MAONESHO ya 39 ya Kimataifa ya Biashara yameanza rasmi jana huku
kukipigwa marufuku kuingiza bidhaa zisizo na nembo za ubora au
vifungashio bora.
Maonesho ya mwaka huu yatafunguliwa rasmi Ijumaa ijayo na Rais Jakaya
Kikwete huku kukiwa na banda maalumu la masuala ya elimu kumwezesha
kujua vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi na kupata wafadhili.
Siku hiyo ya jana baadhi ya washiriki waliendelea kupanga bidhaa zao
katika mabanda huku wengine wakimalizia ukarabati wa mabanda.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (TANTRADE),
Jacqueline Maleko alisema kuwa maonesho ya mwaka huu hawataki kuona
bidhaa zisizo na nembo, bidhaa feki pamoja na vifungashio hafifu kama
asali kuweka katika chupa za konyagi.
Maleko alisema pia wamepiga marufuku biashara ndogo barabarani hivyo
wameandaa sehemu yenye meza kwa ajili ya biashara hizo. “Pia hatutaki
mavuvuzela au vyombo vinavyotoa sauti ili kufanya kuwa maonesho ya
biashara ya kuwezesha watu kupata oda na siyo kuuza,” alisisitiza.
Alisisitiza kuwa ulinzi umeimarishwa kwa sehemu zote kuwa na vifaa
maalumu vya usalama ili kudhibiti wezi ma matukio mbalimbali. “Licha ya
kuwa vifaa hivyo vilikuwepo tangu mwaka jana lakini tumeviongeza kwani
mwaka jana tuliwakamata watu wawili kwa kutumia vifaa hivyo mmoja aliiba
simu na mwingine aliwaibia laptop wafanyabiashara wa nje,” alisema.
Alisema nchi ambazo kampuni zimeongezeka ni pamoja na Japan ambayo
ilikuwa na kampuni 10 lakini mwaka huu kuna kampuni 17, India, China,
Italia, Pakistani nchi nyingine kufikia makampuni zaidi ya 400.
Akizungumzia kuchelewa kupangwa kwa bidhaa mpaka jana yalipoanza
maonesho alisema mabanda mengi yaliyo wazi ni ya washiriki kutoka nje
ambao wanashiriki siku chache.
Alisema kawaida maonesho ya kimataifa ni siku nne au tano lakini haya
yanafanyika siku 10 hivyo wataanza kufika kuanzia Julai mosi mwaka huu
huku wale wa ndani alisema wamejenga tabia ya kuchelewa tu.
Maonesho hayo yanashirikisha nchi 25, kampuni zaidi ya 400 kutoka nje ya nchi na 4,700 za nchini huku kukiwa na wizara sita.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment