MBUNGE wa Mwibara,
mkoani Mara, Bw. Kangi Lugola,amelazimika kukatisha vikao vya Bunge
vinavyoendelea Mjini Dodoma na kwenda jimboni kwake, Kijiji cha Nambaza,
Kata na Tarafa ya Nansimo, wilayani Bunda, ili kushughulikia adha
wanayoipata walimu wa shule ya msingi kijijini hapo. Walimu
hao wanadaiwa kufanyiwa vitendo vya kishirikina kwa kuteswa,
kudhalilishwa hivyo kulazimika kuomba uhamisho ili wakafundishe shule
nyingine zilizopo mbali na jimbo hilo. Wakisimulia vitendo
wanavyofanyiwa, walimu hao walisema usiku wakiwa wamelala, wachawi
huwafuata na kuwanyoa nywele sehemu za siri, kuwaingilia kimwili,
kuwaibia mali pamoja na fedha zao. Walisema mbali ya vitendo
hivyo, pia wamekuwa wakikuta mikojo, ugali na samaki ukiwa umefunikwa na
shuka kitandani hali ambayo imewafanya washindwe kufundisha na kuomba
wahamishwe. Mwalimu Joyce Maugo ambaye ni mkongwe katika shule
hiyo, alisema walimu wa shule hiyo wako hatarini kutokana na vitendo vya
kishirikina wanavyofanyiwa ambapo mmoja wa walimu wa kike ambaye
kimaumbile ni mdogo, aliingiliwa kishirikina hadi akazimia. Alisema
asubuhi alipoitwa kwenda kushuhudia yaliyomkuta mwalimu huyo, alikuta
amefanyiwa mambo ya aibu akiwa hawezi kutembea ambapo kitandani kulikuwa
na damu, mikojo na kinyesi. Aliongeza kuwa, mwalimu mwingine wa
kiume, Pasco Mayamba, alikuwa amefunga milango na madirisha ya chumba
chake lakini asubuhi alipoamka, alikuta madirisha na milango iko wazi,
kitanda kimejaa mikojo, ugali, kipande cha mnofu wa sangara na mchuzi. "Wakati
mwingine tukila chakula usiku kinabadilika, kama ulikuwa wali na nyama
unakuwa ugali na dagaa au mboga za majani hali ambayo ni ya mateso
makubwa, kama kuna makosa tumefanya bora tuambiwe ili tuombe msamaha
badala ya kuendelea kututesa na kutunyima amani ya kazi na maisha,"
alisema Bi. Maugo. Mwalimu mwingine aliyefahamika kwa jina moja
la Lucy, alisema mbali ya kupata adha hiyo, wachawi hao huwaibia fedha,
vitambulisho, kadi za benki na mali nyingine na wakati mwingine hukuta
mikojo na kinyesi kwenye madebe ya unga na chungu cha mboga vitendo
ambavyo vinawanyima morali ya kazi. "Kuna wakati tunakuta vinyesi
madarasani jambo ambalo huwalazimu wanafunzi na walimu kuvizoa na
kufanya usafi...tunawaomba viongozi wa kijiji wachukue hatua dhidi ya
vitendo hivi," alisema. Akizungumza na gazeti hili Mjini Bunda,
Bw. Lugola alisema vitendo vya kishirikina wanavyofanyiwa walimu hao si
vya kufumbiwa macho bali vinapaswa kukemewa na wahusika wakibainika
wachukuliwe hatua kali kwani mbali na madhara wanayoyapata walimu ikiwa
ni pamoja na kuingiliwa kimwili, vitendo hivyo vinawadhalilisha na
kudidimiza maendeleo ya elimu jimboni humo. "Nimelazimika kwenda
Kijijini Nambaza kushughulikia tatizo hili na kesho (leo), nitafanya
mkutano wa hadhara na wananchi wa kijiji hicho ili kutafuta ufumbuzi wa
tatizo liweze kukoma lisitokee tena," alisema. Hivi karibuni,
wakazi wa kijiji hicho walifanya mkutano wa hadhara na kuwapigia kura
baadhi ya wanakijiji ambao wanadaiwa kuwa wahusika wakuu wa kufanyia
walimu hao vitendo vya kishirikina na kinara wa mambo hayo inadaiwa ni
kiongozi wa kijiji hicho ambaye anaishi jirani na shule hiyo. Katika mkutano huo, wanakijiji waliazimia wahusika hao wahame haraka kijijini hapo kabla hawajachukua sheria mkononi wakidai vitendo
wanavyovifanya mbali na kuvunja sheria vitasababisha shule yao ikose
walimu wa kuwafundisha watoto wao hali ambayo inaweza kusababisha
kijiji kukosa wasomi. Akizungumzia uamuzi wa kijiji hicho, Bw.
Lugola alisema anayaheshimu maamuzi hayo na kabla wananchi hawajafikia
hatua ya kuchukua sheria mkononi atawashauri watu hao wahame kijiji
hicho haraka. Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Joshua Milumbe, aliliambia
gazeti hili kuwa vitendo hivyo hawezi kuvivumilia kwani ni
udhalilishaji ambao Wilaya haiwezi kuufumbia macho hivyo lazima achukue
hatua. Alisema atakwenda Nambaza kuzungumza na wananchi wa kijiji
hicho ambapo kwa mamlaka aliyonayo kwa mujibu wa sheria, atachukua
hatua kali dhidi ya wote ambao watabainika kuhusika na vitendo hivyo vya
kihuni na kusisitiza atayaheshimu maamuzi ya wananchi. Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Bi. Lucy Msofe, alisema,
amesikitishwa na vitendo wanavyofanyiwa walimu hao ambao umri wao ni
mdogo ambapo huo ni ukatili wa hali ya juu. "Tayari nimelazimika
kumuhamisha mwalimu mmoja wa kike ambaye alifika kwangu akiwa na hali
mbaya kutokana na vitendo alivyofanyiwa na watu hao...kama hali hiyo
itaendelea, nitawahamisha walimu katika shule hiyo na kuwapeleka shule
zenye mahitaji kwa sababu huenda shule hii ya Nambaza haiwataki,"
alisema. Aliongeza kuwa, hayuko tayari kuendelea kushuhudia
watoto wa watu wakiendelea kuteseka, kunyanyasika, kudhalilishwa na
kufanyiwa unyama kiasi hicho akidai atawahamisha kama vitendo hivyo
havitakomeshwa.
This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
0 comments:
Post a Comment