Uhaba wa mafuta ya petroli umezikumba sehemu mbalimbali
za Nigeria kutokana na mgomo ulioitishwa na wasambazaji wa mafuta, na kusema
watarudisha usamabazaji wa mafuta hadi serikali itakapowalipa malimbikizo ya
madeni yanayofikia dola bilioni 1. Kwa sasa uhaba wa mafuta sio tu unakwamisha
magari barabarani, bali pia umeanza kuathiri uchumi.
Uhaba wa Petroli, Dizeli na mafuta ya taa
unawaathiri karibu wanigeria wote, hasa wale wenye kipato cha chini wanaotumia
mafuta hayo. Lakini hata mashirika ya binafsi na ya umma pia yanaathiriwa kwa
kuwa yanatumia petroli na dizeli kuendesha jenereta zao. Mashirika ya umeme
ambayo pia yanategemea mafuta hayo kuzalisha umeme, sasa yamepunguza uzalishaji
wa umeme na kufikia megawati 1,327 ambacho ni kiwango cha chini kabisa katika
historia. Pamoja na kuwa wanigeria wengi wanatumia umeme unaotokana na
majenereta binafsi, uhaba wa mafuta umewafanya nao pia washindwe kutumia
majenereta yao.
Misururu mirefu ya magari na ya watu wakiwa na
madumu ya mafuta imekuwa inaonekana katika sehemu mbalimbali za Nigeria. Baadhi
ya safari za ndege za ndani zimekatishwa, na baadhi ya ndege za safari za
kimataifa zinalazimika kutua katika nchi jirani ili kuongeza mafuta. Uhaba huo
pia umefanya baadhi ya vituo vya Radio vya FM kutangaza kuwa vitasimamisha
matangazo, baadhi ya matawi ya benki na mashirika ya simu pia yamesema
yatasimamisha huduma zao.
Sababu ya upungufu wa mafuta nchini Nigeria imetajwa
kuwa ni mgomo wa wafanyakazi wa mafuta wanaodai malimbikizo ya madeni. Msemaji
wa shirika la mafuta la Nigeria Bw Ohi Olegbe amesema walikuwa na akiba ya siku
25, lakini uhaba uliopo umechochewa na mgomo huo. Amesema kutokana na mgomo
chama cha madereva wa malori ya mafuta PTD wamegoma kusafirisha mafuta, na
wanachama wa chama kikubwa cha wauza mafuta nchini Nigeria wamegoma kununua
mafuta kutoka nje. Kutokana na hali hiyo biashara haramu ya mafuta katika mji
wa Lagos imeanza kushamiri.


0 comments:
Post a Comment