RAIS Jakaya Kikwete amewaomba viongozi wa dini nchini kuendeleza hali
ya amani na utulivu uliopo nchini kwa kuhakikisha kuwa nchi inabaki na
amani, kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 25,
mwaka huu, 2015.
Aidha, Rais Kikwete amelishukuru Kanisa Katoliki nchini kwa
kuendeleza ushirikiano wake na serikali katika kutoa huduma za kijamii
na kusaidia kuleta maendeleo ikiwemo katika sekta ya elimu na afya.
Akizungumza katika sherehe ya kuadhimisha miaka miwili ya Upapa wa
Baba Mtakatifu Francis iliyofanyika Juni 26 mwaka huu, nyumbani kwa
Balozi wa Vatican nchini Tanzania eneo la Oysterbay Dar es Salaam,
alisema amani ya nchi ni lazima iendelee kulindwa.
“Naacha nchi yenye amani na utulivu, nchi ambayo inapitia katika
kipindi cha ustawi wa kiuchumi na kijamii ambao haujapata kutokea katika
historia ya Tanzania.
“Napenda pia kusisitiza kuwa hakuna binadamu aliyekamilifu. Kwa wale
ambao niliwakosea, naomba waelewe ukomo wa uwezo wa binadamu. Hakuna
asiyekosea.
Nimejaribu kwa kadri ya uwezo wangu, na nina hakika kuwa mrithi wangu
ataendeleza kazi nzuri ambayo nimeifanya katika miaka 10 iliyopita hasa
ile ya kujenga na kuimarisha uhusiano kati ya Dola na Kanisa,” alisema
Kikwete.
Alisema Dola na Kanisa ni taasisi zinazoendeshwa na binadamu,
inatokea wakati mwingine uhusiano kati ya taasisi hizo mbili ukapitia
katika mawimbi lakini ni uhusiano unaoendelea kuwepo na kuimarishwa.
Sherehe hizo ziliandaliwa na Balozi Askofu Mkuu Francisco Padilla na
kuhudhuriwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Kanisa Katoliki la Dar es
Salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo na maaskofu wengine wa majimbo
yote ya Katoliki ya Tanzania.
Katika sherehe hizo, Rais Kikwete pia alitumia nafasi hiyo kuwaaga
viongozi wa dini na wakuu wa Kanisa Katoliki akiwasisitizia kuwa anaacha
nchi yenye amani na utulivu na nchi inayopitia katika ustawi wa
kiuchumi na kijamii ambao haujawahi kutokea katika historia ya Tanzania.
“Kila miaka mitano, Tanzania hupiga kura kupata ridhaa ya wananchi ya
kuongoza. Makabidhiano ya madaraka katika Tanzania limekuwa ni suala la
amani na tunabakia mfano wenye kung’ara katika Afrika kwa kuruhusu
makabidhiano ya amani,” alisema.
Aidha alisema ana imani viongozi wa dini watashirikiana vyema na
kiongozi mpya atakayeteuliwa na kuendeleza mema yote aliyoyaacha pamoja
na kusimamia vyema mchakato wa uchaguzi na makabidhiano ya uongozi
vinakuwa vya amani.
Kuhusu miaka miwili ya uongozi wa Papa Francis, Kikwete alisema kuwa
kiongozi huyo ameleta matumaini mapya duniani, ujumbe mpya wa amani,
heshima kwa utawala wa sheria, amani na utulivu.
Vilevile ujumbe wake kuhusu changamoto nyingi duniani ikiwemo
tabianchi umeongeza sauti yenye nguvu sana kwa namna dunia
inavyoendeshwa.”
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment