kuimarisha taaluma ya wakenya na waafrika katika
teknolojia ya ujenzi wa reli na kukuza uchumi wa Kenya na Afrika"
Bw Xianfa alisema wajenzi wa
China wanajali sana mazingira na uhifadhi wa wanyamapori ndiposa wakajenga
daraja kubwa na refu ili kurahisisha uvukaji huru wa wanyama mbugani,bila
kujali gharama kubwa za ujenzi wa daraja hilo.
Kwa upande wake Rais wa
kampuni ya CRBC Bw Lu Shan amesema kampuni ya CRBC inatilia maanani ubora
katika ujenzi wa mradi huo.
"Kampuni ya CRBC inajali
sana kuhusu ubora.Tuna mifumo mitatu ya uangalizi wa ubora,tuna kituo kikuu cha
uhandisi na vingine 17 vidogo. Tunakagua ubora wa mradi huu mara kwa mara ili
kuhakikisha ubora unaohitajika bila matatizo yoyote"
Tangu kuanza kwa ujenzi wa
mradi huu,wakenya wengi wamepata fursa za ajira.Kufikia sasa wakenya 10,889
wanahusika moja kwa moja katika ujenzi wa mradi huu,huku wengine 4,000
wakihusika japo sio moja kwa moja kama vile maajenti wa usafirishaji.
Kampuni ya CRBC ina mipango
ya kuwapatia mafunzo wafanyakazi wa kikenya kuhusu teknolojia ya reli na
uendeshaji ambao watasaidia wakati wa ujenzi na pia reli hiyo itakapoanza
shughuli.
Mradi huu
utakapokamilika,treni za abiria zitaenda kwa kasi ya kilomita 120 kwa saa huku
treni za mizigo zikienda kwa kasi ya kilomita 80 kwa saa.Hii itapunguza muda wa
kusafiri kati ya Mombasa na Nairobi hadi masaa manne na nusu kwa treni za
abiria na masaa manane kwa treni za mizigo.


0 comments:
Post a Comment