Wachezaji kutoka klabu mbalimbali za hapa
nchini na nje wanatangazwa kusajiliwa na klabu mbalimbali, hasa zile kubwa
ambazo zina wadhamini na wafadhili wanaozifanya zionekane zina fedha.
Kipindi hiki pia ndicho kinachotawaliwa na
habari za migogoro baina ya wachezaji na viongozi wa klabu kuhusu mikataba yao
na stahiki zao. Wachezaji hulalamikia kutotekelezwa kwa mikataba yao kuhusu
malipo mbalimbali, kama fedha za usajili, pango na wengine huingia kwenye
migogoro na viongozi kwa kutaka fedha ili wasaini mikataba mipya.
Wakati mwingine migogoro hii huishia kwa
wachezaji kupoteza haki zao kwa kuwa wengi wao hawana ufahamu wa kutosha kuhusu
mikataba na pia hakuna chombo imara cha kuwatetea wakati wanaponyimwa haki zao
kwenye klabu.
Suala hili linazidi kuwa kubwa kwa kuwa
wachezaji hawana kimbilio na hivyo wanalazimika kuachia haki zao, na wengine
kulazimika kuachana kabisa na mpira wa miguu kwa kuuona kuwa hauna maana kwao.
Hili si jambo zuri hata kidogo kwa kuwa
linakatisha tama wachezaji na kufanya vijana ambao wana vipaji waamue kutafuta
vitu vingine vya kufanya na hivyo kuwaacha wale tu ambao wanaweza kuvumilia
kuporwa haki zao ndio waendelee kujishughulisha na mpira wa miguu.
Wakati huu tunashuhudia hayo, ni muda mzuri
kwa wachezaji kutafakari kuhusu haki zao na wanawezaje kuungana ili wawe na
chombo kimoja ambacho kitakuwa kikisimama imara kuwatetea pale wanapokuwa na
matatizo na klabu zao.
Tunajua kuwa kwa sasa kuna Chama cha Wanasoka
wa Tanzania (Sputanza) ambacho kina wajibu huo wa kuwasimamia wachezaji, lakini
kinashindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo kutokana na kutokuwa na fedha na
pia kuwa sehemu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Sputanza imeshindwa kuonyesha umuhimu wake
kwa wachezaji ambao nao wanashindwa kujihusisha nayo kwa kuona kuwa si muhimu.
Kwa maana hiyo ni muhimu kwa Sputanza kuanza
kutafakari nafasi yake katika kusimamia na kutetea maslahi ya wachezaji, hasa
kipindi hiki ambacho kinaonyesha wazi kuwa wachezaji wanahitaji msaada mkubwa
wa watu wenye ufahamu wa masuala ya sheria na mikataba ili wasidhulumiwe haki
zao.
Sputanza haitakiwi kusimamia wachezaji ambao
ni wanachama wake tu, bali isimame kutetea wachezaji wote na ndipo wataona kuna
umuhimu wa kujiunga na chama na hivyo Sputanza kuwa na wanachama wengi ambao
watakifanya kiwe na nguvu zaidi.
Hatuhitaji kuwa na sheria au kanuni mpya kwa
ajili ya kusimamia haki na maslahi ya wachezaji kwa kuwa tayari Shirikisho la
Kimataifa la Mpira wa Miguu (Fifa) lilishatengeneza kanuni imara ambazo
zinaweza kusimamia haki za mchezaji popote pale alipo ulimwenguni.
0 comments:
Post a Comment