TIMU ya Yanga yenye maskani yake mtaa wa Jangwani na Twiga, jana
iliifunga Friends Rangers mabao 3-2 kwenye mchezo wa kirafiki uliochezwa
Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam.
Yanga ambayo ilikuwa inawajaribu wachezaji wake waliosajiliwa msimu
huu, ilianza kupata bao la kwanza dakika ya 11 lililofungwa na Kpah
Sherman akimalizia pasi ya Busungu.
Hata hivyo, Friends Rangers walisawazisha bao hilo dakika ya 25
lililofungwa na Mussa Juma lakini dakika ya 37 Yanga waliongeza bao la
pili lililofungwa na Busungu baada ya kupokea pasi kutoka kwa Sherman
bao lililodumu hadi mapumziko.
Kipindi cha pili kila timu ilifanya mabadiliko ambapo, Yanga iliwatoa
Sherman, Geofrey Mwashaiya, Andre Countinho na kipa Benedicto Tinoco na
kuwaingiza kipa Ally Mustapha ‘Barthez’, Amis Tambwe, Simon Msuva na
Deus Kaseke.
Mabadiliko hayo yaliongeza mashambulizi kwani kila mchezaji
alijitahidi kuwafurahisha mashabiki waliokuwa wamefurika uwanjani hapo,
lakini mchezaji Cosmas Lewis wa Friends Rangers aliwanyamazisha
mashabiki baada ya kusawazisha bao dakika ya 83 kabla ya Busungu
kuifungia Yanga bao la ushindi dakika ya 88.
Friends Rangers ambao wanacheza ligi daraja la kwanza tena hawajaanza
mazoezi walionesha kandanda safi mbele ya Yanga ambayo imeanza mazoezi
takribani wiki mbili sasa, huku ikiwa na wachezaji wake wa kigeni.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment