Image
Image

Waziri mkuu: Tuwalinde vijana na dawa za kulevya *Azindua Jimbo la Mashariki Kanisa la Moravian *Ahimiza malezi mema kwa vijana, amani na umoja.


WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amewaomba viongozi wa dini nchini waitumie mikutano yao ya mahubiri kutoa elimu juu ya athari za dawa za kulevya kwa waumini wao na Watanzania wote kwa ujumla.

Ametoa wito huo leo mchana (Jumapili, Mei 3, 2015), wakati akizungumza na viongozi na waumini wa Kanisa la Moravian Tanzania kwenye ibada ya uzinduzi wa Jimbo la Mashariki la kanisa hilo uliofanyika makao makuu ya jimbo hilo, Mbagala Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

“Niwaombe sasa viongozi wa dini tuungane na Serikali kutoa elimu juu ya athari za biashara ya dawa za kulevya na matumizi yake katika jamii. Ninawasihi viongozi wa dini tuanzie makanisani na misikitini, na kwenye mikutano yote tunayoifanya; tusimalize mikutano yetu bila kutoa elimu kuhusu athari za dawa za kulevya kwa waumini wetu na umma kwa ujumla,” alisema Waziri Mkuu.

“Viongozi wa dini mna jukumu kubwa la kuwalea zaidi vijana ili wasijiingize kwenye matumizi ya dawa za kulevya kwa sababu wao ndiyo kundi kubwa zaidi miongoni mwa waumini wenu. Ninaamini tukishirikiana kutoa elimu hii pamoja, tutaweza kuwaokoa vijana wetu ambao ndiyo waathirika zaidi,” alisema.

Alisema jimbo hilo jipya linalojumuisha mikoa mitano ya Dar es Salaam, Morogoro, Lindi, Mtwara na Pwani lina jumla ya wakazi 9,817,207 kwa mujibu wa Sensa ya Makazi na Watu ya mwaka 2012. Pia lina ukubwa wa kilometa za mraba 190,646 sawa na asilimia 20.1 ya eneo lote la Tanzania.

“Kati ya wakazi hao, asilimia 56.8 ni watu wenye umri wa kufanya kazi yaani kuanzia miaka 15-64, wengi wao wakiwa ni vijana. Pia kuna asilimia 38.1 ambao ni watoto wenye umri chini ya miaka 15 na waliobakia ni wazee wenye miaka 65 na zaidi sawa na asilimia 5.1,” alisema.

Aliutaka uongozi wa kanisa utumie fursa zilizopo kwenye mikoa hiyo za kilimo, madini na gesi asilia kwa kuwahamisha waumini wake na kuwabadilisha kifikra ili wazitumie fursa hizo kujiletea maendeleo na kujikomboa kiuchumi.

Akizungumzia kuhusu mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwaomba viongozi wa dini washirikiane na Serikali kukemea kwa nguvu zote vitendo hivyo vya kikatili. “Tangu mwaka 2006 kumetokea mauaji ya watu 46 na kati ya hayo, matukio 43 yalikuwa kwenye ukanda ya ziwa na mikoa ya magharibi. Niwaombe tena taasisi zote za dini zitusaidie kuondoa au kubadili imani hizi za kishirikina miongoni mwa jamii. Ninaamini tukiunganisha nguvu zetu kwa pamoja dhidi ya fedheha hii tutashinda,” alisisitiza.

Mapema, akitoa mahubiri katika ibada hiyo ya uzinduzi, Askofu Kiongozi wa Kanisa la Moravian Tanzania (KMT), Dk. Isack Nikodemo aliwataka waumini wa Kikristo Tanzania waombe sana kwa ajili ya amani ya Taifa hili hasa katika kipindi hiki ambacho Taifa linajiandaa kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao.

“Kanisa la Tanzania kaeni magotini kwa Yesu, liitieni jina la Bwana kwa sababu amani inahitajika sana. Taifa la Tanzania liko safarini, linahitaji amani wakati huu kuliko wakati mwingine, hata kama mawimbi yatainuka kama mlima, mwiteni yeye naye atatuliza dhoruba zote,” alisema huku akinukuu neno kutoka kitabu cha Marko sura ya nne aya ya 35-41.

Alisema hata katika maisha ya kila siku, watu wanakumbana na safari za aina mbalimbali iwe ni kazini, kwenye ndoa au kwenye familia. Alionya kuwa ipo hatari ya kusafiri bila Yesu katika maisha ya mwanadamu.

Katika uzinduzi huo, Waziri Mkuu pia alitoa vyeti na nishani kwa Askofu mstaafu Lusekelo Mwakafwila na wachungaji wengine wanane pamoja na wazee wawili ikiwa ni ishara ya kanisa hilo kutambua mchango wao wa kueneza injili katika jimbo la Mashariki tangu likiwa chini ya Jimbo la Kusini.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment