Jana Waziri wa Fedha, Saada Mkuya aliwasilisha bajeti kuu ya Serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2015/16. Katika hotuba yake aliliomba Bunge liidhinishe jumla ya Sh22,495.5 trilioni.
Kama ambavyo tumeshawahi kusema siku za nyuma kuwa bajeti zetu si endelevu na hazilengi kufuata vipaumbele muhimu vya Taifa.
Kuthibitisha hoja hii, mwaka huu, fedha za maendeleo zilizotengwa ni Sh5,919.1 trilioni sawa na asilimia 26 ilhali fedha zilizoombwa kwa matumizi ya kawaida ni Sh16,576.4 trilioni sawa na asilimia 73.7.
Uthibitisho mwingine kuwa bajeti zetu hazina jipya hasa yanapokuja masuala ya kimaendeleo, tunaweza kuutoa kwa kuangalia bajeti ya mwaka unaoisha.
Fedha za maendeleo zilizotengwa zilikuwa Sh6.44 trilioni sawa na asilimia 32.4 tu ya bajeti, huku fedha zilizoombwa kwa matumizi ya kawaida zikiwa Sh13.4 trilioni sawa na asilimia 67.4 ya bajeti nzima.
Tayari wachambuzi wa masuala ya uchumi na wadau wa maendeleo wameshaikosoa bajeti ya mwaka huu wakisema kuwa haina jipya hasa katika upande wa mikakati ya kukuza uchumi wa nchi.
Lakini pia hotuba ya Waziri Saada haikutaja kwa kina utekelezaji wa mipango na mikakati mbalimbali ya kiuchumi iliyotajwa katika bajeti ya mwaka jana.
Mathalani sisi pamoja na wananchi kwa jumla tulitarajia kuona si tu Serikali ikitaja mazingira yaliyosababisha Deni la Taifa kupaa hadi Dola za Marekani 19.5 bilioni sawa na Sh35 trilioni kutoka Dola 18.7 bilioni mwaka jana, kuwa ni kushuka kwa thamani ya Shilingi dhidi ya Dola na malimbikizo ya riba ya madeni ya nje. Lakini pia tulitarajia kusikia Serikali ikionyesha namna deni hilo lilivyoleta tija si tu katika ukuaji wa uchumi wa nchi, lakini pia katika kuboresha ustawi wa mwananchi mmoja moja.
Tunasema hivi kwa sababu licha ya kuelezwa kuwa uchumi wetu unakua, bado umasikini umetamalaki kwa wananchi walio wengi.
Kuna ishara kuwa deni hilo limekuwa likiongezeka kwa sababu zaidi ya zilizotajwa jana ambazo ni ukopaji wa ovyo, ubadhirifu, matumizi yasiyo ya lazima na msamaha wa kodi kwa watu, mashirika, kampuni na taasisi mbalimbali.
Pia tuna shaka na ufanisi wa utekelezaji wa maeneo muhimu yaliyomo kwenye mpango wa maendeleo wa mwaka 2015/16 uliowekwa hadharani jana na Serikali.
0 comments:
Post a Comment