Ametoa wito huo leo mchana (Ijumaa, Mei 29, 2015) wakati
akizindua kampeni ya kuandika wosia kwenye maadhimisho ya miaka 25 ya Chama cha
Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) yaliyofanyika katika viwanja vya Karimjee,
jijini Dar es Salaam.
Akizungumza mara baada ya kushuhudia uandishi wa wosia
mbele ya wakili, Waziri Mkuu alisema uandishi wa wosia ni suluhisho la migogoro
mingi inayosababishwa na wanandigu ambao wakati mwingine wala hawakushiriki
kuchuma mali wanayogombea.
“Kuandika wosia siyo uchuro kama ambavyo watu wengi
wanadhani… ninatoa kwa Watanzania kuandoak wosia mapema kwani inasaidia kuondoa
matatizo ya mirathi baada ya mmoja wao kuondoka duniani,” alisema.
“Mtua anapaswa kutamka mali nilizonazo ni kadhaa na endapo
nitakufa mali hii apewe fulani, na hii fulani na nyingine fulani. Hati hii
inapaswa kutunzwa kwa mwanasheria, benki au kwa Kabidhi Wasii. Tusipolifanya
hili, matatizo yataendelea kuwakumba wajane na watoto walioachwa na marehemu,”
alisema.
Aliipongeza TAWLA kwa kuchukua jukumu la kuhamasisha umma
kuhusu suala la uandishi wa wosia lakini pia akawataka wanachama wa TAWLA
wajikite zaidi kwenye kutetea haki za makundi maalum kama walemavu wa ngozi,
vikongwe na watu kutoka makabila madogodogo. “Haya makundi yana shida zao
ambazo hazifanani na watu wengine. Nendeni vijijini, mkatoe elimu, jueni
changamoto wanazokabiliana nazo, wasikilizeni shida zao na muone ni njia gani
mnaweza kuwasaidia,” alisema.
Akitoa mfano, Waziri Mkuu alisema katika kipindi cha miaka
nane kuanzia mwaka 2006 hadi 2014, jumla ya vikongwe 2,219 waliuawa katika
mikoa ya Geita, Simiyu, Mara, Kagera na Mwanza ambayo alisema yote iko Kanda ya
Ziwa. “Mauaji haya yanasababishwa na imani potofu za kishirikina; jamii
kuwa na uelewa mdogo wa sheria; ukosefu wa imani za kiroho; ukosefu wa elimu;
na waganga wa kienyeji kupiga ramli,” alisema.
Alisema makabila madogo yanakabiliwa na matatizo ya ardhi
ambayo ndiyo tegemeo lao kuu, vikongwe na watu wenye ulemavu wa ngozi
wanatishiwa usalama wa maisha yao bila sababu yoyote. “Nendeni mkatoe elimu
zaidi kwa watu hawa ili tuwalinde wazee wetu, makabila madogo kama Wahadzabe na
Wasandawe pamoja na ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi,” alisisitiza.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki
maadhimisho hayo, Mwenyekiti wa TAWLA, Bi. Aisha Bade alisema chama hicho
kimetumia wanasheria wanawake zaidi ya 200 na wasaidizi wa kisheria 400
(paralegals) kutoa msaada wa kisheria kwa watu mbalimbali ambao hawana uwezo
kumudu gharama za kesi.
“Katika mwaka 2014, tumetoa msaada wa kisheria kwa watu
zaidi ya 10,000 ambao hawana uwezo kumudu gharama za kesi kwenye mikoa
mbalimbali hapa nchini,” aliongeza.
Naye Balozi wa Sweden nchini, Bw. Lennarth Hjelmaker,
akizungumza kwa niaba ya wadau wa maendeleo nchini alisema Serikali ya nchi
hiyo ilitenga kiasi cha sh. bilioni 4 kusaidia mpango wa miaka minne wa chama
hicho wa kuimarisha utawala bora, uwajibikaji na usawa wa kijinsia.
“Hadi sasa tumekwishatoa sh. bilioni 3.5 ambazo kati ya
hizo, sh. bilioni 1.1 zimetumika kusaidia wanawake wapatiwe haki zao; sh.
milioni 500 zimetumika kutoa mafunzo kwa watumishi wa afya ili watoe huduma
rafiki za afya ya uzazi kwa vijana na sh. milioni 700 zimetumika kutoa mafunzo
kwa viongozi wa ngazi ya chini wanaohusika kutoa maamuzi. Kiasi cha sh. bilioni
1.2 kimetumika kuendeleza shughuli za chama,” alifafanua.
Pamoja na kutoa elimu kwa jamii na kutetea haki za
akinamama na wasichana, Balozi huyo wa Sweden alisema kuna haja ya kuweka mkazo
ili kuwafikia wanaume na wavulana wengi zaidi ili waweze kujirekebisha na
kubadili tabia na mitazamo yao dhidi ya wanawake na wasichana.
0 comments:
Post a Comment